Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Momba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa, naomba nitumie nafasi hii kumpongeza na kumtia moyo Mheshimiwa Rais wetu kwamba, pamoja na watu wachache ambao siyo waadilifu kutweza utu wake ameendelea kuwa ni mtu ambaye amekaa kimya na kunyamaza. Nasema wakati mwingine kunyamaza ni ibada. Mwenyezi Mungu amsaidie aendelee kunyamaza ili ibada zake ziendelee kuwa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia nafasi hii kuishukuru Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kutusaidia kupata umeme kwenye vijiji vyote 72 ambavyo viko ndani ya Jimbo la Momba pamoja na kwamba, vitongoji bado, lakini vijiji vyote 72 kwa scope ya kilometa moja umeme unawaka. Pia, natumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu pamoja na timu yake yote bila kumsahau Naibu Waziri wake, hongereni kwa kazi nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa siku ya leo nina maneno machache tu. Nina maombi pamoja na ushauri. Ombi la kwanza, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu ambaye ni Waziri wa Nishati, alipofanya ziara pale Jimbo la Momba mwaka 2021 akiwa ni Waziri wa Madini, tulimpeleka kwenye Mradi wa Chumvi Itumbula, Ivuna, pale kuna chanzo cha majimoto. Kwa hiyo, katika hotuba yake umesema wanaviangazia hivyo vyanzo kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa umeme nchini. Naiomba taasisi ambayo inahusika na mambo haya ifike kwa ajili ya uchunguzi zaidi, kinaweza kikatumika kikawa chanzo kizuri cha umeme kwenye nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi la pili, ndani ya Jimbo la Momba tuna changamoto ya kupata umeme ambao siyo toshelevu, low voltage, kiasi kwamba inavunja moyo na kutokuakisi yale malengo ambayo Serikali imepeleka umeme vijijini, wakati mwingine hata watu ambao wanataka kuchomelea hawawezi kufanya hizo shughuli kwa sababu, umeme ni mdogo. Kwa hiyo, naomba jambo hili kwa Jimbo la Momba na maeneo mengine kama changamoto hiyo ipo tusaidiwe, ili lile jambo la umeme vijijini ambalo limekusudiwa liweze kuleta tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi la tatu ni ukosefu wa mita ndani ya Jimbo la Momba. Mimi mwenyewe toka nimejenga nyumba yangu kijijini kwetu Ihende mwaka 2022 sina umeme kwa sababu, hakuna mita. Sasa you can imagine Mbunge hana mita, wananchi wa kawaida hali ikoje? Wakati mwingine kutokana na jambo hili, vishoka wamekuwa wakiwadanganya wananchi kwamba watawaletea mita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri kwa Wizara juu ya mambo machache tu. Ushauri wa kwanza kwa Wizara ni namna ambavyo Wizara ya Nishati wanatoa taarifa. Ni kweli nia yenu kwa Watanzania ni njema, mfano, kama sasa hivi wametupa taarifa na siku wakati tunafunga maonesho yenu pale walisema kwamba, wamezalisha kiwango cha umeme kikubwa kuliko matumizi ambayo tunayataka. Naamini ni nia njema, lakini wakati mwingine taarifa hizi zinaenda tofauti na uhalisia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, turudi huko nyuma kipindi kile ambacho mvua bado hazijaanza, miezi mitano au sita kurudi nyuma, walikuwa wanasema kukatikakatika kwa umeme kunasababishwa na kukosekana kwa maji. Mvua zikaanza kuja kuanzia mwezi Desemba, Januari na Februari, wananchi mtaani wakaanza kuuliza, mbona mvua zipo za kutosha, zimezidi na zinaharibu miundombinu, lakini umeme bado unakatika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, wazungu wanasema kwamba, action speaks, matendo huongea zaidi kuliko maneno. Kwa hiyo, naomba waache actions zi-speak louder than words. Watekeleze kwanza halafu ndipo sisi tuanze kuona, kuliko sasa hivi wanatupa taarifa, wanatupa matumaini makubwa. Wakati mwingine taarifa za umeme nazichukulia ni kama taarifa za utabiri wa hali ya hewa, namna wanavyotoa taarifa za umeme, ndivyo watu wengine wanazichukua taarifa hizo wanaanza kuzifanyia kazi. Labda mtu anataka kufungua kiwanda chake, mtu anataka kuagiza samaki wengi, lakini taarifa zao zinavyokinzana na ule uhalisia kwenye jamii ndiyo mambo ambayo yanazua taharuki. Huku wanafanya wananchi wanakuwa wanaongelea hilo jambo na kuona kama Serikali ilikuwa inawahadaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaomba taarifa nzuri walizonazo ndani ya Wizara waende kwanza wakazifanyie action, halafu matendo yao yata-speak very louder na