Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote namshukuru Mungu kwa kunipa pumzi ya uhai na kuweza kusimama hapa leo kuleta hoja zangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo kila sababu ya kumpongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu ambaye ni Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Biteko, hakika hotuba yake imejaa na imesheheni kila jambo ambalo tungependa kulifahamu. Kipekee pia naomba kumpongeza sana Naibu Waziri wake Mheshimiwa Judith Kapinga, binti yetu ambaye hakika yuko makini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza timu nzima ya Wizara ya Nishati akiwepo Katibu Mkuu, Ndugu yetu Felchesmi Jossen Mramba na Naibu wake ndugu yetu Mataragio, pia timu yote naa idara mbalimbali zilizo chini ya Wizara hii ya Nishati. Imenipendeza kufanya hivyo baada ya kuona mambo makubwa waliyofanya. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa uteuzi huo na safu hiyo makini ambayo inatufanya leo tunasherehekea utendaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana, kipindi kama hiki, wizara hii iliomba shilingi 3,048,632,319,000, lakini hadi ninaposimama hapa nikizungumza, wameshapewa shilingi 1,813,026,147,056. Ni sehemu ndogo sana waliyopewa na tumebakiza miezi michache bajeti iishe, lakini kazi zilizofanyika ni nyingi na kubwa, sisi ni mashahidi, tumeona karibu wanakamilisha lile Bwawa la Mwalimu Nyerere na pia mambo mengine yamefanyika. Ombi langu ni kwa Waziri wa Fedha, ile hela iliyobakia sasa ilipwe, atakapoziona hizo certificates tunaomba alipe kwa sababu sisi ni mashuhuda, tumeona kazi imefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea, natamka wazi naunga mkono hoja na nawaomba wenzangu, tuwaunge mkono waweze kupatiwa ombi la mwaka huu, kwa sababu bajeti yao ina uhalisia. Nimetamka, waliomba shilingi trilioni tatu, mambo yamefanyika, mwaka huu wanaomba shilingi 1,883,759,455,000. Unaweza ukaona jinsi ambavyo hii bajeti ina uhalisia, nilitaka kuliweka hilo wazi. Naomba tuwaunge mkono na wapewe, wala tusianze tena kutaka ufafanuzi wa kushika shilingi ya Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia kwenye maeneo mawili, naanza na moja la TANESCO kuhusu huduma kwa wateja, nasema wazi kwamba tumependa mabadiliko yaliyofanyika TANESCO, tumeona kazi inayofanyika lakini umeme bado unakatika. Sitaki kufika kule kwangu maana yake ile lane yangu ndiyo mbovu kabisa, huko ninakoishi, nitarejea huko baadaye, lakini wametuambia katika kitabu alichosoma Naibu Waziri Mkuu, kwamba TANESCO wameboresha elimu kwa wateja ikiweko chat board yaani unawaeleza tu shida yako bila kupiga simu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kuna mfumo mwingine waliouleta TANESCO kuanzisha Mfumo wa Benki ya Taarifa na Elimu (Desa System). Sasa, tunaomba basi, hiyo elimu itolewe kwetu na pia kwa watu wetu. Tunaenda ku-desa vipi, maana yake kama kuna kitu ambacho kina shida na kinatesa na kichefuchefu, ni jinsi ambavyo tunavyoripoti kukatika kwa umeme, unaambiwa nenda lane fulani, mara inakata, wenyewe pia wanakatiwa umeme hukohuko walipo kwenye mitambo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo inakuwa kwa watu ambao wanakaa mbali kama vijijini, mtu analipa nauli anakwenda mpaka mjini kwenda kuripoti hatukuwa na umeme, labda ni hizi mvua zinazoendelea, ni transfoma ilikatika, lakini ni kitu chenye usumbufu. Wameeleza kama maeneo manne ambayo wanakwenda kurekebisha ili wateja tuweze kuwapata kwa unafuu zaidi. Naomba sana, hili jambo lifanyike na elimu itolewe tuweze kuwafikia TANESCO. Hata hapa, nadhani watu walio nje ya Dodoma wanadhani sisi ndiyo tunaopata umeme siku zote, hapana. Ile juzi wametueleza kwamba