Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kondoa Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
3
Ministries
nil
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu sana ya Nishati. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema mbalimbali. Nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuwapa afya njema viongozi wetu wakiongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waheshimiwa Mawaziri wote ambao wanamsaidia Mheshimiwa Rais na Watendaji wa Serikali wote ambao wapo kwa ajili ya kuhudumia wananchi hawa wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Nimesimama kuchangia nikiri kwamba, mambo mengi tayari tuliyazungumza na Wizara nikimshirikisha mwenyewe Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu ambaye ndiye Waziri wa Nishati na kwa kweli namshukuru sana aliweza kunipa ushirikiano mkubwa. Nikiri Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, kwamba, watu wake wamenihudumia vizuri sana na imekuwa ni kawaida, watu wake ni wakarimu sana. Kwa kweli tumefika tumezungumza nao na wamenipokea vizuri na nikiri wamekubalina na yale ambayo tuliyaomba kwa ajili ya manufaa Wanakondoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Naibu Waziri, dada yetu Mheshimiwa Judith amekuwa amei-own sana Wizara hii kana kwamba amekuwa hapo kwa muda mrefu. Naamini anamsaidia Waziri vizuri na anamsaidia Mheshimiwa Rais, vizuri. Aendelee kuchapa kazi kama icon ya vijana wa Tanzania hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa shukurani kwa Wizara kwa niaba ya Wanakondoa kwa sababu ni mji ambao uliachwa nyuma sana. Ni mji wenye mitaa michache sana (36), lakini ni mji ambao una mitaa mingi ambayo haijafikiwa na umeme na pia ni mji lakini hauna umeme. Tumefanya mazungumzo ya muda mrefu sana na Wizara ya Nishati na ni watu wakarimu wamenielewa. Tumepewa hiyo mitaa 15, REA wameichukua. Namshukuru sana Mhandisi Hassan Said amekuwa mkarimu sana na alitupokea tukiwa na viongozi wangu na tukawa tumei-mention mitaa ile 15 na maeneo ambayo yanatakiwa yapewe umeme na REA na yamechukuliwa. Nashukuru sana hilo na nawashukuru kwa niaba ya Wanakondoa na naamini sasa Wanakondoa watapata na wenyewe huduma ya umeme kwa gharama ile ile ambayo wangepata Watanzania wengine kutokana na hali ngumu za wananchi wetu, tunafahamu ni mitaa lakini ni vijiji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ambayo yamebaki tumezungumza na Menejimenti ya REA, wameyachukua na wameyaweka kwenye Mpango wa Bajeti hii ambayo tunaijadili. Kwa maana hiyo, sasa naunga mkono hoja ya Wizara hii. Naunga mkono sana Hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwa sababu mambo mazuri yanakuja kwa ajili ya wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo nina mambo machache sana. Namshukuru pia Katibu Mkuu wa Wizara maana ni mtu makini sana na ana vijana wake makini sana. Engineer Bakar Kalulu huyu ni Meneja wa TANESCO Kondoa, ni mchapakazi sana. Pia, namshukuru hata Meneja wetu wa Mkoa wa Dodoma ni mtu mahiri, ni mtu msikivu na kwenye maeneo mengi ametusaidia sana katika kutatua changamoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukianza kata moja, kata ya kwanza, naweza nikaizungumzia Kata ya Kingale, kuna Mitaa Tampori, kuna Mtaa wa Kwamtwara na Mtaa wa Chemchem, mitaa hii ni mikubwa, lakini haijawahi kufikiwa na umeme. Hata hivyo, Wizara imekwishaichukua na watu wa REA wameichukua hii na wataiingiza katika mpango. Kwa hiyo, kwa niaba ya wakazi wa mitaa hii mitatu, nawashukuru sana na naomba wachukulie hiyo serious ili watu hawa pia waweze kupata umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata hiyo hiyo ya Kingale kuna maeneo ambayo hayakufikiwa na umeme kwenye vitongoji, pia, vimechukuliwa vimewekwa katika mpango. Kwa hiyo, Wanakondoa wasubirie kwamba, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inawapelekea umeme na watapata huduma. Kata ya Suruke tunashukuru tulikwenda tukazungumza na Menejimenti ya REA wakatupatia mitaa ile mitatu ya kata, kata ilikuwa haina umeme, lakini wakawa wametupelekea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe