Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili niwe mchangiaji wa mwisho katika siku hii ya leo. Jambo la kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa ambayo ameifanya katika kutekeleza miradi mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ambayo ameifanya katika kuisimamia Wizara hii ya Nishati, nawapongeza viongozi wa taasisi zote na mashirika yote yaliyopo chini ya Wizara hii, kwa kweli kwa pamoja wanafanya kazi nzuri sana, hongereni sana. Nawapongeza pia kwa kuja na bajeti nzuri, bajeti ambayo inatupa mwelekeo mzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa umeme kwenye maendeleo ya nchi yoyote unajulikana na unaeleweka vizuri, nchi yoyote inapotaka kujinasua katika ujenzi wa viwanda inahitaji umeme wa uhakika. Tunahitaji umeme kwa ajili ya kujenga viwanda mama, viwanda vidogo vidogo, viwanda vya kuongeza thamani ya mazao, tunahitaji umeme kwa ajili ya kuweka maisha yetu yawe mazuri ili wananchi waweze kula maisha safi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hiyo tu, tunahitaji nishati nzuri kwa ajili ya kupikia. Tunahitaji umeme ili wananchi waweze kupikia pia tunahitaji gesi kwa ajili ya kupikia na tunahitaji kwa ajili ya kusafirishia mazao na kufanya kazi nyingine mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hizi za umeme, kazi za nishati zikifanyika vizuri tutapunguza umaskini wa nchi yetu, tutapunguza tatizo la ajira kwa wananchi wetu kwa sababu wananchi walio wengi kule vijijini umeme ukifika wanaanzisha viwanda vidogo vidogo mwingine anakuwa na friji anaanza kutengeneza ice cream, mwingine anaanza kufanya kitu kingine chochote, mwingine anakuwa na soda na kadhalika, hii inachangia kutoa ajira na kupunguza tatizo la ajira lakini pia inachangia kupunguza umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wetu wa Songwe pamoja na kazi nzuri ambayo inafanywa na Wizara hii lakini kumekuwa na shida kubwa sana ya kukatika umeme katika Mkoa wa Songwe. Umekuwa unakatika mara nyingi sana, hii inatokana na miundombinu ya umeme kuwa midogo na bado haijakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa tunasubiri sana ule mradi wa backbone wa grid kubwa ambao walisema kwamba itatoka Iringa, itakuja Mbeya, itakuja Vwawa, itakwenda Tunduma itaenda mpaka Rukwa ili kusudi umeme sasa uweze kusambaa na uweze kupatikana. Sasa hivi umeme unaopatikana kule ni mdogo pamoja na kwamba sasa hivi uzalishaji umeweza kunasua, Bwawa kubwa lile wameweza kuzalisha umeme wa kutosha na ziada, lakini miundombinu ya kusafirisha ule umeme kutufikia bado ni hafifu na hivyo kusababisha ukatikaji mkubwa sana wa umeme katika eneo lile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kwetu tulikuwa tuna-experience karibu ukatikaji wa umeme mara 15, mara ngapi kwa siku, sasa hivi waliposema umeme umekuwa mwingi nikategemea sasa kukatika kutakuwa kumekwisha, lakini mara utasikia kuwa nguzo imedondoka, mara sehemu fulani kumetokea hii, bado tatizo lipo! Kwa hiyo tunaomba ule mradi backbone kwa kweli wauharakishe, ambao utaenda kuunga na switch ile ya kwenda Zambia ambapo sasa kama kuna tatizo la upungufu wa umeme hapa nchini tunaweza kutumia umeme wa Zambia, tunaweza tukatumia umeme wa Kenya, tunaweza tukatumia umeme wa Ethiopia na maeneo mengine. Kwa hiyo, katika utaratibu huu kwa kweli ni vizuri sana wakahakikisha kwamba ule mradi unakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuchangia ni kuhusu vijiji. Kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Waziri na nawashukuru sana REA pamoja na TANESCO, wamefanya kazi nzuri. Vijiji vyangu vyote ambavyo