Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dr. Oscar Ishengoma Kikoyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu. Nampongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuliongoza Taifa letu kubwa na la kimfano Afrika na dunia nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze Wizara kwa kazi kubwa wanayoendelea nayo. Kuanzia kwa Waziri wake ambaye ni Naibu Waziri Mkuu, ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Biteko. Nimpongeze Naibu wake na watendaji wote wa Wizara, kwa kweli Wizara ina watu makini na wasikivu, tunashauriana tunasikilizana na kazi zinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza kwa miradi mikubwa ambayo inaendelea kutekelezwa ya kuzalisha nishati. Kama wengine waliotangulia kusema hatuwezi kujenga uchumi bila nishati hii muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Profesa Muhongo amechangia asubuhi na wengine waliochangia wameonesha umuhimu wa kuwa na Wizara hii na kazi kubwa waliyonayo. Kagera hatujaungwa kwenye gridi ya Taifa kama dada yangu Mheshimiwa Mushashu alivyosema, bado tuna hitaji kubwa na kilio chetu kikubwa ni kuunganishwa kwenye gridi ya Taifa. Umeme tulionao tunaupata kutoka nje, kama waswahili wasemavyo nguo ya kuazima haikustiri, kwa hiyo tunaiomba Wizara hii pamoja na Serikali yetu sikivu na pendwa, walituahidi Mradi wa Rusumo ukikamilika Kagera itaungwa kwenye gridi ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma kwenye bajeti kwamba Rusumo sasa imekamilika na nawapongeza Wizara, nimeona kwenye bajeti ijayo kwamba mradi sasa umeanza kutekelezwa, tunawaomba sasa waukamilishe na Kagera hasa baadhi ya wilaya ziweze kuungwa kwenye gridi ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama dada yangu Mheshimiwa Benardeta Mushashu alivyosema, nimeangalia takwimu tulizonazo Kagera vijiji ambavyo vimeungwa kwenye umeme ni 39% tu, tunaomba bado tuna kazi kubwa na safari bado ni ndefu kuhakikisha kwamba vitongoji vilivyobaki ambavyo havina umeme, sasa najua Wizara ina watu makini, naomba sasa hivi vijiji na vitongoji vyenyewe vikapatiwe nishati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kushauri kwenye hili kwamba tumekuwa tukisikia Waheshimiwa Wabunge wanapewa vitongoji 15, sijui vingapi tunapokuwa hapa, naomba kumshauri Mheshimiwa Waziri kwamba, hii sera nadhani ni nzuri inatuheshimisha kama Waheshimiwa Wabunge, lakini nadhani tuangalie ni wapi ambapo kuna mahitaji makubwa zaidi baada ya kila Mheshimiwa Mbunge kumpa vitongoji 15. Nadhani tukae kama Taifa tuangalie ni wapi pana mahitaji makubwa. Ukiangalia takwimu tulizonazo kwa Mkoa wa Kagera bado tuko nyuma sana, nadhani Serikali inahitaji kutupa jicho kubwa zaidi kuliko pale ambako labda huduma imeshasambaa kwa ukubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwenye Wilaya yangu ya Muleba. Muleba tuna vijiji vingi lakini kwenye taarifa tuliyonayo leo ni vijiji 12 havijapata huduma ya umeme. Najua kuna kazi zinaendelea, kuna baadhi ya vijiji vina wakandarasi, lakini baadhi ya wakandarasi kama mtangulizi alivyomaliza kusema, wanafanya kazi, wamepewa kazi na Wizara lakini kazi inaenda kidogo kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewasiliana na Watendaji wa Wizara, nilishalipeleka kwa Mheshimiwa Waziri, akatoa msukumo, Mheshimiwa Naibu Waziri amelipatia msukumo, kwenye maonesho yaliyopita, nashukuru tumeongea na watendaji wa REA na TANESCO, wamenihakikishia kwamba kabla ya mwezi Juni vijiji vyote vitakuwa vimepata umeme. Nina imani kwenye hilo kwa sababu nawaamini wana nguvu ya kufanya na wamekuwa wakifanya, nina hakika ifikapo mwezi Juni, Kijiji changu cha Kiholele ambacho kina mkandarasi, Kijiji cha Bihanga, Kijiji cha Burungura vitakuwa vimepata umeme na wenyewe waweze kufurahia matunda ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya yangu ya Muleba tuna Kata tano ambazo ziko visiwani, ziko off grid, naomba