Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Bajeti ya Wizara ya Nishati na nimeshawahi kuwa Mjumbe kwenye Kamati hii na kwa kweli niwapongeze sana. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati lakini pia nimpongeze rafiki yangu ambaye alikuwa Mwenyekiti wetu wa Wabunge Vijana Bungeni Mheshimiwa Naibu Waziri Judith Kapinga, kwa kweli anatuheshimisha sana vijana wenzake kwenye Bunge hili. Pia, niwapongeze kwa kweli wote, Makatibu Wakuu, ndugu yangu James Mataragio, tulikuwa naye kule amekuwepo tangu kipindi hicho na tunaendelea kushirikiana naye vizuri, kwa kweli wanafanya kitu kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitachangia zaidi sana katika eneo moja. Nitachangia energy mix (nishati mchanganyiko) kuelekea nishati jadidifu 100% (Energy Mix in Transition to 100% Renewable Energy) katika nchi. Kwa kweli kwanza nipongeze sana, nimesoma Hotuba ya Mheshimiwa Waziri na nimesoma na maoni ya Kamati na nimeona na wao wamezungumza kuhusiana na energy mix. Kwa kweli energy mix ndiyo suluhisho na kwa sababu jana tulijadili Bajeti ya Wizara ya Mazingira na kuna baadhi ya vitu ambavyo ndiyo maana tunakubaliana na suala la nishati mchanganyiko (energy mix) kwa sababu hakuna anayetabiri nini kitatokea baada ya muda fulani kwenye masuala ya mabadiliko ya tabianchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa namna moja au nyingine athari za mabadilko ya tabiachi leo tulikuwa tunazungumza Hydroelectric Power Plant ya Mwalimu Nyerere ambayo ni megawatt 2,115, bado sisi hapa wote hatujui nini kitatokea miaka miwili, mitatu ijayo. Pengine panaweza pakakauka pale na hatuombei, lakini kwa sababu tunasema mambo yanabadilika kila siku hatujui. Kwa hiyo energy mix ndiyo solution kuelekea 100%. Kwa sababu nchi yetu imeridhia pamoja na nchi nyingine kwenye kuhakikisha tunapunguza ongezeko la joto duniani na kuendelea ku-maintain 1.5 Celsius ongezeko la joto duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo miongoni mwa jitihada zote unazozifanya ni pamoja na kuhakikisha kwamba tunahamia kwenye renewable energy nchi zote. Mimi hii naichukulia kama fursa kwenye nchi yetu kwa sababu na sisi mwaka jana pia tumesaini Mkataba wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu wa IRENA pamoja na kwamba tulichelewa lakini pia ni kitu kizuri kwamba nchi imeona ni wakati mwafaka wasaini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimesoma document kadhaa. Nimesoma An Outlook of Tanzania’s Energy Demand Supply and Costs by 2030. Pia, nimesoma Analytical Study on National Energy Policy and Regulation Frame Work in Tanzania, Technical Report ya Power Shift Africa na hii pia nyingine ni ya Power Shift Africa lakini ni African Development Bank Group ambao wamefanya Research zao. Pia, nimesoma Energy Development Plan to Re-carbonize the Economy ya upande wa Tanzania peke yake ambayo pia imefanywa na Power Shift Africa na kwa kweli kwa kusoma hizi nakubaliana na maelezo ya Mheshimiwa Profesa Muhongo asubuhi kuhusiana na wakati tunazungumza energy mix ni lazima tuangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu eneo moja la hydroelectric power ni eneo moja, lakini tukizungumza nishati jadidifu tunazungumza pamoja na umeme wa upepo, tunazungumza pamoja na umeme wa jua, lakini tunazungumza geothermal. Kwa sababu nafahamu kila Serikali inayokuwepo madarakani kwa namna moja au nyingine ni lazima Kiongozi wa nchi awe