vilikuwa havina umeme sasa hivi umeme umefika, lakini haujawashwa kwa wananchi, umewashwa kwenye transfoma. Sasa wananchi siyo kwamba wanataka wauone kwenye transfoma, wanataka wauone ule umeme wanautumia kule majumbani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu karibu zaidi ya miezi mitatu sasa hivi hawajasambaziwa na tatizo limekuwa kwamba kuna upungufu wa mita. Sasa tunaomba Mheshimiwa Waziri kwa sababu umeme umeshafika, tunaomba walishughulikie haraka suala la mita ili vile vijiji vyangu karibu 15 ambavyo umeme umefika, umewaka kwenye transfoma uweze kuwaka katika maeneo yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina uhakika kwa sababu wananchi kama wale wa Kijiji cha Ilomba, Idunda, Ipyana, Nyimbili, Hantesya na maeneo mengine wamekuwa wakilalamika sana wanahitaji umeme, kule Namwangwa wanahitaji umeme kwa kweli, kwa hiyo naomba waharakishe suala la kupeleka hizo mita ili wananchi waweze kufungiwa na waweze kupata umeme na waanze sasa kula maisha vizuri. Tunamshukuru sana kwa upande wa vitongoji, kuna vitongoji ambavyo bado havina umeme. Mradi umekuja na vitongoji vichache lakini vipo vitongoji vingi ambavyo bado havina umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Wilaya yetu ya Mbozi nina vitongoji karibu 600 na zaidi, vitongoji 300 vina umeme, nusu bado havina umeme. Sasa tunaomba mkakati uongezeke ili kuhakikisha vitongoji vile ambavyo havina umeme vinakuwa na umeme. Maeneo kama Izyika kule, maeneo ya Hasanga, maeneo ya Josho kule bado vile vitongoji hawana umeme na umeme unahitajika sana. Maeneo kama ya Nsenya, Msia Kati, Igunda na maeneo mengine yote yanahitaji umeme. Tunaomba kweli huu mradi wa vitongoji kwa kweli waongeze kasi ili kusudi wananchi waweze kunufaika na suala hilo la umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Waziri ningependa kushauri mambo mawili. Jambo la kwanza, sasa hivi tatizo la climate change, tatizo la mabadiliko haya ya tabianchi yataendelea kutusumbua na yanatuathiri sana. Tunahitaji kuwa na mkakati wa kutosha kuhakikisha kuwa tunakabiliana nayo. Angalia kuna wakati unakuta kwamba kuna upungufu wa maji umeme utapungua, sasa maji yamezidi umeme utapungua. Kwa hiyo tatizo linakuwa bado ni kubwa. Mafuriko yakitokea tuna tatizo, tukiwa na ukame tuna tatizo. Kwa hiyo, tunahitaji mkakati madhubuti wa kuhakikisha kwamba kwa kweli tunakabiliana na hili suala vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, sasa hivi ukataji wa miti, watu wanakata miti sana. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri wametupa majiko ya gesi machache kwa ajili ya kuwapa wananchi ili waweze kutumia majiko ya gesi, lakini bado safari ni ndefu, kwa sababu wananchi walio wengi wa Tanzania kwa zaidi ya 98% wanatumia kuni na bado tunaendelea kukata miti na wanakata ovyo ovyo. Matatizo yote haya kama hatutakuwa na program ya kuhakikisha kwamba tunarudishia au tunapanda mti, bado tatizo la tabianchi litaendelea kutuathiri sana. Kwa sababu ukame unaweza ukatukuta, miti itaendelea kukatwa na tutakuwa na upungufu wa maji na hivyo kusababisha kusiwe na umeme wa kutosha. Naomba Mheshimiwa Waziri aweze kulishughulikia suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba dakika moja kama unaweza kuniruhusu, kwa sababu ya muda niombe tu, kuwapongeza sana kwa kazi nzuri waliyoifanya, lakini wachukue hatua katika kukabiliana na haya masuala, zaidi ya hapo naomba niseme kwamba tunahitaji umeme na tunayo imani kazi wanayoifanya ni nzuri, nawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na nawatakia kila la kheri, ahsante sana. (Makofi)