taarifa Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu kwamba wamewasha umeme kwenye mitaa na kwa mara ya kwanza kwenye kata hiyo wamewasha umeme na umebaki Mtaa mmoja wa Tungufu ambao kidogo kuna changamoto ambazo zipo ndani ya uwezo wa Menejimenti ya Wilaya. Wakifanyia kazi najua Tungufu pia watapata umeme. Kwenye kata hii ndipo kwenye ile changamoto sasa ya maeneo ya Guluma ambayo hayakufikiwa na umeme. Mradi umepita ukaruka haya maeneo, ni wakazi wengi wanafika 2,000, lakini mradi huu uliwaruka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndipo nilipokwenda kwa Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nishati na pia nilifika kwa Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, lakini vilevile tumezungumza na Menejimenti ya REA kuona ni namna gani wanaweza kumalizia ile mitaa, wananchi wanalalamika sana. Kwa maana hiyo, kwenye Kata hii ya Suruke kuna mambo mawili, naomba wanisaidie kwa uharaka wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, ni hilo la kuhakikisha ule Mtaa wa Guluma Churumai ambao umebaki umaliziwe kwa mkandarasi Huyu huyu kabla hajakabidhi mradi, kwa sababu ni kitendo cha kumwongezea tu scope ili aweze kumaliza ile Mitaa ya Churumai na Guluma iweze kupata umeme. Uzuri nguzo zipo, bado zimejaa tele katika mtaa huo huo na ndipo nilipomwambia Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu kwamba kulikuwa na wazo la kutoa zile nguzo na kuzihamisha jimboni. Ni jambo ambalo lingetufedhehesha sana hasa mimi Mheshimiwa Mbunge, Diwani na Wenyeviti, lakini pia tusingemsaidia Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu ana njaa hapo unanyanyua chakula unapeleka sehemu nyingine kabla hujakamilisha. Sasa nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kuzuia jambo hilo na naomba sasa mkandarasi huyu huyu kwa sababu bado yupo site, amalizie zile kaya ambazo zimebaki. Kata ya Serya, Mongoroma, Chandimo, Dumi na Hurumbi, pia ni maeneo ambayo hayana kabisa umeme. Basi naomba wakandarasi hawa wapatikane mapema ili wapeleke umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo mengi katika mitaa yangu ambayo hayana umeme, Kata ya Kilimani, kuna maeneo ya Damai. Jambo kubwa ambalo naomba Damai, Chavai na Kirere nilichokuwa naomba Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, yapo maeneo TANESCO wameyahudumia. Wamepeleka miundombinu ya umeme lakini wamepeleka kwa bei ya shilingi 320,000 mpaka 600,000 na 900,000, wananchi wa mitaa ile hawana uwezo wa kuingiza umeme kwa gharama hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeomba kwamba TANESCO waweze kuona, Katibu Mkuu asaidie hapa aweze kuona, kwa sababu kuna mahali jirani walifungiwa kwa shilingi 25,000. Wao wanapelekewa kwa shilingi 320,000 jambo ambalo linawafanya wananchi wengine wanakuwa wanyonge wakati Serikali yetu ni hii na uwezo wao ni mdogo kama wale waliofungiwa kwa shilingi 27,000. Kwa hiyo yale maeneo yote ambayo TANESCO wamepeleka umeme, nguzo zimesimama, nyaya zipo tayari wamefunga transformer, lakini hakuna mtu hata mmoja aliyeunganishiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upo Mtaa mmoja wa Damai wameunganisha wafanyabiashara wawili tu wa mashine za kusaga, wananchi wengine wote wanasubiria ile fair ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kufunga umeme kwa gharama ile ya Watanzania maskini wengine. Kwa maana hiyo tunaomba yale maeneo yote yaliyofikiwa na umeme wa TANESCO hebu walione hilo. Kwa upande wa Kata hii ya Suruke tumekwishaandika barua tumeipeleka kwa Meneja wa Mkoa ili kuomba TANESCO waone hali duni ya Watanzania ambao wanaishi kwenye mitaa ambayo inafanana na vijiji, waweze kuwekewa umeme kwa gharama ya shilingi 27,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yote kwa yote naunga mkono hoja na naishukuru sana Wizara kwa kukubali mitaa yangu ile kuchukuliwa na REA na kukubali mitaa iliyobaki tuiingize kwenye mpango huu. Nawatakia kila la heri Mungu awabariki sana, wachape kazi kwa ajili ya Watanzania. Ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)