na mtazamo kuhusiana na jambo fulani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata mimi nasema hivyo kwa sababu hata mimi ningekuwa kwenye nafasi fulani kwenye hizi kubwa za juu ambayo ina impact kwenye maamuzi ukiachana na nafasi zetu za Ubunge, ningetamani na mimi nibakishe kitu ambacho watu watanikumbuka nacho. Kwa hiyo nitoe wito kwa Washauri wa Mheshimiwa Rais, miongoni mwa vitu vya kufanyia kazi kwa kiwango kikubwa sana ni kuhakikisha tunapata umeme ambao ni reliable kwenye nchi kama ambavyo tulianza na hatua ya kutengeneza Mradi Mkubwa wa Mwalimu Nyerere ambaye mtangulizi wake aliweka. Basi sehemu ya pili ya kutumia fedha zote ikiwezekana na fedha za mabadilko ya tabianchi ambazo tunazihitaji, basi Waziri atafute fedha na tuandike miradi tupate fedha kwa ajili ya ku-fund miradi ya umeme wa upepo na miradi ya umeme wa jua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nieleze tu kama nchi tuna baraka mimi naziita baraka. Tanzania is a promising country kwenye upande wa solar. Kwenye upande wa solar ambao Mheshimiwa Profesa Muhongo aliongea pia asubuhi kwa maana nchi nyingine ambazo ziko industrialized kama India na China wametumia hiki. Sasa Tanzania kijiografia kwa mwaka tuna uwezo wa kupata masaa 2,800 mpaka 3,500 ya miale ya jua. Sasa wakati tunajua mabadiliko ya tabianchi yanaweza yakakausha vyanzo za maji wakati huo huo kinyume chake ni kwamba kama kutakuwa na chochote kinachokausha vyanzo vya maji maana yake itakuwa ni upatikanaji wa jua la kutosha kwenye nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tusilie kwamba hapa Kanda ya Kati kuna ukame, tutumie ukame kutengeneza umeme wa jua kwa maana tuweke resources zetu kwa ajili ya ku-fund miradi ya umeme wa jua. Mheshimiwa Waziri wa Mipango yupo hapa na nafurahi sana kwa sababu yeye ndiye anayetupangia. Nilitamani sana kama mwanasiasa ambaye bado nina muda wa kufanya siasa kwenye nchi yangu, vijana washiriki katika mnyororo huu wa thamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunazungumza umeme wa jua na umeme wa upepo. Ili upate umeme wa jua na umeme wa upepo inabidi uwe na wind turbines (mitambo ya kutengeneza umeme wa upepo). Ili utengeneze umeme wa solar lazima uwe na solar panels. Kuna madini Tanzania yamegunduliwa ambayo yanaweza kutusadia kuweka viwanda. Kwa hiyo Waziri wa Mipango ni lazima awe anafikiri kwenye namna ya kushiriki kwenye mnyororo wa thamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani tuna-plan kuweka 100% nishati jadidifu kwenye nchi halafu tunategemea kuagiza mitambo, tunategemea kuagiza solar panels, tunategemea kuagiza wind turbines wakati kuna Wizara ya Mipango inaweza ikatusaidia tukatafuta resources tukajenga viwanda vya kutusaidia kuzalisha solar panels ili tukazalishe kwa sababu critical minerals zinazozalisha solar panels zipo nchini, tutazungumza kwenye madini. Kwa hiyo tusiwe tu tunagundua madini, tunasema tunahitaji 100% ya nishati, tunasema tunataka tupunguze kiwango cha joto duniani, tunataka tuhakikishe tunachimba madini yetu, tunanufaika, hivi vitu vyote ni interconnected. Natamani tuweke mipango kwa mtindo huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa kiasi hicho tutashiriki kwanza kuelekea 100% ya nishati. Pili, kuhakikisha vijana wanashiriki katika mnyororo wa thamani na Watanzania wanashiriki kwa sababu tutanufaika sisi ndani, vijana wetu wataajiriwa, vijana wetu watafanya biashara