Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Issaay Zacharia Paulo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ya Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati. Kwanza nianze kwa kuungana na wenzangu wote kumshukuru sana Mwenyezi Mungu wa heri, aliyetujalia muda huu leo tukiwa tunajadili mustakabali wa Watanzania, kwa kweli tuna kila sababu ya kumshukuru kwa sababu ya rehema zake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua pia nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa inayofanyika nchini. Kwanza kwa jitihada kubwa, hizi juzi tumeona treni ya mwendokasi ikifanya majaribio. Wakati tukiwa mwanzo wa mwaka huu niliuliza swali hapa Bungeni kutaka ziara au huduma ya safari ya treni mwendokasi itaanza lini? Walisema kabla ya mwezi Juni na Serikali imetekeleza kwa wakati, katika majaribio yale Watanzania wamefurahia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kwa kazi kubwa ya kukamilika kwa Bwawa la Mwalimu Nyerere, kama mnavyojua, nchi yetu ilitoka kwenye mchakato mgumu wa kukatika kwa umeme na upungufu wa umeme nchini. Hii ni faraja kubwa kwa Watanzania na kwetu sote wawakilishi wa wananchi kwa hatua hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi nyingine ni kwako wewe Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Biteko na Naibu Waziri pia na watendaji wote wa Wizara. Kwa kweli tunakupongeza kwa kuteuliwa kwako kuwa Naibu Waziri Mkuu lakini pia Wizara hii muhimu sana. Umetusaidia sana kufanya kazi kubwa ulipokuwa Wizara ya Madini wakati ule na ikampendeza Rais akupeleke mahali hapo. Pia, kwa kazi kubwa inayofanywa na watendaji wote wa Wizara pamoja na Kamati yetu na taarifa yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mchango mdogo katika Hotuba ya Waziri pamoja na Taarifa ya Kamati, lakini kwa kuishauri Serikali. Kwanza natoa mchango huu kwa kuisemea kwamba, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, nadhani Watanzania wa sasa kwa sababu tayari bwawa limekamilika, kuna haja kubwa ya utakapokuja pale utoe kauli ya namna gani basi zile nyumba zote zilizo ndani ya mita 20 mpaka mita 30 katika Mradi ule wa REA, hazijapata kuunganishwa na mpango huu wa umeme wa REA, ziunganishwe zote nchini kwa sababu wananchi wanasubiri kwa hamu kubwa. Kama tunavyojua Mradi wa REA una miaka karibu 10 au na zaidi kutoka utekelezaji wake wa kusambaza umeme vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna majengo mengi sana yapo ndani ya mita 30, mita 20, pamoja na taasisi za Serikali zilizorukwa, lakini pia kwa sababu tayari bwawa limekamilika na uzalishaji wa umeme upo, ni imani yangu kwamba, hizi nyumba zitaunganishwa. Vilevile naamini hatutakuwa na zoezi la kupunguza maji kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere, lakini huduma iliyokusudiwa kwa Watanzania itapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza ujazilishi, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, kwa kweli hatuwezi kukamilisha zoezi hili. Kwa hiyo, pamoja na Wabunge wenzangu tunaomba sana, wale wananchi wote waliopo ndani ya hizo mita 30, mita 20, utafutwe mpango wa dharura wa kuhakikisha angalau wanaunganishiwa nishati hii. Wengine wamefanya wiring, wengine wanasubiri umeme na wanatarajia kwamba, watakapounganishiwa basi kwanza tutapata uzalishaji mkubwa wa umeme kutoka kwenye bwawa lililojengwa na pia tutajibu kiu na matarajio ya Watanzania ambao walikuwa wanasubiri umeme kwa hamu kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo naona ni muhimu sana kufanyike mpango wa mapitio. Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati sasa hivi tunapozungumza umeme kwenda kila kijiji ifikapo Juni 30, kuna maeneo kwa mfano Jimbo langu la Mbulu Mjini, nina vijiji kama 10, nguzo zimesimikwa ardhini zina karibu miezi nane, miezi sita na nyingine ni karibu mwaka, lakini hakuna umeme wala nyaya zilizounganishwa. Nguzo hizo zinaendelea kuoza ardhini, nadhani kuna haja kubwa ya kufanya tathmini ya namna ya kupeleka nguvu kubwa kwenye kuunganisha umeme kwenye maeneo yote nchini ili kuhakikisha kwamba, angalau maeneo yale ambayo wakandarasi wa kusimika nguzo wamewekwa basi waharakishe na fedha zitafutwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja kubwa hapa ni kwamba, angalau Serikali ijitahidi katika mwaka huu wa fedha tunaouanza itoe fedha zote ambazo tunaomba kwa ajili ya Wizara hii ili iweze kutekeleza mahitaji ya wananchi kupata nishati ya umeme. Kwa sababu, hatua hii ya ujazilishi tusipofanya jitihada tunakosa tija na manufaa ya ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere kwa sababu, kwa vyovyote vile umeme tutakaouzalisha ni mkubwa, lakini watumiaji watakuwa ni