Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia Hotuba ya Wizara hii muhimu sana katika ustawi wa wananchi wetu. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya katika nchi hii kwa kuwaondoa wananchi katika giza na kuwapeleka katika mwanga. Kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Kigoma na wa Muhambwe tunampongeza Rais kwa sababu ni yeye mwenyewe alifika Kigoma kwenda kuzima majenereta na kutuunganisha kwenye Gridi ya Taifa ili tuweze kupata umeme wa uhakika lakini umeme wa bei nafuu pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimpongeze Waziri wa Nishati na Naibu Waziri Mkuu kwa kazi nzuri anayofanya katika wizara hii ya kuendelea kutuletea umeme. Nimpongeze Naibu Waziri, Mheshimiwa Judith Kapinga kwa kazi nzuri anayoifanya tunamwona jinsi gani anapambana kuhakikisha kwamba wananchi wa Tanzania wanapata umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niendelee kuwapongeza watendaji wote, Katibu Mkuu Engineer Mramba, lakini Engineer Gisima na Watendaji wote walioko kwenye Taasisi za Wizara hii ya Nishati kwa jinsi ambavyo wanafanya kazi kuhakikisha kwamba wananchi wanapata nishati safi ya umeme kwa ajili ya ustawi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimesimama hapa kuipongeza Wizara hii ya Nishati kwa jinsi ambavyo imefanya kazi katika Jimbo langu la Muhambwe. Mimi ni mnufaika wa kupelekewa umeme katika vijiji, miaka mitatu ya kishindo ya Rais Samia Suluhu Hassan tumeweza kuunganishiwa umeme katika vijiji vyote 50. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwaka 2021 wakati nikiomba kura tulikuwa na vijiji saba tu na leo ninaposimama hapa vijiji 50 vyote vimekwishafikishiwa umeme katika Jimbo la Muhambwe. Kwa hiyo, kwa niaba ya wananchi wa Muhambwe tunampongeza sana Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali na Wizara ya Nishati kwa sababu imefikisha umeme katika vijiji vyote 50. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, isitoshe tumeshafikishiwa umeme kwenye vitongoji 223 kati ya vitongoji 420, ni karibu 50% ya vitongoji vyetu. Hii ni jitihada kubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha kwamba wananchi wake wanapata huduma ya umeme kwa sababu umeme ni uchumi, umeme ni fursa, umeme ni biashara ili tuweze kufanya shughuli mbalimbali kutokana na kuwa na umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata hivyo katika hili naomba nijielekeze kidogo kwenye changamoto tunayoipata. Changamoto tuliyonayo ni kweli umeme umefika kwenye vijiji vyote, lakini wote tunafahamu scope ya kusambaza umeme ilikuwa ni ndogo na hii nitatoa mfano katika Kata yangu ya Murungu ambayo kata nzima wameunganishiwa umeme wananchi 50. Kwa hiyo, unaweza ukaona kwamba pamoja na kwamba umeme umefika katika vijij vyote, lakini bado wananchi hawajafikiwa. Namwamini Engineer Hassan kule REA, anafanya kazi nzuri sana na hii kazi anaiweza. Tunaomba usambazaji wa umeme hasa umeme jazilizi…
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI:...katika umeme jazilizi ambao… (Makofi)
SPIKA: Taarifa inatokea wapi? Aaa! Mheshimiwa Dkt. Samizi kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Catherine Magige.
TAARIFA
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Spika, napenda kumpa taarifa mchangiaji hapo ameongelea changamoto kidogo, pamoja na sifa zote tunazoipa Wizara hii ya Nishati katika Wilaya ya Ngorongoro, eneo la Loliondo kuna changamoto kubwa ya umeme hata jana usiku ulikatika na leo asubuhi pia umeme umekatika.
SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Samizi unaipokea taarifa hiyo?
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Spika, ahsante naipokea taarifa ya Ndugu yangu Mheshimiwa Catherine.
