Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tabora Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuchangia hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025. Naomba nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuipa Wizara hii fedha nyingi za miradi ambayo imeitekeleza. Nasema huyu ndiyo Rais mwenye upendo kwa Watanzania wote, mwenye utu na mlezi wa wananchi wake, tumpongeze sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa usimamizi wake mzuri wa Wizara hii mpaka imefanya mambo makubwa, miradi mikubwa imetekelezeka. Hii ni muhimu sana, hivyo kuleta mafanikio makubwa katika utendaji wa Wizara yote. Pia nawashukuru watendaji wengine akiwemo Naibu Waziri, mtani wangu Judith Kapinga na watumishi wote wa TANESCO na REA ambao katika Jimbo la Tabora Kaskazini wameweka alama kubwa ya umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwenye macho haambiwi tazama. Wizara hii imefanya kazi kubwa hasa katika kujenga miradi ya vyanzo vya umeme na usafirishaji wa umeme nchini kote, Miradi mikubwa kama wa Kinyerezi, Rusumo na ule baba lao wa Bwawa kubwa la Rufiji la Mwalimu Nyerere. Bwawa hili ndiyo mwarobaini wa upungufu wa umeme katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mradi wa REA; katika Jimbo langu la Tabora Kaskazini umeme umefika kila kijiji na natumia neno umefika, siyo kuna umeme vijijini, lakini nasema hongera sana katika vijiji vyangu vyote 82 vya Jimbo la Tabora Kaskazini umeme umefika na sasa tunaendelea na ujazilizi wa vitongoji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la mambo mtambuka kwa Wizara hii ya Nishati na hasa vijijini kwetu na hata mijini pia, kwa kutumia mkaa na kuni kama nishati ya kupikia au kupata joto majumbani. Hapa ndipo Wizara ya Nishati inachukua majukumu mtambuka, Wizara hii ina jukumu la kuzuia kuenea kwa jangwa nchini kwa kuzuia kukatwa miti kwa kusimamia upatikanaji wa nishati mbadala ya kupikia kwa bei nafuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jimboni kwetu tunalima tumbaku, zao hili ni la muhimu sana. Hivi sasa tumbaku ndiyo inaongoza kuleta hela za kigeni, kwa mwaka tumbaku inaleta dola milioni 400 sawa na shilingi trilioni 1.2, inafuatiwa na korosho ambayo inaleta dola milioni 200 na ushee. Kilimo hiki cha tumbaku kina matokeo hasi katika miti, tunakata miti mara mbili, wengine wote wanakata miti kwa mkaa na kuni za kupikia. Sisi pamoja na hilo la pili, tunakata miti kwa ajili ya kukaushia tumbaku, lakini hatuwezi kuacha kulima tumbaku, kwetu sisi Wanauyui, Tabora Kaskazini na Tabora yote kwa ujumla. Tumbaku ni muhimu sana kwa kutuingizia dola milioni 400 kwa mwaka ambapo 60% ya tumbaku yote inalimwa Tabora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ione umuhimu wa kufanya lolote kuzuia au kuleta afua za kuzuia madhara ya tabia ya nchi. Hivi karibuni wametupatia majiko ya gesi kupeleka kwa wakulima vijijini, nikajiongeza nikaongeza mengine 200 yakawa 500, impact au matokeo yake yamekuwa ni makubwa sana. Tunaomba Serikali kwenye mpango wake huu wa kusaidia majiko, maeneo yanayolimwa tumbaku yabaki na matumizi ya kuni kwa tumbaku tu, lakini ile ya kupikia Serikali iweke ruzuku kwenye majiko ili kupunguza kabisa matumizi ya kuni. Hili ni la muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la tumbaku hatuwezi kuliacha kwa sababu tunalihitaji sana kwa ajili ya kuleta uchumi wa hela za kigeni. Kwa kweli, Serikali itoe kipaumbele katika ugawaji wa nishati safi na kama ilivyo ni ajenda ya Mheshimiwa Rais kumtua mama kuni kichwani. Nashauri Serikali itakapoanza kutoa ruzuku ifikirie sana maeneo ambayo miti mingi inakatwa kwa sababu ya kupikia na kukaushia tumbaku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuacha kulima tumbaku, narudia mara kwa mara kwa sababu, inatuletea faida sana. Naitaka Serikali kupitia Wizara hii ya Nishati, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na ndugu yangu Naibu Waziri wa Nishati, mlisimamie hilo. Wajaribu ku-support tumbaku kwa njia nyingine ili kuokoa miti. Naomba maeneo yote yanayolima tumbaku, siyo Tabora tu, lakini maeneo mengine yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la kukatika umeme kila wakati katika Jimbo langu la Tabora Kaskazini. Wilaya ya Uyui iko mbali, njia ya kwenda Nzega, lakini umeme unaotoka Tabora kwenda Nzega mpaka Isikizya ndiyo huo unakuja mpaka Karangasi na Manyoni. Tatizo lolote likitokea huku Chaya tunapopishana na ndugu yangu Mheshimiwa Mbunge wa Chaya umeme unazimika mpaka Isikizya kule Uyui, kilometa 130 na hapo wanaanza kutembea na gari kwa saa kadhaa kutafuta fault iko wapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeambiwa nilipokuja kwenye maonesho pale kwamba, kumbe njia rahisi ni kujenga Kituo cha Kupoza Umeme pale Isikizya na wakati huu ambapo hawajajenga kituo ipo njia rahisi ya kuweka load circuit breakers njiani ili umeme ukikatika mahali fulani kule kwingine umeme uendelee kuwapo. Mazoezi yote mawili, moja ni la muda huu la kuweka circuit breakers, lakini la pili ni waweze kujenga Kituo kile pale cha Kupoza Umeme katika Makao Makuu ya Wilaya ya Uyui Iskizya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia kuipongeza sana Wizara hii inafanya kazi kubwa sana na tumeona matokeo yake kwa kumalizia Bwawa la Mwalimu Nyerere, mgao umepungua sana. Tuna imani kubwa, Mwezi Juni tuliwaomba Bunge wamalize mgao huu, Wizara hii itakuwa imefanya historia kubwa sana na Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu atakuwa ameandika ramani mpya ya matendo mema katika utendaji wake wa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniruhusu na naunga mkono hoja. (Makofi)