Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia Bajeti ya Wizara ya Nishati. Kwanza kabisa, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuongoza gurudumu la maendeleo katika Taifa letu, vilevile kutuongoza katika amani na utulivu. Mimi kama Mbunge wa wanawake kutoka Mkoa wa Tabora na wanawake wenzangu, baba zetu na kaka zetu tutasimama na Mheshimiwa Rais na tutatembea naye 2025. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napongeza hotuba nzuri ya bajeti iliyosomwa na Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati. Naipongeza sana Wizara nzima ya Nishati pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nishati Mheshimiwa Judith Kapinga kwa kazi kubwa anazofanya kwa kuhakikisha Wizara hii inaenda sambamba na mategemeo makubwa tulionayo wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi zote hizo, Mkoa wangu wa Tabora tuna changamoto kubwa sana ya umeme. Kama mikoa mingine ina changamoto za umeme, lakini kwetu naona tunaweza tukawa ni namba moja, tunaongoza na changamoto hizo zina sababu mbalimbali. Pamoja na changamoto hizo viongozi hawa, Mawaziri hawa wa Wizara hii, Naibu Waziri pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Nishati kaka yangu Doto Biteko wamekuwa pamoja na sisi mkoani kwetu kwa ziara mbalimbali. Hawajatuacha nyuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkoani kwetu tuna Miradi ya Ujenzi wa Vituo vya Kupozea Umeme, kimoja kimejengwa Sikonge, Kata ya Ipole na Urambo, Kijiji cha Umoja. Pamoja na ujenzi huo unaoendelea toka mwaka jana kwa vituo vyote vya wilaya zote hizo mbili tayari Mheshimiwa Naibu Waziri ameshakuja kwenye vituo hivyo. Alikuja Urambo kituo kikiwa kina asilimia 64 ya ujenzi, lakini haikuishia hapo Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, ambaye ni Waziri wa Nishati, naye amekuja mwezi Machi katika Wilaya ya Urambo kuangalia maendeleo ya vituo hivyo vya kupozea umeme ambavyo vikikamilika wananchi wa Mkoa wa Tabora, hususan Wilaya ya Urambo, Kaliua, Jimbo la Ulyankulu pamoja na Sikonge, watakuwa wamepunguza adha kubwa ya ukatikaji wa umeme. Umeme ambao hauna viwango vya kuwawezesha wananchi wa mkoa wetu kufanya shughuli zao mbalimbali hususan vijana na akinamama ambao wamejiajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati alikuja kukagua kituo hicho kuna jambo moja ambalo linaendelea ambalo halijakaa sawa. Naiomba Wizara, kuna suala la mkandarasi anayeleta line ya umeme kutoka Tabora kuja mpaka Urambo iende Kaliua, ambaye ni ETDCO, amesaini mkataba toka 2021, lakini mpaka sasa hivi ana 20% tu ya kazi hiyo ambayo ameifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa vituo vya kupozea umeme umeshafika 84%, karibu na kumalizika. Wanachokisubiri ni zile line zitoke Tabora kuja kufika pale Urambo, kisha aweze kuwasha kwa ajili ya majaribio. Kwa hiyo, unakuta mkandarasi B amekamilisha kituo na ameanza mwaka jana, ameshamaliza, lakini anamsubiri mkandarasi anayeleta line ya umeme kutoka Tabora kuja Urambo ambaye bado yuko kwenye 20%. Mkataba unasema anatakiwa akabidhi kazi Juni, 2024, lakini mpaka sasa hivi tuko Aprili, 2024, kazi bado iko kwenye 20%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara na Waziri wa Nishati, wananchi wa Urambo watafarijika sana kwenye hotuba yake, atakapokuwa amesimama hapa atwambie mkandarasi huyu ETDCO, ambaye ni kampuni tanzu ya TANESCO, wana mpango gani naye kwa ufanyaji kazi huu ambao hauridhishi? Anatuletea hasara kubwa kwa sababu, inabidi kumlipa mkandarasi ambaye ameshamaliza kazi yake, lakini inabidi amsubiri mkandarasi mzembe ambaye hajaifanya kazi yake kwa wakati kama inavyotakiwa. Kwa hiyo, inabidi tuendelee kumlipa, ili aendelee kuwepo site mpaka mkandarasi A atakapokamilisha. Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati akisimama hapo kuhitimisha, awaeleze Wanatabora waweze kujua hatima yao kuhusu umeme, lakini na huyu mkandarasi anayetuchelewesha ni nini hatima yake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kuipongeza Serikali na Wizara kwa ujumla kwa kazi ambayo wanaifanya kwa mradi mkubwa ambao tunao katika nchi hii, Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. Mradi huu umekuja kuwa ni mkombozi wa upatikanaji wa umeme wa kutosha katika nchi hii na tayari tunaambiwa mgao utapungua. Kama kuna mgao sehemu siyo kwa sababu, nchi haina umeme ila ni kwa sababu ya miundombinu ambayo ni chakavu na mvua nyingi ambazo zinasababisha nguzo kudondoka na hitilafu mbalimbali zinazojitokeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Wizara, kama tunafanya matengenezo ya line, tunabadilisha line hizi za umeme na tumeshatengeneza vituo vya kupozea umeme, basi naomba twende sambamba na ubadilishaji wa hizi nguzo za miti ambazo kwa Mkoa wangu wa Tabora nyingi zipo maeneo ambayo yana maji sana. Kipindi hiki cha mvua, Mwenyezi Mungu ametujaalia mvua ya kutosha, umeme unakuwa unakatika kwa sababu nguzo nyingi zinadondoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wakati yule mkandarasi anatengeneza line za kupeleka umeme, basi mkandarasi wa nguzo za zege naye awe anaanza ili ziende kwa pamoja ikiwa ni pamoja na kuhakikisha vituo vya kupozea umeme, ambavyo ilikuwa ni kilio kikubwa sana kwa mkoa wetu, navyo vimekamilika. Changamoto ikija kutokea tena kwamba, umeme umekatika kwa sababu tu maji yamejaa, wananchi hawatatuelewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanachohitaji ni umeme wa kutosha. Mwananchi hajui Bwawa la Mwalimu Nyerere na hasa ndugu zangu mimi tulioko Tabora, hatujui Bwawa la Mwalimu Nyerere kwa sababu haliko Tabora. Hatujui sijui nguzo zimekaa kwenye maji kwa sababu, sisi siyo wakandarasi, tunachotaka ni umeme wa kutosha. Hatujui kwamba, sijui line nazo zinatakiwa kufanyiwa service, tunachojua ni zile nyaya ambazo huwa zimewekwa zinatakiwa tu kuwepo milele na milele kwa hiyo, wao wanachotaka ni kuona umeme unawaka. Naishauri Wizara ijitahidi, inapofanya matengenezo ya line basi pia, itengeneze pamoja na nguzo za kupitishia nyaya za umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)