Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Zuberi Mohamedi Kuchauka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa nafasi. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa uhai na kuniwezesha kusimama jioni hii kwenye Bunge lako Tukufu na kutoa mchango wangu kwenye hotuba iliyopo mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama iliyo ada kwanza niwashukuru Naibu Waziri Mkuu, Naibu Waziri wa Nishati na watendaji wote wa Wizara hii ya Nishati kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa kuliangaza Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba yangu ya leo naomba niielekeze kwanza kwa upande wa REA, ama kwa hakika REA wanafanya vizuri. REA Liwale yenye vijiji 76 tumebakiza kijiji kimoja ili kifikiwe na umeme na vijiji vitatu nimeambiwa viko njiani bado vinasubiri ukaguzi, jambo hili ni la kusifiwa sana. Tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Liwale ni wilaya ambayo sisi hatuna mitaa, sisi tuna vijiji, Wilaya yetu ya Liwale Mjini ina kata tatu. Kata hizi ni Kata za Likongowele, Nangando na Liwale Mjini, hatuna mtaa. Sasa, shida iliyopo ni kwenye malipo ya umeme. Hawa watu ambao wako kwenye hizi kata za Liwale Mjini, wanatakiwa walipe shilingi 350,000 jambo ambalo si sawa kwa sababu wana sifa zote za kuwa vijijini. Iko Kata ya Liwale B; hii kata iko kilometa mbili kutoka Liwale Mjini, vijiji vyake vyote vinalipa shilingi 27,000, na kwenye Kata hizi tatu za Liwale Mjini, viko vijiji zaidi ya kilometa mbili kutoka Liwale Mjini lakini vinatakiwa vilipe shilingi 350,000, jambo hili haliwezi kuwa sawa. Kuna Vijiji vya Kuchocholokana, Nangando, Nganyaga, Naluleo, Kilipwike na Hulia, hivi vyote ni vijiji na vina sifa zote za vijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali wapelekewe umeme; hawa watu walipe shilingi 27,000 kwa sababu wana sifa zote za vijiji. Kama ni suala ya vipato, kukaribia mjini haina maana kwamba kipato chako ni cha juu. Wapo watu wanaishi vijijini, wana kipato kikubwa kuliko hata hawa ambao mnawaita wako mjini. Jambo hili naomba tulichukulie vizuri na tulielewe vizuri, naomba sana Mheshimiwa Waziri, hawa watu waendelee kulipa shilingi 27,000 ili waweze kufikiwa na umeme kama wanaopewa watu wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie suala la CSR; ninapozungumzia CSR nazungumzia CSR ya Bwawa la Mwalimu Nyerere. Mwaka jana wakati nachangia hapa nilitoa hoja ya kuiomba Serikali itambue kwamba Liwale ni miongoni mwa wilaya inayochangia ardhi kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere na leo nimekuja na takwimu sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bwawa la Mwalimu Nyerere lina square metre 1,194,400,000, contribution kwa kila wilaya, Kilombero wana square metre 552,280,155, Liwale wana square metre 341,406,683, Morogoro wana square metre 176,660,786, Rufiji wana square metre 99,925,691, Ulanga wana square metre 24,126,686, huo ndiyo mchango wa ardhi kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunakuja kwenye hiyo inayoitwa CSR, kwanza ninachofahamu, miradi yote inayotekelezwa na CSR kwa fedha za CSR huwa inakwenda sambamba na mradi husika, lakini leo Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere unakwenda kufika mwisho lakini hakuna mradi hata mmoja uliotekelezwa kwa fedha za CSR. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa zisizo rasmi; mgao wa CSR Bwawa la Mwalimu Nyerere haukufuata sheria. Hapa mimi nashindwa kuelewa, Serikali waje na majibu, hivi shida ni Sheria ya CSR au CSR haifahamiki au watu wanafanya makusudi kukiuka CSR? Kama unaweza ukapeleka Mradi wa CSR shilingi milioni 80 Kigoma ikajenga Chuo cha TEHAMA, ukapeleka Mradi wa CSR Dodoma shilingi milioni 40 ukajenga Chuo cha Tiba, shilingi milioni 40 mnataka kuipeleka Tanga ikajenge Chuo cha Tiba, ni sawa kwa jina kwamba huu mradi ni Mradi wa Kitaifa, nakubaliana na hilo, lakini iko miradi ya Kitaifa, kuna SGR ni Mradi wa Kitaifa, CSR yake itagawiwa kama ilivyogawiwa hizi? Kuna Bomba la Mafuta la Hoima, Chongoleani – Hoima Uganda, nalo CSR yake itagawiwa kama ilivyogawiwa hii? Kuna Mradi wa Daraja la Kigongo – Busisi nalo ni Mradi wa Kitaifa, CSR yake itafika lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, kuna Mgodi wa Mererani, kuna Mgodi wa Bulyanhulu, kuna Mgodi wa North Mara, CSR yake itaenea kama ambavyo wanafikiria hili? Kwa nini jambo likiwa ni...

