Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hii Wizara ya Nishati. Awali ya yote ni pongezi, nampongeza sana Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa kazi nzuri anayofanya, Naibu Waziri wa Nishati kwa kazi nzuri, Katibu wa Wizara na Naibu Katibu, Mkurugenzi wa REA na TANESCO, Wenyeviti wa REA na TANESCO wote wanafanya kazi nzuri, hongera sana kwao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, muhimu nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuwateua wote hao. Mheshimiwa Rais tunamwamini amefanya kazi nzuri na tunamwombea yeye aendelee kuwepo. Kuna vitu vingine vingi sana huwa najiuliza, unapomzungumza Mheshimiwa Rais labda kwa jambo fulani, jambo fulani, jambo fulani unashindwa kujua watu aliowaweka kwenye vitengo maalum ni watu thabiti. Kama leo tuna matatizo ya umeme nchini, tuhangaike na Mheshimiwa Dkt. Doto tu, kwa nini tunahangaika na Mheshimiwa Rais? Mheshimiwa Rais amemteua Mheshimiwa Dkt. Doto afanye hiyo kazi, tuhangaike naye humu ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama masuala ya kilimo tuhangaike na Mheshimiwa Bashe, kama ni suala la madini Mheshimiwa Mavunde yupo. Kwa hiyo sisi tunachosema ni kwamba Mheshimiwa Rais ametuteulia watu mahiri tuhangaike nao kama hawatendi kazi. Huo ndiyo ushauri wangu, nataka kuona kwamba unafanyika. Kwa hiyo Mheshimiwa Rais anafanya kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe ushauri mdogo kwa Wizara hii ya Nishati na hasa watu wa TANESCO na REA. Kumekuwepo na lugha ambazo hazifanani, hapa katikati tulikuwa tunasema Bwawa la Mtera mvua inanyesha maji hayajai, umeme haupo, tukapiga kelele tukazungumza mvua ikaja. Baada ya muda mfupi maji yakajaa umeme siku mbili umekatika hapa nchini, wanasema Bwawa la Mtera maji yamejaa, yanaharibu mifumo ya umeme, khaa! Sasa hayo maneno gani? Maji hayapo umeme hamna, maji yamejaa mifumo imeharibika. Kwa hiyo tuwe makini sana kwenye hili jambo la umeme na mimi niombe Mheshimiwa Waziri wa Nishati na bahati nzuri Mheshimiwa Rais amemteua amempa na madaraka mengine makubwa. Kwa hiyo haogopi mtu yeyote, wala hakuna anayemsogelea. waangalie watu wanaokaa kwenye vyanzo vikubwa vya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Bwawa la Mtera, Bwawa la Nyerere na maeneo mengine yote ambayo yanaongelewa kwenye maji, wangalie watumishi wanaokaa maeneo hayo kama wana muda mrefu kwenye maeneo hayo wawaangalie kama wanatenda kazi, kama hawatendi kazi wawapunguze kwa kuwapeleka katika maeneo mengine. Nasema hivi kwa sababu ni lazima wawe na lugha moja ya kuzungumza, siyo maji yajae umeme eti shida, maji yapungue umeme ni shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ni la ushauri, naomba ushauri wa Mheshimiwa Profesa Muhongo ufuatwe hasa umeme wa jua. Huko tunakoenda tumeshaona hivi vyanzo vya maji vina matatizo. Ni kweli tuna umeme megawatt 2,115 ya Bwawa la Nyerere, lakini huko nyuma tumeshaona mabwawa ya maji yanapungua na umeme unakosekana. Kwa hiyo niombe, tuone kwamba hivi vyanzo vya umeme vingine tofauti na vyanzo vya maji, tuone kwamba unapatikanaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine ninaoutoa muhimu sana kwenye REA, watuambie ni kweli 2025 vitongoji vyote vya Tanzania vitakuwa vimepata umeme? Je, ni mwaka 2025 au ni 2030? Lazima tuwe na lugha moja, siyo tunazungumza leo umeme 2025 vitongoji vyote vitakuwa na umeme, kumbe haiwezekani. Kama kuna mkakati wa kutosha wa kutengeneza vitongoji vyote vya Tanzania 2025 vitapata umeme tuambiwe ili twende kwa wananchi tuwaambie, siyo tunawaambia leo hiki kesho inakuwa tofauti. Kwa hiyo nilikuwa natoa ushauri huo ili tuweze kuuzingatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli watu walikuwa wanazungumza mara nyingi sana hapa. Ni kweli Mheshimiwa Naibu Waziri ametupa hotuba ya matumaini na Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba ni bora kutawala maskini mwenye matumaini kuliko kutawala maskini asiye na matumaini. Maskini mwenye matumaini ni yule ambaye ana kuku anakwambia nikope shilingi 1,000 nitauza kuku nikupe, nikope shilingi 2,000 nitauza mazao yangu nikupe. Maskini asiye na matumaini ni yule ambaye hana kitu chochote. Atakwambia nini umkopeshe alipe nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wametuaminisha hapa kuna umeme wa Bwawa la Nyerere, kuna umeme wa Rusumo, kuna umeme wa gesi asilia, tumeona, wametupa vyanzo vingi vya umeme na kweli hapa katikati umeme umepungua kukatika. Watupe uhakika huko tunakokwenda, watu hawahitaji vyanzo vikubwa vya umeme, hatuambiwi kwamba umeme megawatt 5,000 wakati hata hakuna