Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Sylivia Francis Sigula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mungu Mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kuwa wazima wenye afya na tuko hapa tunajadili bajeti ya Wizara ya Nishati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa sana anayoifanya ya kutuletea maendeleo Watanzania. Nisibaki nyuma, nimpongeze Naibu Waziri Mkuu ambaye ni Waziri wa Nishati kwa kweli amefanya kazi kubwa sana, hotuba ni nzuri hata sisi wenyewe wachangiaji tunaona kama hotuba imesheheni kila kitu. Kwa namna ya pekee sana nampongeza Naibu Waziri wetu, Mheshimiwa Judith Salvio Kapinga, Mbunge kijana, Mbunge mahiri, Mbunge msikivu, anapokea simu, anajibu message na anatusikiliza sana Waheshimiwa Wabunge wenziwe. Nampongeza sana Mheshimiwa Judith Kapinga, sisi vijana wenzake ametuheshimisha, tunamupongeza sana, sana, sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa najielekeza kwenye mchango wangu na nitachangia maeneo mawili. Nitachangia upande wa gesi asilia, lakini pia nitachangia eneo la umeme. Kwenye gesi asilia hapa, nitazungumzia mambo mawili, nitazungumzia gesi ya magari, lakini pia nitazungumzia gesi ya majumbani. Mheshimiwa Rais alianzisha kampeni ya kumtua mama kuni kichwani, kampeni ambayo Wizara waliitendea vizuri, tumeona matamasha makubwa yamefanyika. Wananchi wamegawiwa mitungi ya gesi, Waheshimiwa Wabunge hapa, kila mmoja jimboni kwake ameenda kugawa mitungi ya gesi. Hakika hilo ni jambo kubwa sana ambalo limefanyika tunampongeza Mama Samia na pia tunawapongeza Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nilikuwa na ushauri kwenye hii gesi ya majumbani. Tunafahamu kabisa vipato vya Watanzania ni vidogo sana na tunafahamu kabisa wananchi wamehamasika na wako tayari kutumia nishati safi ya kupikia. Changamoto yao ni moja, kwanza, ni gharama ya hizi gesi. Pia, huko mitaani gunia la mkaa ni shilingi 20,000 mpaka shilingi 30,000. Leo ukienda mtaani kuna mkaa wa shilingi 2,000, ule mkaa wa shilingi 2,000 unatosha kupikia siku nzima. Naishauri nini hapa Wizara? Sisi kama Wizara inabidi twende mbele zaidi, kwa sababu Watanzania wamehamasika kutumia gesi. Tunatamani kuona tunakuja na mpango ambao hautamlazimisha mtumiaji wa gesi awe na shilingi 25,000 apate mtungi wa kilo sita. Tunatamani kuona mpango ambao hautamlazimisha mtumiaji wa gesi awe na shilingi 58,000 aweze kupata mtungi wa kilo 15. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatamani kuona, kama ilivyo kwa magari, leo mtu mwenye gari siyo lazima aweke full tank, unaenda petrol station na shilingi 15,000 unaweka mafuta ya shilingi 15,000, mafuta ya shilingi 20,000, mafuta ya shilingi 30,000. Tunatamani kuona tunakuja na mpango ambao tutapata ujazo tofauti tofauti ili watu wote, leo nikiwa na shilingi 3,000 nyumbani kwangu niweze kwenda kununua gesi ya shilingi 3,000 nipikie ikiisha nikanunue tena. Ukichukua hii shilingi 25,000 kwa mtungi wa kilo sita ni wastani wa shilingi 4,000 kwa kilo moja. Sasa kama mtu anaweza akawa na shilingi 4,000 akaenda kuweka kilo moja na akaweza kupikia hiyo itaturahisishia sana sisi Watanzania kuondokana na matumizi mabaya ya nishati na kwenda kwenye nishati safi ya kupikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija kwenye gesi za magari, tumeona Watanzania wamehamasika na naipongeza Wizara tumeona kwenye hotuba zaidi ya magari 3,000 yamebadilisha mfumo wa gesi. Tunasema, Watanzania wanatamani kuendelea kutumia gesi kwenye magari yao kwa sababu gesi ni gharama nafuu. Changamoto inakuja, tumeona mna mpango wa kuongeza vituo lakini bado vituo ni vichache, foleni inakuwa kubwa kusubiri gesi. Pia, bado vifaa vya kubadilishia mifumo ni gharama sana ambavyo vinafanya ubadilishaji wa mifumo uwe bei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukiwa na gari yako unataka kubadilisha mfumo kwenda kwenye mfumo wa gesi siyo chini ya shilingi milioni mbili, kwa