kwenye solar panels na wind turbines. Kwenye upande huo itoshe labda niseme kitu kimoja kwa sababu kwenye Kamati ukurasa wa 36, Kamati imezungumzia na Mheshimiwa Waziri pia kwenye Hotuba yake amezungumzia uwezo wa mitambo ya gridi ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nisome takwimu; uwezo wa mitambo katika gridi ya Taifa Februari, 2024 kuzalisha umeme wa maji, mitambo ina uwezo wa kuzalisha umeme wa maji megawatt 836.61, lakini tunazalisha megawatt 755.56, hiyo upande mmoja. Kwenye gesi asilia mitambo ina uwezo wa kuzalisha megawatts 1,198.82 lakini tunazalisha megawatts 935.11, umeme wa mafuta uwezo ni megawatts 83.92, lakini tunazalisha megawatts 65.75. Sasa tungamotaka kwenye megawatts 10.5 tunazalisha zero na Kamati imeeleza kwamba mitambo haina uwezo, kuna masuala ya miundombinu mibovu. Sasa vitu kama hivyo vinaturudisha nyuma, wakati tunahesabu kwamba eti umeme TANESCO wanatangaza umeme umezidi tumezima mitambo, tunaonekana kama jokers samahani na kwa due respect vitu vingine tuviache tu vinatudhalilisha hata wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tukijumlisha hizi megawatts zote full power ya TANESCO kwenye Gridi tutakuwa tuna umeme megawatts 4,000, tukijumlisha na Mwalimu Nyerere ikiwa full power zile 2,115 tutakuwa na umeme megawatt 4,241.85. Bado si kitu cha kujisifia, capacity yetu sisi ukiangalia estimated umeme ambao tunahitaji, tunahitaji by sasa hivi tu tuna megawatts 5,000 na ili tukijumlisha zote full power, kwa sababu nimewaambia hapa uwezo ni huu na tunazalisha pungufu kwa sababu mitambo mibovu. Sasa sifikirii kama ni busara kufikiri kwa kurudi nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilifikiri kuna haja ya kufanyia kazi hoja ya Kamati, kwamba sasa Serikali ikafanye marekebisho ya mitambo badala ya kutoka kwenye miji na kujisifia kwamba tumezima mitambo kwa sababu umeme umezidi. Nafikiri tunaonekana tunakwenda kwa kurudi nyuma. Kwa hiyo, hili nilitaka niliseme na nakubaliana na Kamati na kwa kweli Kamati wamefanya kazi kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa labda niende kwenye jimbo. Nashukuru sana kwa upande wa kwetu Singida, REA kwa Wilaya yangu ya Ikungi wamefanya vitu, niwapongeze sana. Kwenye Jimbo langu la Singida mashariki wame-connect vijiji vyote isipokuwa sehemu chache tu. Nimpongeze sana Meneja wetu wa REA pale, dada yetu anaitwa Leah, amefanya vizuri kwa sababu amefanyia kazi mambo ambayo tumemshauri na ame-connect vijiji vyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika REA III, Mzunguko wa Pili, vijiji 20 vimekuwa connected vyote upande wa Singida Mashariki. Niombe, bado hawaja-connect umeme katika Sekondari ya Ntuntu, Sekondari ya Lighwa pamoja na Kisima cha Maji cha Mungaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nyumba za ibada, Kanisa la KKKT Mbwanjiki, Kanisa la Pentecostal Mlumbi, Katoliki Dayosisi Singida Kinku, pia Kanisa la FPCT Mkunguakihendo. Hii yote ni mashariki, kwa kweli wanashukuru sana na wanaendelea pale kufanya shughuli zao na ni jambo kwa kweli ambalo ni zuri. Maeneo mengine ni Shule ya Msingi ya Kikio, Shule ya Msingi ya Nkundi, Shule ya Msingi Mnane, Lighwa, Ujaire, Sakaa, Taru, Ntuntu, Ntewa, kote wame-connect na ni jambo la kushukuru, ni vitu ambavyo kwa kweli tunaona ni going forward.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi na vitu vingine pia nitavipeleka kwa njia ya maandishi. (Makofi)