umeme, haiwezekani. Lazima watuambie umeme unapatikana na unawaka, si umeme huu tumezalisha mwingi na huku umeme unakatika kila siku. Hilo nalo tuliangalie kwamba wametupa matumaini, kwa hiyo tunahitaji umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wamezungumza hapa vijiji, mimi huwa nafikiria jambo tofauti sana. Hivi unavyoniambia vijiji vyote 12 vina umeme ni sawa lakini vijiji ni nini? Vijiji ni vitongoji, kijiji kimoja kina vitongoji sita mpaka saba. Kwa hiyo kama kuna kijiji kimepata umeme maana yake ni kitongoji cha center chenye umeme, vitongoji vingine vyote havina umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwatolee mfano mimi nina Jimbo lenye vitongoji vingi katika kijiji kimoja. Kuna Kijiji kinaitwa Mariwanda kina Vitongoji 16, hakuna Mbunge hata mmoja hapa ana vitongoji vya namna hiyo haipo kwenye kijiji kimoja. Vitongoji 16 kijiji kimoja, vilivyo na umeme ni vitatu. Kuna Kijiji kina vitongoji 14, vilivyo na umeme ni vitatu, vitongoji 11 vilivyo na umeme viwili. Ni kweli nimepewa umeme na watu wa TANESCO na REA, hasa REA. Namshukuru sana Mkurugenzi wa REA na mwenzake anaitwa Olotu wanafanya kazi vizuri, lakini tuna wingi wa vitongoji kwenye maeneo ya vijiji. Kwa hiyo lazima tuangalie kwamba tuhangaike na vitongoji ili watu wapate umeme kwa eneo kubwa kuliko kusema tumemaliza vijiji, lakini kumbe kijiji kimoja kina vitongoji 11, kitongoji chenye umeme ni kimoja. Sasa hilo nalo tuliangalie vizuri huko tunakokwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni REA. Tusiende kufanya survey, twende tukafanye survey kabla ya kwenda kupima vijiji. Siku hizi REA walivyo wao maana yake wanakwambia bwana tumekuletea kilometa mbili kwenye Kijiji A. Ninachoshauri ni kwamba, waende kwanza wafanye survey kwenye eneo husika, wanaweza kukuta kuna shule inahitaji umeme kama umechukua nguzo nyingi, unaweza kukuta kuna kisima, unaweza kukuta kuna miundombinu mingine, inaweza kuwa idadi ya watu ni kubwa. Hiyo survey wanayoifanya ndiyo ikupe nafasi ya kutoa umeme kwenye kijiji kuliko ilivyo sasa, tunapeleka survey wakati tayari tunapeleka umeme kilometa tatu, survey haijafanyika na hilo limetokea kwenye maeneo yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Nishati maombi maalum, Kijiji cha Nyabuzume na Kijiji cha Nyaburundu tumewapa umeme wa migodi. Pale kuna dhahabu nyingi sana zimetoka Nyabuzume na Nyaburundu, wanapeka kilometa 1.5. Wahitaji wa umeme huo ambao ni watu wa migodi wanahitaji kilometa tano at least. Kwa hiyo naomba Nyabuzume tuwape kilometa tatu na Nyaburundu tuwape kilometa tatu za kuanzia, tafadhali namwomba sana Mheshimiwa Waziri. Tunahitaji hela, watu ni maskini hata kama hiyo dhahabu imetokea nyingi Nyabuzume, tunamwomba Waziri tafadhali awasaidie kwenye hiyo nafasi waweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii miradi ya umeme tunayokuwa tunaizunguza hapa tumekuwa nayo kwa muda mrefu na tuna mikakati. Wananchi unapozungumza habari ya kwamba miundombinu ni mibovu, kitu gani ni kibovu, hiki, hiki ni kibovu hawaelewi. Nimeona bajeti ya 2016 tumeweka bajeti na mikakati, 2017/2018, 2018/2019 mpaka leo ukisoma hiyo Hotuba yetu ya Nishati ina mikakati mingi sana. Tunaimarisha miundombinu, tunaimarisha hiki, tunaimarisha hiki. Ifike muda tuwaambie Watanzania hata kwa umeme walionao sasa, hata bila kuongeza mwingine basi inatosha kufanya hiyo kazi. Watu wanateseka, viwanda vinakuwa havina umeme, ukienda viwandani wanalia, watu wazima wanalia, mama ntilie wanalia na kila mtu analia, hapana ifike mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nawaza hivi, Naibu Waziri Mkuu anapatikanaje? Nilikuwa nawazawaza hilo. Nikaangalia nikaona 1985 Mheshimiwa Salim Ahmed Salim alipewa Unaibu Waziri Mkuu, sasa nikajiuliza alipewaje? Kumbe kipindi hicho nchi ilikuwa na matatizo mengi, kulikuwa na uchumi mgumu akateuliwa kusaidia nchi ikaenda ikasaidika kidogo. 1993 Mheshimiwa Mrema alipopewa kulikuwa na ujambazi wa kutupa kwenye nchi yetu akasaidia saidia mambo yakaisha yakaenda. Tamaa zake zikampeleka huko alikoenda lakini alisaidia nchi ikaenda ilikokuwa inaenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa imekuja mwaka huu amepewa Mheshimiwa Dkt. Doto, amepewa kwenye wakati ambao umeme ni shida kwenye nchi yetu. Umeme na Nishati ni shida kwenye nchi yetu, tumeona kwa kipindi kifupi walichonacho amepeleka at least mgao wa umeme umepungua. Kwa hiyo nafikiri kwamba kumbe Manaibu wanapewa kwa kazi maalum. Namwombea Mheshimiwa Dkt. Doto, afanye hiyo kazi. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, ahsante sana.