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA:...habari za Kusini kunakuwa na songombingo songombingo? Naomba ...

MWENYEKITI: Mheshimiwa Zuberi Mohamedi Kuchauka kuna Taarifa. Taarifa tafadhali.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, niko hapa, niko hapa naitwa Mheshimiwa Tabasam.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Tabasamu, tafadhali karibu.

TAARIFA

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba nimemsikia mchangiaji anasema Miradi ya CSR namna inavyosambazwa pesa zake na akataja Daraja la Kigongo – Busisi. Sisi CSR ya Kigongo – Busisi hatujawahi kuiona. Ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Zuberi Mohamedi Kuchauka, Taarifa.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sifikirii kuipokea taarifa yake, ngoja niipokee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Waziri mwenye dhamana anahitimisha hotuba yake mwaka jana kuhusiana na CSR alisema hapa mbele kwamba, tunakwenda kujenga miradi ya Kitaifa lakini hata hivyo kwa ile sehemu ambayo imehusika moja kwa moja direct tuleteeni maandishi mahitaji yenu tuweze kutekeleza. Mimi ni miongoni mwa nilioongea na Mkurugenzi wangu tukaandika miradi tukapeleka, mpaka leo hatujui mwanzo wake ni nini wala inaishiaje. Jamani, watu wanasema ukitaka kula na kipofu usimshike mkono, kwa sababu wameamua kula na kipofu, basi angalau watudanganyedangaye. Hivi kweli mahali ambapo tunachangia zaidi ya mita 340 na pointi, tushindwe kupata hata zahanati?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Liwale tuna stendi yetu pale ya kisasa, tunavurugana huu mwaka wa 10 hatujaweza kuijenga. Tuna uwanja wetu wa mpira ambao umejengwa na halmashauri, tunategemea tungepata hapa angalau hata shilingi bilioni moja, hata shilingi bilioni mbili, shilingi bilioni tatu, wanakula na vipofu tunaona hili jambo wanalolifanya haliko sawasawa. Haiwezekani Liwale ambayo inachangia kilometa nyingi namna hiyo tukose hata shilingi bilioni tano, nini kinafanyika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninazo takwimu hapa zisizo rasmi; wanasema hawa wenzetu wa Morogoro wana shilingi bilioni 10, Pwani wana shilingi bilioni 10, yaani Pwani yenyewe wamesema wanaenda Kisaki na hawa ndugu zetu wa Pwani wanasema itapelekwa Mloka, sisi Liwale wanatuweka wapi au hatuhusiki? Hapa sioni nia njema, sioni nia njema ya Serikali kwenye mradi huu, kwenye CSR hii na ndiyo maana mpaka leo hakuna mradi uliotekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua unapokuwa na nia ambayo siyo njema hata Mwenyezi Mungu naye ana karama zake. Ndiyo maana unakuta huu mradi unayumba, mpaka leo hii hakuna hata mradi mmoja uliotekelezwa, lakini ni kwa sababu hawajanyooka, wangenyooka haya mambo yangeenda lakini kwa kuwa waliamua kuzungukazunguka, mara wapeleke Kigoma, mara wapeleke Tanga, mara wapeleke wapi, matokeo yake tumekwenda mahali tumekwama, hili jambo haliwezi kuwa sawa. Nawaomba sana, Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa, asiponieleza sababu ya kupeleka shilingi bilioni 80 Kigoma nitashika shilingi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Zuberi Mohamedi Kuchauka.