Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.

Hon Ally Juma Makoa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kondoa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.

MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Naibu Spika, nipo. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu na nishukuru kwa Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kutekeleza miradi katika nchi hii. Ninaanza na kuunga mkono hoja iliyopo mezani, nina michango michache sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Serikali imefanya mambo makubwa katika bajeti hii ambayo tunaendelea nayo na mwaka wake unaisha wiki moja ijayo, kwa maana hiyo tunaimani kubwa sana na bajeti hii ambayo tunakwenda kuipitisha na kutokana na hilo sasa ndiyo maana nikaunga hoja, nikaunga mkono hoja mapema kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepeleka fedha nyingi sana kwenye Majimbo yetu katika kutekeleza miradi na hivyo tunayo imani kubwa hata mwaka ujao wa fedha kasi na mwendo utakuwa ni huo huo na hivyo kuendelea tu kuisisitiza Serikali kuhakikisha fedha ambazo tunazipitisha kwenye Bunge hili ziwafikie wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona juhudi za Serikali hata katika bajeti hii kwa mfano, tulipangiwa visima vitano katika kila Jimbo na tumeona Wizara imeshapeleka wataalamu na tayari maandalizi ya kuanza kutekeleza miradi hii yameanza. Kwa hiyo, naipongeza sana Serikali lakini pia hata katika shule ambazo tumepangiwa na Serikali katika bajeti hii ambayo tunakwenda kuipitisha nimeona maandalizi kwamba wameshaanza kwenda kuangalia maeneo na kujiridhisha ili waweze bajeti ikipita hii waweze kupeleka fedha haraka na kwenda kutekeleza miradi, hiyo napongeza sana Serikali na nina imani kubwa na Serikali yangu iliyo chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba katika kipindi hiki cha mwaka tumefanya miradi mingi na miradi mingi bado haijakamilika. Kwa mfano, miradi ya maji, sehemu kubwa ya miradi ya maji bado ipo kwenye utekelezaji na mwaka wa bajeti ndiyo huu unakwisha, ninaiomba Serikali kuhakikisha ile miradi yote tuliyoanza nayo yenye miaka mitatu, miaka miwili ama mwaka basi katika kipindi hiki tunachoelekea bajeti inayofuata basi miradi ile iende ikakamilishwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukimalilisha ile miradi ndipo tutakapoanza na miradi mingine. Kikubwa ninachosisitiza hapa ni kwamba matokeo ya fedha ya Serikali yatakamilika tu pale ambapo wananchi wataanza kupata huduma kupitia ile miradi. Kwa maana hiyo nina imani na ninaamini kwamba kwa sababu imekuwa ni kilio cha Waheshimiwa Wabunge juu ya miradi yetu hii ambayo imekamilika, basi Serikali itaweka mkazo kulipa madeni ya wakandarasi pamoja na kumalizia viporo vilivyobaki nyuma kabla hatujaanzisha miradi mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nazishauri Wizara zote kwa ujumla zishirikishe Wabunge ili pasiwe na changamoto katika kutekeleza miradi hiyo. Nimeona mfano hapa wa haya maeneo ya sekondari; wataalamu walipokwenda kwenye jimbo langu kuyaangalia wakakutana na changamoto. Wamekwenda bila kutoa taarifa kwa mwenye jimbo, lazima utapata changamoto. Wamekwenda kuoneshwa maeneo wakayakataa maeneo, maeneo ambayo unakuta ni maeneo ya milima; na kweli ukiweka fedha ya Serikali kujenga shule maana yake shule haitakamilika, bajeti ndiyo hiyo ilipangwa, tutaanza kuisumbua tena Serikali kwenda kutafuta fedha ambazo hazikuwepo kwenye mpango ili kukamilisha zile sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo nimeona barua za kuyakataa yale maeneo, lakini nilipigiwa simu na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Elimu, nikamwambia Jimbo la Kondoa Mjini wazee wanamwamini sana kijana wao. Kama tatizo ni eneo katika sekondari zote tulizozijenga wazee walinikabidhi mimi maeneo, kwa sababu wana imani. Hata walipokwenda wakakwama maana yake ni kwamba, wamekwama kwa sababu hawakumshirikisha mwenye jimbo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimtoe hofu Mheshimiwa Waziri, tayari wazee wamenipigia simu kwenda kunionesha maeneo mazuri kwa ajili ya ujenzi wa miradi hiyo ya sekondari mbili; Sekondari ya Kingale na hiyo tunayokwenda kuijenga kule Suruke. Kwa maana hiyo mpango huo wa fedha wasije wakakwama kupeleka kwa sababu ya kuwa na mashaka na maeneo. Ninawatoa mashaka, mpango uendelee vizuri, nina hakika ndani ya wiki hii nitakamilisha utaratibu mzima wa hayo maeneo na nitailetea Serikali ili iweze kutekeleza miradi kwa ajili ya wananchi wa Kondoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ninalolisisitiza ni kwamba, tuna jambo kubwa sana la ujenzi wa lile Daraja la Mto Bubu, kila siku tunaliongelea jambo hili. Lile daraja likijengwa litakuwa ndio uchumi wa watu wa Kondoa. Kwa hiyo, kwa sababu tayari taratibu za awali zimekamilika ninaiomba Serikali ianze kuona namna ya kupeleka fedha kwa ajili ya kuanza kujenga Daraja lile la Munguri B; tumezoea kwa kusema ni Daraja la Munguri. Baada ya kuyasema hayo ninaunga mkono hoja. Ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)