Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia katika Bajeti hii Kuu ya Serikali. Awali ya yote napenda kumshukuru sana Mungu kwa kunipatia nafasi ili na mimi niweze kusimama leo na kuchangia katika Bajeti hii Kuu ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuipongeza sana Serikali kwa jinsi ambavyo imeweza kuwasaidia vijana wetu, hasa wa vyuo vikuu kwa kuwapatia mikopo na fedha nyingi sana na kuwawezesha vijana wengi sana wa Kitanzania kupata fursa ya kusoma katika vyuo vyetu vikuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo hii ya vyuo vikuu imekuwa msaada mkubwa sana tangu imeanza kupatikana katika nchi hii ya Tanzania. Wengi tuliosoma katika vyuo vikuu hivi tupo hapa kwa sababu ya hii mikopo. Hivyo, basi, mimi niendelee tu kuisisitiza Serikali yetu sikivu iwapatie wanafunzi wetu mikopo kwa wakati sahihi, na wale waliojipambanua kwamba wanahitaji hii mikopo kamili wapate kwa asilimia 100 na kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee pia kuipongeza Serikali kwa jinsi ambavyo inaendelea kuboresha miundombinu katika vyuo vyetu vikuu majengo yajengwa, vyuo vikuu vingi vinapata miundombinu mizuri sana. Sasa naomba leo mchango wangu nijikite katika kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundisha katika vyuo vyetu vikuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, udahili wa vyuo vikuu umeongezeka, na hii imetokana na uboreshwaji wa elimu katika nchi yetu. Sekondari zimejengwa nyingi na wanafunzi wengi sasa wamehamasika kusoma. Kwa hiyo, wanafunzi hawa wanakuwa na ndoto nyingi sana za kufika vyuo vikuu. Hivyo basi, ni vizuri sasa Serikali ikaangalia jinsi ya kuboresha vyuo vyetu vikuu ili viwe tayari kuwapokea hawa wanafunzi wengi ambao wanakuja katika miaka ya hivi karibuni. Kwa sasa hivi kumekuwa na ongezeko kubwa sana la wanafunzi, takribani 150,000 wanajiunga na vyuo vikuu. Udahili huu ni vizuri ukaenda sambamba na miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua ya kwamba ardhi inabaki pale pale lakini wananchi wanaongezeka. Hali kadhalika ndivyo ilivyo katika vyuo vikuu. Vyuo vikuu vipo pale pale lakini wanafunzi wanaongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hali halisi iliyopo sasa hivi ni kwamba miundombinu ya vyuo vikuu vingi hasa vya umma haiendani sambamba na uongezeko la wanafunzi. Hapa tunamaanisha miundombinu kama mabweni. Ni hivi, vyuo vyetu vikuu sasa vinapokea asilimia 30 tu ya wanafunzi wanaolala katika mabweni ya vyuo vikuu, wanafunzi wengine wanalala nje, hii ni changamoto. Wanatafuta vyumba nje ya vyuo vikuu ambavyo vinakuwa mbali huku wanafunzi wakikumbana na changamoto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikichukulia mfano wa Chuo Kikuu cha MUHAS wanafunzi wengi wanakaa mbali na hivyo wanakumbana na changamoto za usafiri na vilevile wanakumbana na changamoto za kuishi nje ya chuo. Hivyo, wanakuwa na changamoto ya kuwa vizuri katika masomo yao na hutumia muda mwingi katika kufikiria mambo mengine nje ya masomo yao. Hivyo basi ninaishauri Serikali katika bajeti hii ijaribu kuongeza vyumba vya mabweni katika vyuo vyetu vikuu ili wanafunzi waishi katika sehemu ambazo zinaeleweka, wapate mahitaji yao katika sehemu inayoeleweka na waweze kujifunza masomo yao na kuyazingatia vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuhusiana na kumbi za mihadhara katika vyuo vyetu vikuu; ni kwamba wanafunzi wanaongezeka lakini kumbi za mihadhara ni zile zile na zikiongezeka hali kadhalika haziendi sambamba na uwiano wa wanafunzi. Kumbi za mihadhara ndizo sehemu ambako pia wanafunzi wanafanya mitihani yao ile ya monthly test, quarter test. Sasa wanafunzi ni wengi sana katika kumbi hizi, hata mhadhiri kuwasimamia inakuwa ni ngumu kuhakikisha kwamba kweli mwanafunzi anafanya hii mitihani peke yake bila kupata usumbufu mwingine wa kuwa karibu na mwingine wakati wa mitihani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hali kadhalika labda niseme tu kwamba kuna suala la motisha kwa wahadhiri wetu, jambo hili ni changamoto. Ninaishukuru sana Serikali angalau safari hii ongezeko na madai ya wahadhiri wetu imetimizwa, na wahadhiri kwa kweli wanaishukuru sana Serikali kwa kupata malimbikizo ya mishahara yao, na hata wale wanaostaafu kupata stahiki zao kwa wakati. Ninaishauri Serikali jambo hili liwe endelevu, lisiwe tu suala la kipindi fulani halafu kipindi fulani wahadhiri hawapati malimbikizo yao ya mishahara au stahiki zao zingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, kuhusu ofisi za wahadhiri; Serikali iliangalie jambo hili. Maprofesa siyo sahihi kabisa kukaa chumba kimoja na wahadhiri wengine. Maprofesa ni watu ambao wana kazi nyingi, hawa maprofesa wanafanya utafiti, hawa maprofesa wanafanya machapisho mbalimbali na hawa maprofesa ndio ambao wanafunzi wa Masters na PhD huwaona mara kwa mara kwa ajili ya kuweza kupata consultation ya kuwaona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wanapokuwa katika ofisi ambazo zimechanganyikana na wahadhiri wengine ni changamoto. Huyu mhadhiri anataka document zake zikae vizuri katika ofisi yake, ahakikishe kwamba vitabu vyake vipo. Si vyema maprofesa jioni kuanza kukusanyakusanya vitu vyao na kwenda navyo sehemu nyingine. Kwa hiyo, naomba nishauri sana Serikali iangalie kwa kuhakikisha wahadhiri wanakaa katika ofisi nzuri na ambazo zinaweza kukidhi mahitaji yao kulingana na taaluma zao. Ahsante sana; nami ninaendelea kuishukuru Serikali na ninaunga bajeti hii mkono kwa asilimia 100. (Makofi)