Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye hoja hii. Kwanza kabisa napenda kumpongeza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote walio katika Wizara hii kwa kazi kubwa na nzuri wanayofanya. Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko, tunamfahamu, utendaji wake tunaujua, kila Wizara aliyokabidhiwa imefanya vizuri sana. Kwa bahati nzuri sana amepewa Naibu Waziri kijana, yeye mwenyewe ni mtu ambaye anajiamini na mchapakazi, najua sasa wanaenda kufanya kazi vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti waliyoleta mbele yetu ni nzuri sana, haijapata kuonekana. Nimesoma kitabu chao, 95.28% ya fedha zote ambazo watapewa Wizarani zinaenda kwenye miradi ya maendeleo, haijapata kuonekana. Nampongeza kwa Wiki ya Nishati, kwa kweli walituonesha mambo mengi, wakatufungua macho. Nilifurahi sana nilipoona mikoa yote inaonesha ni kwa jinsi gani na kwa kiasi gani umeme umeweza kusambaa vijijini, kwa sababu kila mkoa, kila wilaya ilioneshwa ni vijiji vingapi vimeweza kupata umeme kupitia Mradi wa REA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakatuonesha pia na jinsi gani teknolojia imekua nchini maana yake tumeona hata magari yanayotembea kwa mfumo wa gesi. Vilevile, wakaweza kutupeleka kwenye Bwawa la Kufua Umeme la Nyerere bila kufika kule kwa kupitia virtual reality, tukaona jinsi ambavyo mradi mzima unafanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu mpendwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo ameendelea kutoa hela na kuwezesha miradi yote ya kimkakati kukamilika. Tukumbuke alipoingia madarakani huu Mradi wa Kufua Umeme wa Mwalimu Nyerere ulikuwa kwenye kama 30% hivi. Sasa hivi mradi umeshatekelezwa umefikia 95.8%, ahsante sana Mama Samia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi mtambo mmoja wameuwasha umeweza kuingiza kwenye Gridi ya Taifa megawatts 235 na ghafla mgao uliokuwa unawatesa wananchi ukapungua sana, karibu na kwisha. Tunasema Mama ahsante sana, yeye ana maono makubwa na nchi yetu. Sisi Watanzania tunampenda na tunasema, mitano tena. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kagera tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutuletea umeme vijijini. Kati ya vijiji 662 vilivyopo Mkoa wa Kagera vijiji 613 tayari vina umeme, tunasema ahsanteni sana. Kati ya vitongoji 3,365 vilivyopo Mkoa wa Kagera vitongoji 1,450 vina umeme. Hapo unaona kwamba bado tuko chini kwenye umeme katika vitongoji. Ombi letu kwa Serikali ni kwamba tunaomba waongeze bajeti ya kusambaza umeme mkoani Kagera ili vijiji vyote 49 ambavyo havijapata umeme vipatiwe umeme na vitongoji vyote viweze kupatiwa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wanakagera tunaamini kwamba umeme ni ajira, umeme ni fursa, umeme ni maisha, umeme ni maendeleo, tunachoomba kwako Mheshimiwa Waziri ni umeme. Tunaipongeza Serikali kwa ule mradi ambao ulikuwa unaendeshwa na nchi tatu: Tanzania, Rwanda na Burundi wa pale Rusumo Ngara, umekamilika na Tanzania tumeweza kupata megawatts 27, tunasema ahsanteni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kagera karibu wote unapata umeme kutoka Uganda. Huu umeme unakatika katika haijapata kuonekena unaweza ukakatika mara tatu au mara nne kwa siku. Kwa hiyo, watu wana adha kubwa kwa umeme huo ambao unakatika katika kila wakati, hii ni kwa sababu hatuko kwenye grid ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kile Kituo cha Nyakanazi kukamilika angalau sasa Wilaya za Ngara na Biharamulo zinaweza