hii shida inakwenda kuisha, kwa hiyo tunatarajia hii shida iishe na mwakani tusisimame tena hapa kuzungumzia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalokwenda kuzungumzia, nalo naanza kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kumletea mwanamke nishati safi na salama ya kupikia. Hili jambo ni jema na naipongeza sana hii Wizara ya Nishati kwa sababu kwenye ukurasa wa randama, ukurasa huu wa tano, kwenye Project Code 3001 – 3002, wametenga shilingi bilioni nane kwa ajili tu ya hii clean cooking project na hela hiyo inatoka kwenye hela za ndani, kwa hiyo naona hili jambo linakwenda kuwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, walianza vema sana, walituletea REA, REA wakafanya kazi nzuri sana, wametupa mafunzo hapa lakini haikuishia hapo, REA ikatoa tenda. Mitungi ya gesi ikamwagika kutoka kwenye makampuni mbalimbali ambayo ni ya wadau. Tuliona mitungi ya Oryx kwa wingi sana, tukaona mitungi ya Taifa Gas, tukaona mitungi ile ya grey, majina ni mengi lakini Oryx iko kichwani kwa sababu aisifuye mvua imemnyeshea. Tuliiona hiyo mitungi na ipo mitungi ya rangi zote kijani, grey, manjano, Mihan na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu, hii hela iliyotamkwa hapa, ikaendeleze hayo mambo mazuri ambayo yameanza. Tuliona Wizara ikifanya kongamano lililofana sana hapa Dodoma na tukamwona Mheshimiwa Naibu Waziri akilisimamia na sisi wenyewe tukaona na tukashiriki, wanawake wanaendelea kusubiri. Mitungi hii siyo rahisi itolewe bure kwa kufuatia kaya zilizoko nchini zilizooneshwa na NBS, kwa sababu kaya zote zimeorodheshwa, vijiji, vitongoji, kata, wilaya na Serikali haiwezi kugawa zote, kwa hiyo lazima tunachangia, katika kuchangia huko, Waheshimiwa Wabunge tunachangia zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sasa, kadri tunavyoendelea kuboresha elimu au wanavyotuboreshea elimu, Wabunge wao tuko tayari kwenda kushusha elimu hiyo chini mpaka kwenye level ya kata na kaya. Bado nasisitiza mitungi hiyo isigawiwe bila elimu. Leo ukatokea mlipuko, watasema aah! ni vile vitu vipya vilivyoletwa vya gesi, kumbe hapana! Wapate elimu, hairuhusiwi, haikubaliki gesi kuleta maafa katika familia. Kwa hiyo, tuko tayari sisi kuendelea kuwa walimu wa walimu kama Waheshimiwa Wabunge waliopo hapa wote na pia tuko tayari kuendelea kugawa nishati hiyo kwa watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alitamka na akasema ifikapo 2034, angetamani kuona taasisi ambazo zina watu zaidi ya 100 watumie gesi hii. Wanasema her wish is a command, ametaka hivyo, hiyo ni ameshatamka, mamlaka imesema! Namba moja ikisema, wote inatakiwa tutekeleze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoomba, kutumia nishati hiyo inatakiwa pia miundombinu iwe imetengenezwa, kwa hiyo tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, aweze kuendelea kuzungumza vizuri na hawa wadau ili yale maeneo yenye watu zaidi ya 100 zikiwemo shule, maeneo ya kuishi watu ambao wana shughuli mbalimbali, vyuo, magereza, kokote kule ambako kuna watu 100 na zaidi, waweze kujengewa hiyo miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikishajengwa miundombinu, akatokea hapo mmoja mwenye roho nzuri, anaweza pia kupeleka hiyo gesi kwa kuanzia halafu mwendelezo ukawa ni kazi kwao. Tunajua na tunakubali kwamba hata huko Ulaya walianza kwa moto wa kufikicha lakini inapofika mahali…

(Hapa kengele ililia kuashira kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa naomba hitimisha tafadhali.

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na nilishaunga mkono hoja, lakini naunga tena mkono hoja na nawaomba wote tuunge mkono hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)