Waziri atusaidie tuweze kujua hawa wananchi ambao wako off grid, wako visiwani katika Wilaya yangu ya Muleba, naongelea Wilaya ya Muleba siongelei Jimbo, tunacho Kisiwa cha Ikuza, tuna Kisiwa cha Mazinga, tuna Kisiwa cha Bumbire, tuna Kisiwa cha Goziba, tuna Kisiwa cha Kerebe na hizi zote ni kata ambazo zinaunda kata tano kati ya kata 43 tulizonazo katika Wilaya ya Muleba. Kata hizi tunamwomba Waziri atupe mkakati wizara inafikiria kufanya nini ili na hawa wananchi wa hivi visiwa vyetu vitano, kata zetu tano waweze kupata hii nishati ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwetu pale Muleba tuna wakandarasi ambao walitoa huduma kipindi cha mwaka 2014/2015, lakini walipomaliza pale walimaliza kwa kutoelewana na Serikali na mkataba ulivunjwa lakini kuna sub contracts ambao walikuwa wametoa huduma kwenye hizi kampuni, kampuni yenyewe nadhani kama sijasahau ni Kampuni ya UR, wakaondoka lakini walituachia malalamiko na manung’uniko makubwa, watoa huduma waliokuwa wanawapatia huduma hiyo kampuni, waliondoka bila kuwalipa. Namwomba Mheshimiwa Waziri, wakati anahitimisha bajeti yake hapa, atuambie, hawa wananchi tunawasaidiaje ili waweze kupata pesa yao kwa sababu najua hii kampuni bado ipo na inaendelea kufanya kazi sehemu nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua mkataba ulikatishwa, lakini wananchi bado wanadai, kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Waziri, atusaidie tuweze kumaliza hayo manung’uniko ya hao sub contracts waliotoa hizo huduma, kazi ilifanyika lakini hawakupata malipo na wanadai hela nyingi sana kutoka kwa mkandarasi huyu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo suala la vitendea kazi katika wilaya yangu. Mheshimiwa Waziri anajua Wilaya ya Muleba ni kubwa na huku kwetu katika Mkoa wa Kagera inaitwa Kanda Maalum. Ni wilaya ambayo ina Kata 43, sasa ukiangalia wilaya yenye Kata 43 huwezi kuilinganisha na wilaya nyingine ambazo zina kata chache. Tunayo Majimbo mawili lakini tuna ofisi moja ya TANESCO na tunapogawa vitendea kazi tunaichukulia Kanda Maalum kama Wilaya ya kawaida lakini pale tuna Wilaya mbili. Hivyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, kwenye mgawanyo wa vitendea kazi, vijana wake wanafanya kazi kubwa na ni wasikivu, wanajituma kwelikweli, lakini wana tatizo la magari. Wana gari moja ambalo na lenyewe kusema kweli muda wake unaelekea ukingoni. Namwomba Waziri, hawa vijana wake ambao wanatufanyia kazi nzuri katika Wilaya ya Muleba, atusaidie wakapate vitendea kazi, awapatie magari ili waweze kuhudumia wilaya yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wilaya yetu pamoja na kuwa kubwa, lakini jiografia yake ni mbaya, kuna maeneo ambayo mvua zikinyesha huwezi kufika kwa mguu na huwezi kufika kwa magari ya kawaida, sasa hawa waangaliwe kwa jicho la namna ya pekee hasa kwa upande wa vitendea kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, niongelee suala la gesi. Naishauri Serikali, wenzangu waliotangulia wamesemea suala la gesi, ni kweli tunahitaji gesi na bei yake ni nafuu. Napenda Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja yake, atupatie elimu kidogo. Tuna mkakati gani kama Taifa kuhakikisha kwamba gesi ambayo Dar es Salaam tumeanza, lakini hii miji mikubwa hasa Majiji kama Mwanza, Mbeya, Arusha, tunawapelekeaje hii huduma ili kupunguza gharama ya nishati katika haya majiji makubwa ambayo wana magari mengi na msongamano mkubwa wa magari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jiji la Dar es Salaam peke yake, tumefanya kazi kubwa na nzuri ya kimajaribio tuangalie tunakuja na mkakati gani kuhakikisha kwamba Jiji lote la Dar es Salaam, Wilaya zote za Jiji la Dar es Salaam na wenyewe wanapata hii huduma kubwa na nzuri ambayo inapunguza matumizi ya pesa yetu ya kigeni kuagiza mafuta kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Nashukuru na nawatakia kazi njema. (Makofi)