Mheshimiwa Spika, naomba niendelee, umeme umefika kwenye vijiji vyetu na kwenye kata, lakini Taasisi zetu muhimu hazijapelekewa umeme. Misikiti yetu haijapelekewa umeme, Makanisa yetu hayajapelekewa umeme, kule kwangu Murungu, Lugongwe umeme haujafika kwenye Makanisa. Makanisa haya yana vyombo vya muziki, yana vyombo vya matangazo vinashindwa kufanya kazi na vinaharibika kwa sababu havina umeme. Shule zetu za sekondari na za msingi hazina umeme, shule hizi zina computer ambazo zinatakiwa zitumie umeme bado hazijapata umeme, Sekondari yangu ya Kumgogo haina umeme na Sekondari yangu ya Kumsenga haina umeme na ina vifaa vya computer. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niombe Wizara ije na mkakati maalum wa kuzisaidia hizi taasisi kwa sababu kama hizi Taasisi hazitapata umeme kwanza kelele zake ni nyingi. Pili, hizi Taasisi zina uhakika wa kuchangia hasa makanisa kulipa hizi revenue, lakini vyombo walivyonavyo vitaharibika. Niombe Wizara ije na mkakati maalum wa kusaidia hizi taasisi ziweze kupata umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, minara yetu ambayo tumejengewa minara ya mawasiliano Halotel na Voda haina umeme. Minara tunayo, lakini huduma za mawasiliano zinakuwa hafifu kwa sababu hatujapata umeme wa uhakika. Tunawaamini REA, tunamwamini sana Engineer Hassan aje na mkakati, tuliona kwenye mabanda angalau aje na hata huduma ya solar ya harakaharaka kwenye hizi shule kwa sababu huduma ya solar ni huduma ya mara moja, lakini pia ina gharama nafuu, ukishaweka mradi umeweka ili angalau hizi shule zipate umeme kwa haraka ili vifaa viendelee kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niendelee kumpongeza Naibu Waziri Mkuu na kwa kweli apokee maua yake kwa Mkoa wetu wa Kigoma na jinsi ambavyo ameendelea kutuongezea umeme, tumeshuhudia utiaji saini wa mkataba wa kujenga umeme megawatt 49.5 kupitia Mto Malagarasi. Hata hivyo, isitoshe tumeona tuna megawatt tano za solar katika Mkoa wetu wa Kigoma na Waziri ametuthibitishia ataongeza mpaka megawatt 10. Kwa hiyo, hii umetupa confidence na assurance kwamba Mkoa wetu wa Kigoma utaendelea kupata umeme wa kutosha na hii itatusaidia kwamba tuendelee kupata wawekezaji.
Mheshimiwa Spika, umeme wa Malagarasi umekuwa kwenye vitabu kwa muda mrefu lakini Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu amethubutu kuanza mradi huu kwa kweli apokee maua yake kwa maamuzi haya magumu ya kuanzisha huu mradi na nimeona kwenye ukurasa wa 49 amesema mradi huu utaisha mwezi Oktoba mwaka huu, tunampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwapongeze Wizara ya Nishati na Madini kwa maonesho waliyofanya kwenye viwanja hivi, kwa kweli imetusaidia sana kufungua macho na kuelewa vizuri Wizara hii. Nilibahatika kutembelea banda moja la Kampuni ya Kuzalisha Nguzo za Umeme za Zege Tanzania, TCPM. Kampuni hii inasimamia wazalishaji wa Nguzo za Zege kwa mikataba ya kushirikiana na nimeona Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu amesoma kwenye taarifa yake kwamba wameshafanya majadiliano na Taasisi Binafsi au wadau 17 ambao wameonesha nia ya kuzalisha nguzo, ni jitihada kubwa, tunaipongeza sana Wizara kwa kufanya jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nguzo za zege ni nguzo ambazo hazidhuriki na mvua, hazidhuriki na mchwa, hazidhuriki na mto, lakini ni rafiki wa mazingira. Tunafahamu jinsi ukataji wa miti kwa ajili ya nguzo unaleta madhara kwenye jamii yetu na hasa kuleta uharibifu wa mazingira. Nguzo hizi ni himilivu kwa maana kwamba hata dhoruba kama hii ya moto kama kule kwangu Muhambwe kwenye moto kichaa, watu wakiandaa mashamba wanachoma moto, ina maana nguzo hizo zitaendelea kusimama, lakini tumeshuhudia hata kule Rufiji pamoja na mafuriko yaliyotokea nguzo za miti zilianguka lakini nguzo za zege zilibaki zimesimama.