wachache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia, Serikali iangalie mpango huu wa kutoa kazi za kikandarasi kwa wenzetu hawa kupitia REA. Unakuta mkandarasi mkubwa anashika mikoa mitatu, anatafuta subcontractors wengine kwa hiyo, kunakuwa na mkanganyiko mkubwa, huyu analeta nguzo, unakuta hapa amesimika nguzo, mahali pengine hajapeleka waya, mahali pengine hata kuwasha umeme bado, waya zimeunganishwa. Kazi hii itakapokuwa inakwenda katika mazingira ya namna hii, wananchi wanasubiri umeme hawafikirii tatizo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yetu mengi katika majimbo tuliyotoka, hasa Jimbo la Mbulu Mjini, maeneo mengi ni sura ya vijiji. Mimi, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, japokuwa ameniahidi atafanya ziara mwezi Juni katika jimbo langu, lakini Jimbo la Mbulu Mjini tuna kata 10 ambazo zipo vijijini, maeneo yake ni ya vijijini, kata saba za mjini pia eneo la mji kwenye kata tatu tu ndiyo katikati ya mji. Kata nyingine ni za pembeni, ukienda Kata ya Silaloda kwa mfano ni kilometa kama nane, lakini huko ni vijiji hakuna hata nyumba za miji au nyumba zilizokusanyika mahali pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nguzo nyingi zinahitajika na usambazaji wa umeme unahitajika. Kwa hiyo, mpango huu kuunganisha wananchi wetu kwa shilingi 27,000 ukizungumza maeneo ya mji hayapo kwenye huu mpango, siyo sahihi, ukija pale utuambie. Kwa kweli, bado Serikali itazame jambo hili na kuyaweka maeneo haya katika mpango ule wa shilingi 27,000 ili umeme uweze kusambaa vizuri na kuweza kupata huduma iliyo bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye maeneo ya shule, kwenye makanisa, migodi, visima vya maji, vijiwe vya biashara pamoja na maeneo mengine yenye uzalishaji mkubwa tuna mahitaji makubwa ya umeme kwenye majimbo na hasa Mbulu Mjini. Kuna mgodi wa TAWA, ambao umeanza nadhani miaka 10, watu wanatumia majenereta, umeme haujafika. Tunaishukuru Serikali imepeleka nguzo, maeneo kama yale yakifanyiwa tathmini yanaweza kuleta tija katika uunganishaji wa umeme, lakini pia kwa mafanikio zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kukatika kwa umeme. Mkoa wa Manyara nadhani ni mkoa unaoongoza sana kukatika kwa umeme katika Taifa letu katika kipindi kilichopita. Kwa kweli, tunapata kadhia kubwa kwa wananchi, lakini janga lile lilikuwa kubwa. Hata hivyo, hata sasa bado kuna hali ya kukatika kwa umeme kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu. Nashauri, kama itawezekana tutafute mradi wa dharura wa miundombinu yote iliyochakaa nchi nzima kufanyiwa mapitio, ili walau tujue maeneo gani kwa mwaka huu yatafanyiwa ukarabati kuondoa tatizo hili la leo. Kunatokea tatizo la nguzo, kesho kunatokea tatizo la transformer, siku nyingine kunatokea tatizo la hitilafu kwenye njia ya umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote yanazalishwa kwa sababu, baadhi ya miundombinu yetu imechakaa na kwa kuwa, imechakaa kuna haja kubwa ya kufanya mapitio kinchi ili kuona tunazalishaje na kuondoa kadhia kubwa kwa wananchi wetu. Tunapata changamoto hiyo ya kukatika kwa umeme Mkoa wa Manyara, lakini pia tuna maeneo ya kijiografia ambayo ni ya vijiji, ambayo ni ya vitongoji. Kauli hii ya kusema umeme utawashwa Juni, 30 kwa kila kijiji, tunampenda sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, yeye ni mtendaji mzuri, je, inatekelezeka? Mbona hii inakuwa ni ajali kabisa ya kisiasa kwa wanasiasa kuanzia sisi Wabunge wote na hata Serikali kwa ujumla? Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, jambo hili litazamwe, Juni ni kesho kutwa, tumebakiza miezi miwili, katika vijiji vyangu 10 vya Mbulu Mjini kutawaka umeme? Japo tayari tumeweka nguzo zote katika kila kijiji, nyingine hazijasimikwa kama kule TAWA, nyingine zimesimikwa lakini hakuna waya na inawezekana hata wakandarasi wakatuangusha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, jambo hili linahitaji maandalizi, mapitio yakifanyika nchi nzima tunaweza kuwa na kauli ya pamoja ya kwenda kuwaambia wananchi ili waiamini Serikali yao, lakini pia wajue utaratibu wetu umekaaje. Hawa wakandarasi wababaishaji ni hatari sana, hapa kila Mbunge ukimuuliza hawezi kujua mpango ambao upo kwa jimbo lake kwa kipindi hiki cha mwezi wa Januari kwenda Aprili na Mei kwenda Juni, yaani mipango yao ni ya mfukoni, mipango yao ni ya kutembea nayo, mipango yao haiko wazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani ifike mahali kama ambavyo wanafanya baadhi ya Mawaziri...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa. Hitimisha tafadhali, ahsante.

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mengine nitaandika kwa maandishi, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)