hiyo, gharama hizi bado ni kubwa. Kwa hiyo, naishauri Serikali ione namna nzuri ya kufanya ili Watanzania wengi magari yao yafunge mfumo wa gesi. Tunaweza tukapunguza kodi kwenye vifaa hivi vya kubadilishia mfumo. Tunaweza kuwashirikisha wadau wa sekta binafsi wakawekeza katika mifumo hii ya kubadilisha magari yetu kwenda kwenye mfumo wa gesi, ili magari ya watu wengi yabadilishwe kwenda kwenye mfumo wa gesi, wapunguze matumizi ya mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejiuliza hapa, sijaona Serikali kama yenyewe ndiyo inasema inasimamia jambo hili, hamasa ipi inatupa kama Serikali? Wao kama Serikali ni magari mangapi ambayo tayari yana mfumo wa gesi? Wao kama Serikali wameanza kitu gani kutuonesha kwamba now wako serious na jambo hili. Kwa hiyo, ningependa sana kuona jambo hili linachukuliwa kwa uzito wake hasa na Wizara na Serikali kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia pia kuhusu umeme. Tumekuwa na phase nyingi za mabadiliko ya matumizi ya umeme. Tulianza na mafuta, tukaja na gesi kwa zaidi ya 65%, sasa hivi tumeenda kwenye maji, lakini ukiangalia gharama za umeme bado ziko juu. Leo kwa zaidi ya miaka mitano unit moja ya umeme bado bei ni ile ile. Tulitarajia kwa kuwasha mitambo hii ambayo imewashwa basi gharama za umeme zingepungua walau hata kidogo. Leo mwananchi ananunua unit moja kwa shilingi 350 lakini tulitarajia kwa sababu gharama za uzalishaji zimepungua, tunatarajia kuona na gharama za umeme zinapungua ili kuleta unafuu kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewaambia vijana wajitokeze, wafanye biashara, waanzishe viwanda vidogo vidogo, wanahamasika lakini bado gharama za umeme ziko juu. Kwa hiyo, tunamwomba sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati waliangalie jambo hili kwa kina. Tunatamani kuona vijana wengi wanafanya biashara, wanajiajiri, tunaomba waliangalie jambo hili kwa kina. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuendelea pia kwenye suala la umeme, umeme wa REA. Tumeona hapa kila Mbunge anayesimama anasema REA, wanafanya kazi nzuri lakini mimi binafsi nasimama hapa kwa masikitiko makubwa. Sisi wananchi wa Mkoa wa Rukwa bado jambo hili halijafanyika vizuri. Sisi wananchi wa Mkoa wa Rukwa bado tuna vijiji havijafikiwa na umeme. Sasa haiwezekani Wabunge hapa wanasema kwamba umeme umefika, tuna umeme mwingi mpaka mashine zinazimwa lakini bado sisi wananchi wa Mkoa wa Rukwa kuna vijiji havijafikiwa na umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mkandarasi Rukwa tumempa vijiji 141 na mkataba wake ulikuwa uishe tarehe 30 Mwezi Desemba, 2023. Mpaka inafika Mwezi wa Desemba bado hajakamilisha vijiji 40. Akaomba aongezewe muda, tumemwongezea muda mpaka Mwezi Machi, Mwezi Machi umefika bado vijiji vile 40 havijafanyiwa kazi. Sasa hivi tena kaomba aongezewe muda mpaka Mwezi Juni. Sasa haiwezekani, huyu mkandarasi JV Pomy Engineering and Qwihaya Enterprises wanatukwamisha sana Wanarukwa. Haiwezekani leo wananchi wanaambiwa umeme upo, umeme unatosha lakini kuna vijiji bado havijafikiwa na umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma maoni ya Kamati ya tangu mwaka jana na mwaka huu wanapendekeza hawa wakandarasi ambao hawafanyi vizuri Serikali ione namna nzuri ya kushughulika nao. Sisi wananchi Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu wala hatujui chochote tunachotaka ni umeme. Hatujui wao hawajalipana, tunachotaka ni umeme. Sasa huyu Mkandarasi tangu mwaka jana hajamaliza, ameongezewa muda hajamaliza. Wananchi mpaka leo hawana matumaini kama huo Mwezi Juni umeme utakuwepo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Sylvia unaweza kuhitimisha tafadhali.

MHE. SYLIVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu atakapokuja kutoa majibu ya hitimisho, sisi wananchi wa Rukwa tunataka kujua hatma ya hivi vijiji 40, ni lini hasa tutakuwa tumepata umeme wa uhakika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)