Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KILUMBE S. NG'ENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi hii. Naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya na uzima. Nitumie nafasi hii vilevile kuendelea kuipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa kipenzi chetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ya maendeleo inayoendelea kufanyika kwenye majimbo yetu kote nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mchango wangu leo nataka nijielekeze kwanza kabisa katika ugawaji wa fedha kwenye miradi ya maendeleo. Moja ya tatizo ambalo tunakutana nalo sisi kama Waheshimiwa Wabunge ni suala zima la usawa na haki katika ugawaji wa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kwamba siku zote bajeti haitoshi, tuna mahitaji makubwa lakini kipato chetu ni kidogo; lakini tunataka hicho kidogo kigawanywe kwa usawa. Leo hii ni miaka mitatu sasa Serikali inatenga bajeti ya kukarabati Meli ya Liemba na Mwongozo bila kupeleka fedha na bila mradi kutekelezwa; sasa hii haiwezi kuwa sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo maeneo ipo miradi ya mabilioni kwa mabilioni inafanyika, lakini hii miradi midogo tu kwa ajili ya maendeleo ya wananchi kwenye maeneo hayo haifanyiki. Kwa hiyo, nitapenda Waziri wa Fedha atakapopata nafasi atueleze Wizara yake inaweka priority gani katika ugawaji wa fedha na kusahau kabisa mambo ya msingi kama haya kwenye baadhi ya maeneo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ninalotaka kuzungumzia ni kuongeza wigo wa kodi na tozo. Kwa mfano, hapa tulikaa kuzungumza katika Bunge hili tukatazama kitu kinaitwa capital gain tax…
(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa, tunaomba utulivu ndani ya Bunge.
MHE. KILUMBE S. NG'ENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, tulikaa katika Bunge hili tukazungumzia kitu kinaitwa capital gain tax ambacho kilikuwa kinatozwa asilimia 10. Mtu anauza nyumba yake kwa shida lakini anatakiwa apeleke asilimia 10 ya mauzo yake kwa Serikali. Serikali ikasikia hoja za Waheshimiwa Wabunge ikashusha kutoka kwenye asilimia 10 mpaka asilimia tatu. Ninaipongeza sana Serikali, na ninafikiri na wenyewe wanaona namna ambavyo watu sasa hawakwepi capital gain tax. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini bado kuna tatizo kwenye withholding tax ya rental. Watu wenye nyumba za kupangisha sasa wamekuwa wengi na apartments zimekuwa nyingi, lakini wengi bado wanakwepa kulipa withholding tax kwa sababu bado mmeacha asilimia 10 kwenye withholding tax ya rental. Mimi nilipwe kodi ya nyumba 2,000,000 nichukue 200,000 nipeleke Serikalini. Tulitazame tena eneo hili. Unapotaka kuongeza wigo wa walipa kodi unachokifanya ni kuangalia wingi wao kisha unapunguza ile kodi ili walipe wengi badala ya wengi kukwepa kodi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili nilitaka nije hata kwa bodaboda. Leo uchunguzi unaonesha kwamba asilimia takriban 80 ya bodaboda hawana leseni; na hawana leseni si kwa sababu wanapenda, hawana leseni kwa sababu kipato chao ni kidogo na leseni ni bei kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunachanganya haya mambo, hawa wanaoendesha vyombo vya moto wamegawanywa katika mafungu duniani kote. Anayerusha ndege juu anaitwa pilot ambaye sisi tunamwita rubani, ana leseni yake. Anayeendesha meli anaitwa captain sisi tunamwita nahodha, ana leseni yake. Anayeendesha treni ana leseni yake anaitwa operator maana treni ni kama vyombo vingine, ni kama grader ni kama nini wanaitwa ma-operator. Anayeendesha gari anaitwa dereva, anayeendesha pikipiki haitwi dereva anaitwa rider. Leo hatuna leseni ya rider tunampa driving license, ambayo ni ya mwendesha gari, kwa ku-categorize tu. Kwa hiyo mimi ninachoomba sasa ni kwamba Serikali ije na leseni za rider, kuwe na riding license ambayo kiwango chake kiwe shilingi 20,000. Hawa asilimia 80 wote ambao walikuwa hawalipi sasa watalipa na tutapata fedha nyingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unakumbuka Bunge hili kwa kuangalia uzito na kipato cha kila eneo tuliiomba Serikali na Serikali hii ni sikivu ikaamua hata makosa ya barabarani, haya ya magari yanatozwa 30,000 kwa kila kosa lakini ya pikipiki Serikali ikasikia ikaleta hadi shilingi 10,000. Vilevile leseni kwa ajili ya rider iwekwe shilingi 20,000, watalipa wengi tutapata fedha nyingi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka nimalizie suala la kuipongeza Serikali kwa kuangalia jinsi ya kuongeza mapato ya kikodi kwenye nishati ya gesi. Hili ni eneo ambalo mmeliangalia na mimi kwa kweli naunga mkono. Isipokuwa, siungi mkono kabisa kabisa hoja ya kutoza kodi kwa AMCOS. Hawa ni wakulima tena wakulima ambao sisi tunajua namna ambavyo wanapata shida kubwa sana na vilevile mazao yao hayana uhakika wa bei. Kila mwaka wanaomba Mungu sijui watakutana na kitu gani huko mbele; sasa wamejiunga katika ushirika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tufike mahala tuangalie maeneo haya niliyoyataja ambayo yanaweza yakatuongezea kodi kwa kiasi kikubwa. Kwenye withholding tax ya rental kwenye gesi, sawa lakini kwenye AMCOS hapana. Yaani hawa watoto wanaanza kuinuka tu; umezaa mtoto umemuona tu anaanza kupendeza unaanza kumtafutia mchumba, haiwezekani. Suala la msingi hapa tuache ushirika ukue kwanza. Baada ya kusema hayo. Ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)