Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ili niweze kusema mawili, matatu kwenye sekta hii muhimu sana ya nishati katika nchi yetu. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Wizara hii, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko kwa utendaji wake mzuri. Pia, niseme tu ukweli Mheshimiwa Dkt. Doto ni mchapa kazi, ni mtendaji na ni mtu ambaye ni msikivu kwa kusema kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku moja nilikuwa naongea naye akaniambia bwana hizi kazi wakati wowote (usiku wa manane) unasikia simu kuna jambo limetokea huko inabidi uachane na mambo yako yote ukaanze kushughulika na masuala ya dharura. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Doto tunakupongeza sana pamoja na timu yako yote akiwemo Mheshimiwa Naibu Waziri na Menejimenti yote kwa ujumla. Hata kule mkoani kwetu meneja wa mkoa yule anatupa ushirikiano wa pamoja na wilaya kwa ujumla, tunafanya nao kazi kwa kushirikiana. Kimsingi Wizara hii ipo karibu na wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, pamoja na Wizara kwa ujumla kwa kukamilisha kwa kiwango kikubwa sana Bwawa la Mwalimu Nyerere, ambalo tunasema ndiyo inaenda kuwa ndiyo tiba ya tatizo la umeme hapa nchini. Tulikuwa na janga kubwa la mgao wa umeme, sasa ule mgao tuseme ni kwamba umeondoka imebaki tu sababu za kiufundi. Kwa hiyo, hii inatupa matumaini makubwa sisi Wabunge ambao tupo moja kwa moja kwa wananchi kule. Likitokea tatizo anayepigiwa simu ni Mheshimiwa Mbunge bwana mbona mnakatakata umeme, lakini sasa hivi hilo tatizo halipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naweka connection moja kwa moja Bwawa hili la Mwalimu Nyerere na nataka niseme hapa kwamba, Bwawa la Mwalimu Nyerere ni neema kubwa sana kwa Watanzania, kwa sababu linaenda kutuhakikishia uhakika wa uzalishaji wa umeme. Kwa hivyo, hata tunaposema tunakwenda kwenye Tanzania ya Viwanda, hata wawekezaji sasa watakuwa na uhakika wanapoleta investment zao hapa. Wanakuwa na uhakika wa upatikanaji wa umeme. Kwa hiyo, niendelee kusema kabisa kwamba kusitokee watu wanabeza beza hili Bwawa, ooh mara sijui kulitokea nini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme hapa hapa niunganishe na kutoa pole kwa Watanzania waliopatwa na majanga mbalimbali ya maji kutokana na mvua kubwa ikiwemo kule Hanang na yale maporomoko yaliyotokea kule Mbeya kwa Mheshimiwa Spika. Hata nadhani leo tumepata taarifa kule Mikocheni Njia ya ITV pale, maji yamefunga barabara yaani yamefurika imekuwa kama kabwawa hivi. Sasa kule nako kuna bwawa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tufahamu kwamba hizi mvua zimekuwa excessive mwaka huu na ni masuala ya hali ya hewa. Kwa hiyo watu lazima waelewe, tusifike mahali tukaanza kubeza juhudi zinazofanywa na Serikali kwa ku-connect na mvua, mvua haiwezi kuzuilika. Hii mvua ni ya Mungu, hatuwezi ku-connect utendaji wa Serikali na mvua. Nitumie nafasi hii kuwashauri Watanzania wenzagu, pale tunapoona jambo zuri linafanyika tuliunge mkono na tulipongeze. Kama tunaona jambo halipo sawasawa tushauri kwa busara na kwa utulivu. Tusiwe tunaongeaongea vitu vingine ambavyo havina tija. