Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Deus Clement Sangu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia Wizara hii muhimu ya Nishati. Kama wenzangu waliotangulia, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayofanya hasa katika sekta hii muhimu ya Nishati ambayo hivi karibuni imekumbwa na misukosuko mingi, lakini Mheshimiwa Rais, amesimama imara kuinusuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, ambaye pia ni Waziri wa Nishati. Kwa kweli, kwa muda mfupi ambao ameingia katika Wizara hii tumeona mabadiliko makubwa na mimi binafsi, achilia mbali katika ziara za Kamati, nimeona miradi mingi mizuri na usimamizi wenye tija. Nampongeza pia, Naibu Waziri kijana kabisa, dada yangu Mheshimiwa Judith, kwa kazi kubwa anayoifanya, amewaheshimisha vijana kwa kazi yake nzuri. Aendelee kuchapa kazi, Mwenyezi Mungu atambariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitaongelea mambo mawili. Jambo la kwanza naanzia pale alipoishia Mheshimiwa Sylvia, hali ya utekelezaji wa Mradi wa REA, Mkoa wa Rukwa na la pili ni dhana ya local content katika Miradi ya Gesi na Mafuta.

Mwenyekiti, naanza moja kwa moja kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa jambo kubwa ambalo sasa wametufanyia Mkoa wa Rukwa. Mkandarasi ameanza kazi ya upelekaji wa gridi ya Taifa mwezi Novemba mwaka jana na tunaamini kwa kadri ya mkataba, tayari Mkoa wa Rukwa ifikapo mwakani Mwezi Oktoba tutakuwa tumeunganishwa na gridi ya Taifa. Naomba tu Wizara imsimamie mkandarasi huyu ili itakapofika Oktoba, 2025, mradi huu uwe umekamilika tuondoke kwenye kudoea umeme kutoka nchi jirani na sisi Mkoa wa Rukwa tutegemee umeme kutoka kwenye gridi ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema jambo hilo ambalo lina manufaa makubwa kwa mkoa wetu, nakuja kwenye suala alilosema Mheshimiwa Sylvia Sigula. Ni jambo ambalo linatukera sisi kama Mkoa wa Rukwa. Mkandarasi huyu alikabidhiwa kazi ya kupeleka umeme na alitakiwa kazi hii aikamilishe mwaka jana mwezi Oktoba, lakini cha ajabu akapewa extension tena ya miezi mitatu. Ilipofika Disemba tukategemea vijiji vyote kwenye ile kilometa moja, vijiji vyote vitawashwa, hakumaliza kazi hiyo akaongezewa tena mkataba wa miezi mitatu ili aweze kumalizia kazi iliyobaki kwa kilometa moja. Cha ajabu mwezi Machi umeisha ile kazi haijakamilika na bado nasikia amewaandikia tena REA waje huko tena wamwongezee miezi mingine, sijui mingapi mpaka kufika mwezi Juni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linatukwaza, kila Mwanarukwa linamkwaza. Jimbo la Kwela tu kuna vijiji 17 havijapata umeme hata ile kilometa moja ya kwanza hajaweza kukamilisha huo mradi. Nashangaa sana REA kwa nini walimwongezea kilometa mbili mkandarasi ambaye tunamlalamikia usiku na mchana, kila siku tunapiga kelele, lengo lilikuwa ni nini? Namwomba sana kwa heshima kubwa Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, jambo hili walichukulie kwa uzito mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Meneja wa TANESCO wa Mkoa, Ndugu yangu Engineer Ruhavi, Mameneja wangu wa Wilaya na watendaji wote wanahangaika usiku na mchana, lakini mkandarasi huyu anawasumbua. Juzi nilikuwa ziara Kata ya Mnokola, Kijiji cha Kisalala, Mnokola na Mititi, ameenda kushusha nyaya pale, baadaye baada ya wiki moja anaenda kubeba zile nyaya. Nauliza mkandarasi kwa nini unahamisha? Yeye alinidanganya kwamba, tumeibiwa; sasa nikauliza, mwanakijiji gani anaweza kwenda na crane akabeba zile nyaya? Mwanakijiji anapeleka wapi zile nyaya? Kwa matumizi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kumekuwa na ulaghai na nashangaa sana kama Menejimenti ya REA wamekaa naye huyu vikao vingi sana vya mashauriano, sasa kwa kazi hii ya umma yenye maslahi makubwa hivi, kwa nini tubembelezane? Kwa nini tusichukue hatua tumwondoe? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepata bahati ya kuzungukia miradi mingi kupitia Kamati ya Uwekezaji kwa mikoa mingi. Mikoa mingi niliyopita kama Mwenyekiti wa Kamati, nimekuta umeme 99%, mkandarasi amemaliza. Ukija kwangu ndio kwanza nusu ya vijiji tulivyotakiwa kumaliza mkandarasi hajakamilisha, Mkoa wa Rukwa vijijini 40. Leo hii ukifanya ziara Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu ukifika Rukwa ukigonga tu Ofisi ya CCM ya Mkoa, salamu ya kwanza ambayo itamkatisha tamaa ni jinsi ambavyo Mkoa wa Rukwa tumeumizwa na uzembe wa mkandarasi huyu kufikisha umeme. Sijui na sasa hivi anafanya kazi kwa mkataba gani na kwa jinsi wanavyofanya extension, extension zitakuwa zina muda mrefu kuzidi original contract. Maana yake wanampa tu, akija anawandikia wana-approve, akija anawandikia wana-approve. Sijajua ana specialty gani? Mkandarasi huyu mpaka tuanze kumu-entertain anatuumiza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Bodi ya REA imepita kwenye Kijiji cha Chombe na Kianda Igonda, kulitokea hitilafu hajakabidhi ule mradi lakini vijiji hivi vimewaka. Wiki tatu hawaja-resolve lile tatizo na Bodi ya REA imeenda kumwagiza bwana tarahe 19, ahakikishe amewasha umeme kwenye Kijiji cha Chombe na Kianda Igonda. Now, Bodi ya REA kabisa wanaomwajiri wamedharaulika, sasa atamsikiliza nani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu jambo hili ni jambo ambalo limetukwaza sana Rukwa, limetukwaza sana Jimbo la Kwela. Tunaomba kabisa afanye jambo la pekee kabisa, aunde timu ichunguze kuna shida gani kwa huyu Mkandarasi wa Mkoa wa Rukwa. Baada ya kusema hayo, nisiende sana huko nadhani ujumbe mmeupata vizuri jinsi tulivyokwazika na mkandarasi huyu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni suala la local content limeongelewa sana, mambo ya CSR na yameongolewa kwa namna mbalimbali humu ndani. Kuna jambo moja ambalo nataka niishauri Wizara hii ya Nishati, EWURA ndiyo tumewapa jukumu la kusimamia dhana yote ya local content kwenye Miradi yote ya Oil and Gas, lakini kuna hili suala linaloendelea la Bomba hili la Mafuta la kwenda Uganda (EACOP), kuna mambo ambayo tuliyaona yanasikitisha. Tumekuta kwanza, CSR zinatolewa lakini katika utoaji wenyewe wa CSR ni confidential. Unafika halmashauri wanaomba waambiwe contribution waliyopewa ni kiasi gani? Wale wanaowasaidia wanasema sisi policy zetu zinatukataza ku-disclose. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, interpretation yake ni nini? Unapewa msaada, yeye hatujui ataenda ku-declare vipi kwenye vitabu vyake? Kwa maana hiyo, inaweza ikatumia CSR kama sehemu kufanya tax evasion. Anafika pale ametoa madawati ya milioni tano, kwenye vitabu vyake ataandika bilioni tano. Kwa hiyo, tukawaambia haiwezekani CSR ikawa confidential na kuna CSR policy. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii mikataba ile ya ujenzi ule wa bomba inatakiwa baadhi ya kazi zifanywe na kampuni za wazawa kwa maana ya Kampuni za Kitanzania. Kampuni za Kigeni zinatufanyia ujanja wanapewa ile zabuni wakishapewa zile tender za sub-contract wanaleta kampuni za kwao kule za kigeni. Implication yake ni nini? Tufanye capital flight hela ilitakiwa kubaki kujenga uchumi wa nchi yetu inaenda kule kwao. Sasa sisi tumeingia ubia, kwa mfano EACOP na Uganda, pesa zetu tumeziingiza pale badala yake Uganda watanufaika. Sisi kwa sababu dhana ya local content hatuisimamii vizuri tutapigwa. Niombe na tuliwaambia watu wa EWURA wafanye investigation watuletee ripoti ili tuisaidie nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana. (Makofi)