Mheshimiwa Spika, kwenye taarifa za Wizara hii inaonesha kwamba wanatumia takribani bilioni 80 kwa ajili ya kubadilisha nguzo zinazoharibika kila wakati. Ni pesa nyingi ambazo wangezipeleka kwenye zege, basi tungeondoka kwenye hiyo hali, nguzo hizi zina lifespan ya zaidi ya miaka 70 mpaka 100.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu kwa sababu nimeona ameongelea kwamba sasa kampuni hii itaenda kujengewa uwezo. Ijengewe uwezo kwa maana kwamba pamoja na kuingia mikataba na hizi Taasisi zingine yenyewe kama yenyewe ambayo ni Kampuni ya Serikali ipewe pesa nayo iweze kuzalisha nguzo kwa sababu gani? Itasimama katikati; kwanza, kusimamia ubora wa hizo nguzo; pili, kudhibiti bei lakini na pale TANESCO inapopata dharura au Tanzania hii itatoa nguzo hizi za zege kwa haraka na hatuwezi kuingia kwenye matatizo.
Mheshimiwa Spika, tunasema kila siku kwamba umeme ni usalama na kama umeme ni usalama basi tuwe na juhudi za makusudi kabisa kuiwezesha kampuni hii ya zege iweze kuzalisha kwa ajili ya usalama wa nchi yetu pale inapotokea kwamba tumepata shida. Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu kwenye taarifa yake amesema kwamba, moja ya changamoto tuliyokuwa nayo kwenye nchi kuhusiana na umeme ni uchakavu wa miundombinu na uchakavu wa miundombinu huo ni pamoja na uchakavu wa nguzo ambazo zinaoza na zinaliwa na mchwa. Kwa hiyo nimpongeze Naibu Waziri Mkuu kuliona hili na tunaamini kabisa kwamba sasa taasisi hii itawezeshwa ili iweze kuzalisha nguzo za zege. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, taasisi hii isiwezeshwe kwa hisani kwa maana inategemea Waziri gani yupo pale au Katibu Mkuu gani yuko pale. Kuwe na sheria, taratibu na sera ya kuisimamia ili yeyote mwingine asije na interest zake akaisema leo nguzo za zege mwisho kwa matakwa ya mtu binafsi kwa ajili ya kuilinda nchi yetu, lakini ya kuilinda taasisi hii, ni ukweli usiopingika kwamba Wizara hii imefanya kazi vizuri sana na tunaamini kabisa hizi changamoto ndogondogo ambazo wananchi wanalalamika watakwenda kuzifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa bei ya umeme, REA wanapokuja kutuwekea umeme wanaunganishia wananchi wetu kwa shilingi 27,000. Tunafahamu kabisa hata ilivyo mapambano kuzilipa hizo shilingi 27,000, lakini hata hivyo REA wanapoondoka TANESCO ikiendelea inaleta shilingi 300,000. Kwa kweli wananchi wetu hawawezi kulipia gharama ya 300,000, tunaomba Serikali iangalie upya i-review hizi bei ili shilingi 27,000 ya kuunganishia ibaki pale pale, kwa sababu walikuja na tathmini na ile tathmini jimboni kwangu kata kama tatu walisema ni mjini; Kata ya Bitulana, Kata ya Bitale na Kata ya Kumwambu.
Mheshimiwa Spika, tangu wamefanya tathmini wananchi hawajaweza kuunganishiwa umeme. Kwa hivyo haina faida ya kubaki na ile shilingi 300,000 na kama walifanya tathmini miezi sita ilishapita, si kosa ku-review na kuona palipokosewa na kubadilisha. Tunaomba turudi kwenye bei ya shilingi 27,000 katika majimbo yetu na vijiji vyetu ili wananchi waweze kuunganisha umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, pongezi nyingi sana kwa Wizara hii. (Makofi)