sisi tutaanza kujiuliza, mbona sasa hivi watu wa nishati wanafanya mambo mazuri? Kwa hiyo, taarifa zao zinakinzana na uhalisia ambao uko kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la ushauri ni kuhusiana na umeme kwenye vijiji. Ni kweli tunatambua kwamba, vijiji vyote vimepata umeme kwa scope ya urefu wa kilometa moja. Jambo hili kwa sisi tunaotokea vijijini wakati mwingine wananchi wamekuwa hawatuelewi. Unakuta urefu wa kilometa moja kijiji kingine kina urefu wa kilometa saba mpaka nane. Wakati mwingine wananchi inakuwa ni ngumu kuelewa kwamba, huu ni mkakati wa Serikali kwa hiyo sisi tuombe nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili liende kwa haraka kwa sababu, kule vijijini linaleta mpasuko na linawagawanya wananchi. Wakati mwingine wananchi wanakuwa wanafikiria watu wa kundi fulani ambao nguzo zimepita pale wamependelewa labda kwa manufaa fulani, kumbe hakuna hilo jambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba upelekaji wa umeme vitongojini kwa hizi scope za kilometa mbili ambazo wamekusudia kuongeza ziende kwa kasi ili kuwafikia wananchi kwenye maeneo mengine ambayo bado hawajapata umeme kwenye vitongoji. Pia, litaakisi uhalisia ule ambao tulikuwa tumesema tunataka kupeleka umeme vijijini. Kiukweli tuseme urefu wa kilometa moja tunaotoka huko vijijini ni mdogo na wakati mwingine wananchi hawatuelewi, ni ushauri wangu kwa Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la mwisho ambalo nimekusudia kuwashauri watu wa Wizara ni juu ya kukatikakatika kwa umeme. Tunafahamu inawezekana labda wakati mwingine umeme unakatika nje ya mipango ya watu wa Wizara, labda walikuwa na mpango fulani au wanataka kunusuru jambo fulani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, unakuta kuna mechi imetangazwa, Simba na Yanga, inajulikana itachezwa siku kumi mbele. Mtu amenunua kifurushi chake, amejitangaza pale mtaani labda ana kibanda umiza chake na amenunua vinywaji, mtu ana bar, watu wanaenda kuangalia mpira kwa sababu kile ni chanzo chake cha mapato, lakini unakuta TANESCO wanajua hilo jambo na wanajua kabisa watani wa jadi wanapocheza au mechi yoyote inapochezwa Watanzania hicho ndicho kiburudisho chao wanakifurahia, lakini TANESCO siku hiyo ndiyo wanakata umeme. Hata kama hilo jambo liko nje ya uwezo wao walishindwa kukata hata jana na juzi, leo wawavumilie wawaachie furaha yao iweze kutekelezeka! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine huko mtaani kuna notion ambayo inaonekana kwamba, wapo baadhi ya vigogo wa Serikali ambao wanafanya biashara za jenereta. Sasa wakati mwingine inapokuwa ni siku ya mechi au siku ya tukio muhimu umeme unapokatwa inaonekana kwamba, wale vigogo wa Serikali wanaongea na watu huko TANESCO kwamba, kateni umeme ili labda tuuze mafuta sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo amesema Mheshimiwa Jacquiline, wakati mwingine wananchi hawataki kusikia mambo mengi, wananchi wanachotaka ni kuona umeme, leo ni siku ya mpira wa Simba na Yanga tuangalie mpira. Sasa mtu amekusanya watu chumba cha kutosha, anajua leo atapata shilingi laki mbili alipe ada ya mtoto wake, TANESCO wanakata umeme na wanajua kabisa watu wanapenda mpira. Tunazua taharuki kwenye jamii, watu wanaendelea kuitukana Serikali na wanaendelea kuisema vibaya Wizara ya Nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunaomba waangalie na matukio. Tunaamini kwamba, wanaweza wakajipanga watoe taarifa kama ambavyo huwa wanatoa kwenye nyakati nyingine. Watoe taarifa, lakini wanakatakata umeme kupitiliza hata kwenye matukio ambayo ni ya muhimu, kiukweli hata mimi jambo hili huwa linanikera. Umekaa hapo na wananchi, sasa Mheshimiwa hebu ona, sasa mbona wanakata umeme, kwa kweli inatukera, tunaomba siku za mechi ya Simba na Yanga wasiwe wanakata umeme ili tuweze kufurahia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, nawapongeza sana watu wa Wizara ya Nishati. Naipongeza Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kwa namna ambavyo inafanya kazi vizuri. Nampongeza Mheshimiwa Rais wetu na tuendelee kumtia moyo kwamba, Mheshimiwa Rais wetu amejitahidi sana na amefanya kazi yake vizuri. Aliipokea nchi katika kipindi ambacho watu hawakufikiria kama angeweza kuifikisha nchi hapa, lakini amejitahidi amefanya zaidi ya kiwango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)