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu hapa kazi kubwa ambayo Mheshimiwa Waziri anapaswa kujielekeza sasa hivi kwenye sekta hii ya umeme ni kuhakikisha tunajikita ama tunajielekeza kwenye miundombinu ya umeme. Haiwezekani ikafika mahali sijui kuna transformer imesababisha umeme umekatika mahali ikawa ni kelele nchi nzima, hapana. Hivi ni vitu vya kawaida ambavyo ni vya kitaalamu (technical) ambavyo inapaswa Wizara wawe navyo karibu. Nguzo imedondoka mahali au imekatika inaleta kelele ambazo hazina tija. Kwa hiyo, lazima tujikite kwenye vitu hivi vya kitaalamu (technical) ili kuhakikisha tunaondoa malalamiko yasiyokuwa na tija ambayo kuna watu wanaingia humo humo wanaanza kupandikiza chuki ambazo wala hazina msingi wowote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa kwenye kuzungumzia mambo mahususi kwenye jimbo, ambayo hata wenzagu wamezungumzia kwenye maeneo yao. Kwanza, ni umeme kwenye taasisi za umma, umeme unafika mahali lakini unakuta taasisi fulani imeachwa jirani pale, shule, zahanati, msikiti ama kanisa. Ni vyema na niombe sana Wizara wajikite kuangalia haya maeneo, ni muhimu sana wapatiwe umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kule kwenye jimbo langu kuna Shule ya Msingi Nkwae, Idang’adu, kuna Hospitali pale Misinko, kuna Ughandi kwenyewe, kuna Mfumbu, Mjura, Ikumese, Mpambaa, Shule ya Msingi Kafanabo, Chifu Gwao Shule Shikizi, Shule ya Sekondari Mikiwu na Zahanati ya Malolo. Haya maeneo yapatiwe umeme kwa sababu hayapo mbali, umeme haupo mbali, lakini unakuta ni nguzo moja wanaambiwa hamna. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni vizuri TANESCO wanapoona REA wameishia mahali wao wafike. Wasiwaache REA pekee yao wawaunge mkono kwa nguzo moja ama ikiwezekana kuwe na programu mahususi ya kuhakikisha maeneo yale ambayo REA wameishia na TANESCO nao wasaidie. Hii inaleta malalamiko wakati mwingine hata wananchi tu wa kawaida, umeme upo pale nguzo moja inakuwa ni shida, umeme hamna. Wanaambiwa bwana hapa sisi tumeishia hapa, sasa hii inaleta shida na wananchi wetu hawamjui REA, hawajui nani, wao wanajua ni Serikali. Kwa hiyo, ni vyema kukawa na coordination ya kutosha ili kusiwe na malalamiko yasiyokuwa na msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye ule umeme wa kwenye vitongoji, tulikuwa tumeahidiwa kupata vile vitongoji 15, huu Mradi bado haujatekelezwa. Kwa hiyo, niishauri sasa Serikali watuletee huu mradi lakini pia kwa sasa tusiishie kwenye hivyo vitongoji 15, wa-extend waongeze huo wigo ili wananchi wengi wapate umeme. Kule kwangu kuna vitongoji ambavyo vina size ya vijiji, ni vikubwa kama vijiji. Naomba sana, kitongoji kile, tunaita Kijiji kivuli cha Mukulu wapatiwe umeme. Pale Nkwae Kijiji cha Ikiwu wapatiwe umeme, Mlimani nao wapatiwe umeme, Mburi, Ng’ongoamwandu nao wapatiwe umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kumalizia, naona umewasha mic, kwenye suala la gharama, wale wananchi wetu ambao wapo tunasema peri urban, vijiji lakini ni kama aina fulani ya kamji. Sasa hivi wanaambiwa walipe shilingi 320,000…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa, hitimisha tafadhali.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi. Niombe ile shilingi 320,000 ifanyiwe re-thinking hata kama haitakuwa shilingi 27,000 basi ishuke itoke huko ije hata kwenye shilingi 50,000…
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. ABEID R. IGHONDO: … ili iwe affordable kwa wananchi wetu. Baada ya kusema haya, naomba kuwasilisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)