Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Anna Richard Lupembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara ya Nishati. Naomba nimshukuru Mungu ambaye ametupatia uzima na uhai, anaendelea kututetea katika majukumu tuliyopewa katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze sana Rais, kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya. Tumeona Bwawa la Mwalimu Nyerere sasa hivi limekamilika kwa asilimia kubwa sana na mategemeo sasa hivi nchi yetu umeme utatulia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Naibu Waziri Mkuu, Mheshimiwa Doto Biteko kwa kazi kubwa na kasi ambayo anaendelea kuifanya. Tumeona mabadiliko makubwa kwa muda mfupi. Tunaendelea kumwombea Mwenyezi Mungu aendelee kumpa hekima na kumsimamia katika majukumu aliyopewa ambayo ni mazito. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Naibu Waziri kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya. Kwa muda mfupi anafanya kazi kubwa na tunaiona jitihada yake. Tunaendelea kumwombea Mungu amsimamie katika haya majukumu aliyonayo. Naomba nimpongeze Katibu Mkuu pamoja na Naibu Katibu Mkuu kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kuifanya katika majukumu aliyopewa kwenye Wizara ya Nishati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wetu wa Katavi wananchi wana hamu sana na gridi ya Taifa. Naomba niipongeze sana Serikali, tayari tumeona Kituo cha Kupoozea Umeme pale Ipole kimekwisha, tumeona kipozeo cha umeme pale Inyonga tayari kimekamilika na vilevile tumeona kipoza umeme katika Mji wa Mpanda tayari kimekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona nguzo tayari zimewekwa, tukipita katika maeneo ya Barabara, lakini mpaka sasa hivi gridi ya Taifa ya Mkoa wa Katavi ina 56% tu mpaka muda huu ninapoongea hapa. Mwisho wa mkataba ambao na tulivyoahidiwa tutapata gridi ya Taifa, ni tarehe 30 mwezi Juni, 2024. Hapa naona takribani bado miezi miwili ili tuwashiwe gridi ya Taifa. Hata hivyo, kutokana na mazingira tunayoyaona si rahisi mwezi Juni kupata gridi ya Taifa kwa sababu nguzo zimewekwa tu. Naomba nipongeze wananchi wamelipwa fidia kote ambako nguzo zinapita. Tumeshawalipa fidia naomba nipongeze sana kwa hili, lakini tunaona kasi ya gridi ya Taifa kufika Mkoa wetu wa Katavi bado inasuasua sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipongeze kwa kasi ambayo tumeona, sasa hivi tumebadilisha kutoka kwenye nguzo za mbao tunakwenda kwenye nguzo za cement. Tumeona zipo katika maeneo yetu tukipita barabarani. Naomba sana kasi ya gridi ya Taifa Mkoa wa Katavi iongezeke, kwa sababu Mkoa wa Katavi ni mkoa wa kiuchumi, kuna viwanda, kuna mambo mengi na kuna wananchi wengi ambao wamekuja ili kuwekeza, lakini kutokana na kukosa gridi ya Taifa wameghairi na mpaka sasa hivi kuna miradi mingi na viwanda vingi vimesimama kutokana na kukosa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Mkoa wa Katavi umeme tunaotumia ni wa ma-generator. Sasa hivi yale ma-generator yamechoka. Umeme Mkoa wa Katavi haujatulia, unazima kila wakati, biashara za wananchi wa Mkoa wa Katavi sasa hivi zimesuasua sana, umeme ni uchumi. Sisi tuna viwanda; kutokana na ukulima tuliokuwa nao ndani ya Mkoa wetu wa Katavi wananchi wanalima mpunga na kuna viwanda vya kuchakata mpunga. Sasa hivi vinasuasua kutokana na umeme kutotulia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua 56% mpaka tuje kupata gridi ya Taifa siyo leo. Naomba basi tuongezewe hata ma-generator mawili, kwa sababu Mkoa wa Katavi kuna ma-generator matano tu. Tuongezewe ma-generator mawili ili kuongeza nguvu ili uchumi wa wananchi wa Katavi uweze kusonga mbele. Najua kuna mikakati na kwenye bajeti hii ametupangia bajeti kuhakikisha kwamba gridi ya Taifa inakamilika. Naomba sana, basi sisi Mkoa wa Katavi tunaomba Naibu Waziri Mkuu, mwaka huu tuweze kupata gridi ya Taifa ili na sisi umeme wetu uweze kutulia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu REA. Naomba nimshukuru Mkurugenzi Mkuu wa REA kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya. Ndani ya jimbo langu nina vijiji 54, vijiji 53 vyote vimepata umeme kasoro Kijiji kimoja cha Kanoge mpaka sasa hivi hakijapatiwa umeme wa REA. Katika ramani Kijiji chetu cha Kanoge kilirukwa. Naomba kijiji hiki kiweze kupata umeme, kimebaki kijiji hiki peke yake ambacho hakina umeme wa REA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunapeleka umeme katika vitongoji. Katika vijiji vyetu awamu ya kwanza na awamu ya pili tumeruka taasisi hususan shule za msingi, makanisa, hatujawafikishia umeme wa REA. Naomba kupitia hii awamu ya vitongoji, basi wapitishe umeme kwenye taasisi zetu, makanisa, shule za msingi, shule za sekondari ili watoto wetu waweze kusoma vizuri kwa sababu umeme ndiyo utawafanya waweze kusoma kila wakati, muda wote na vilevile kutumia computer. Sasa hivi Serikali imeelekeza kupeleka TEHAMA katika shule zetu; sasa, umeme haujawafikia. Naomba sana huu umeme unaoenda sasa hivi kwenye vitongoji vyetu, basi uende katika taasisi mbalimbali kama vile makanisa, misikiti, shule zetu za msingi na sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, safari hii sisi kama Wabunge kwanza tunaomba tushukuru, tumepewa majiko ya gesi, tumepeleka katika maeneo yetu ya vijiji ili kwenda kuhamasisha ili kuhakikisha sasa hivi wananchi wanatumia majiko ya gesi kwa ajili ya kuepukana na kukata miti hovyo na wasitumie mkaa kwa sababu ya uharibifu na hali ya dunia jinsi inavyokwenda. Sisi wenyewe tumeshajionea mafuriko. Tumeona athari kubwa katika nchi yetu imetokea. Hata hivyo, majiko ya gesi ni gharama sana. Naomba Serikali kupitia kampuni mbalimbali ambazo wanauza majiko ya gesi, washushe bei kidogo ili wananchi waweze kununua, kwa sababu kutokana na gharama kubwa wanashindwa kumudu. Wapunguze gharama ili waweze kutumia majiko ya gesi na tuweze kutunza mazingira yetu vizuri katika maeneo yetu ya vijiji pamoja na vitongoji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru na naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)