kupata umeme kutoka kwenye Kituo cha Nyakanazi, kwa hiyo wanapata kutoka kwenye grid ya Taifa. Uko Mradi wa Benaco - Kyaka, ule ndiyo unaweza kuwa mkombozi wa Mkoa wa Kagera kama utakamilika, kwa sababu utaweza kuingiza Wilaya za Muleba, Bukoba Vijijini, Bukoba Mjini, Misenyi, Karagwe, Kyerwa, wote wataweza kuingizwa kwenye grid ya Taifa na waweze kupata umeme wa uhakika na unaotosha ili waondokane na hii adha ya umeme kukatika katika kila wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tumebahatika, Mwenyezi Mungu ametupa vyanzo vingi ambavyo tunaweza kuvitumia kuzalisha umeme ikiwemo biomass, natural gas, hydro (maji), makaa wa mawe, geothermal, upepo, jua vilevile na madini ya uranium ambayo tunayo hapa nchini. Ukiangalia kwenye energy mix ya nchi yetu 63% ya umeme tunaupata kutoka kwenye natural gas, 32% tunapata kutoka kwenye maji, asilimia nne tunatoa kwenye mafuta na asilimia chini ya moja tunapata kwenye biomass. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza kwamba tujue tuna mabadiliko ya tabianchi. Kuna wakati ukame utakuwa mkubwa kwa hiyo vyanzo vya maji vinaweza vikakauka au maji yakapungua sana. Kwa hiyo, kuwa tunategemea maji 32% inaweza ikawa ni hatari. Napenda kuishauri Wizara kwamba sasa tuangalie upande wa nishati jadidifu, vyanzo jadidifu, zile renewables kama upepo. Ukienda pale Ujerumani utatembea kilometa nyingi, unaona yale mawimbi (panels) yanavyozunguka. Ukienda pale Morroco unaenda acres and acres of land unakuta zile solar panels wana-generate umeme mkubwa sana. Kwa hiyo, nashauri kwamba na upande huo tuangalie kwamba tuingize renewables kwenye energy mix ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, geothermal, nimeanza kusikia umeme wa geothermal bado nasoma shule nikiwa mdogo hadi leo bado wako kwenye utafiti. Wanasema wameshapata maeneo kama 50 ambayo yana hot springs, mahali ambapo kunatoka maji kwenye surface. Hata kwetu kule Kyerwa kuna sehemu inaitwa Mtagata maji yapo, kwa hiyo maeneo yanafahamika, basi wachimbe angalau tuone hata mradi mmoja uanze kuzaa matunda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa Mkutano wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa COP28 alizindua Mpango wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia. Analenga kwamba ifikapo mwaka 2034, Watanzania 80% wawe wanatumia nishati safi ya kupikia. Tunasema Mama ahsante jitihada tunaziona, tumepewa majiko, tumeenda tumegawa. Nilishuhudia Wizara wanagawa majiko kwa akinamama ntilie na akinababa ntilie. Wale watu wa kawaida kabisa wa chini zaidi ya 1,000 sijui elfu ngapi, wakawapa majiko banifu, majiko sanifu na mitungi ya gesi. Napenda kupendekeza kwamba tunaomba bajeti iongezwe kusudi mitungi zaidi iendelee kugawiwa. Vilevile, tuwashawishi wale wenye uwezo na wao waendelee kununua hiyo mitungi. Vilevile napendekeza kwamba hiyo gesi sasa ifike kule vijijini, kwa sababu mtu hawezi kutembea kilometa 20 mpaka 30 kwenda kujaza mtungi. Kwa hiyo tuhakikishe tunaweka system kwamba hiyo gesi itafika mpaka kule vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napendekeza kwamba sasa hivi bado bei ya gesi iko juu. Kwa hiyo, iwezekane waweze kuuza gesi katika ule ujazo mdogo ambao mtu wa kawaida anaweza kununua. Vilevile, ikiwezekana Serikali waweke ruzuku kwenye hiyo mitungi kusudi bei iteremke na kila mtu aweze kunufaika. Mwisho, tutoe elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ni nzuri, naomba wenzangu wote tuwaunge mkono, naunga mkono hoja. (Makofi)