Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, nianze kwa kumshukuru Mungu kwa fursa ambayo nimeipata tena leo kuwa sehemu ya wachangiaji katika bajeti kuu ya Serikali pamoja na hii ya mipango.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze moja kwa moja kwa kuunga mkono hoja kama zilivyowasilishwa japokuwa kutakuwa na machache ambayo nitayazungumzia. Nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo ameweza kuendelea na uwekezaji mkubwa katika miradi ya kimkakati, miradi ambayo inakwenda kuongeza pato la Taifa katika kila eneo ambalo uwekezaji huu umefanyika. Nipongeze pia katika vipaumbele ambavyo alivyoweka mojawapo katika taarifa walizozitoa hapa ni kuimarisha uwezo wa uzalishaji wa viwandani na utoaji pia wa huduma ambazo ni bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuimarisha uwezo wa uzalishaji wa viwandani, kumewekwa msukumo mkubwa katika suala zima la ukamilishaji wa miradi ipo na ambayo ile inaendelea na tunaiona kwa mfano Bwawa la Mwalimu Nyerere limeshafikia asilimia zaidi ya 95. Kwa hiyo, hiyo moja hapa likikamilika tunaimani umeme unakwenda kusambaa maeneo yote na mpaka sasa hivi upande wa REA wamefanya kazi nzuri mno, almost vijiji vyote lakini kuna maeneo mengine kuna changamoto kubwa kutokana tu na wakandarasi waliopewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaelekea kwenye uchaguzi, moja ya eneo ambalo linaweza kutuangusha kama hatutaangalia ni upande wa REA vijijini na vitongojini hasa kwa wakandarasi ambao wamepewa maeneo, na ukizingatia kanda ya ziwa kule kazi haziendi vizuri zinasuasua, tungeomba sana hili liangaliwe ili kuweza kusogeza hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala zima la tozo hasa kwenye maeneo ya uvuvi, nampongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa aliyofanya katika kuwawezesha wavuvi wa Ziwa Victoria lakini pia hata kule bahari kuu kwa maana ya Bahari ya Hindi. Ametoa vitendea kazi vizuri na vingi ambavyo vinawafanya waende kufanya kazi yao vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto inayokuja, tozo ni nyingi sana kiasi kwamba wanashindwa namna bora ya kuweza kuendelea. Kuna tozo ya asilimia mbili ya mazao ya samaki ambayo ilikuwepo na mwaka 2021 tozo ile ilifutwa na ilifutwa baada ya wavuvi kuandamana kuja kuonana na Kamati ya Bunge na tozo ile ikaondolewa lakini leo tozo ile imerudi; na tozo ile kama hatukuangalia inakwenda kutupeleka kubaya kwa sababu tozo ile pia ilifilisi wavuvi wengi, ikafanya wengi waachane na biashara, viwanda vingi vya samaki vilifungwa kwa kukosa rasilimali, sasa leo tena tunairudisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ningeomba sana Serikali, changamoto tuliyoipata wakati ule 2021mpaka tozo ikafutwa sidhani kama imepata muamala wa kuweza kuendelea kuirudisha tena, ningeomba sana Serikali iangalie. Lakini naipongeza kwa kushusha tozo ile waliyokuwa wameanza kutoza kwenye mazao ya samaki kutoka shilingi 10 ilipanda mpaka 100 sasa hivi wamepunguza wameenda kwenye 50, nashukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tozo ya kusafirisha mabondo nayo imeshuka kutoka 3,500 kwa kilo mpaka 2,800 kwa mabichi mabondo, makavu yameshuka kutoka 2,500 mpaka shilingi 2,000 kwa hiyo, hiyo nayo imesaidia. Changamoto ipo katika suala zima la usafirishaji wa mabondo hayo, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu wakati anatoa hotuba yake alizungumzia habari ya kutumia pesa za Kitanzania kwa maana ya shilingi lakini upande huu bado wameacha kutoza kwa dola kwamba wanatoza kwenye mabondo mabichi dola 3.7 ilikuwa dola 2.7 sasa inakuwa dola 3, makavu ilikuwa dola 3.3 sasa inakuwa dola 3.5. Hii inawafanya wavuvi waendelee kuyumba katika suala zima, ni kipi wanatakiwa kutozwa na ukiangalia wanatozwa zaidi ya 15 ambazo zipo pale, ningeomba sana tozo hii iangaliwe ili kuweza kuona jinsi gani tunaenda kuwasaidia wavuvi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nirudi kwenye gesi, kwa kweli suala la gesi ile huduma bado tunahangaika kuhamasisha halafu leo hatujawa na maeneo mengi ya kufunga ile mifumo, wataalamu wapo wachache na tunahimiza habari ya kuwa na clean energy kama askofu alivyosema. Leo hii tukiwapandishia tunataka pia kurudi nyuma suala ambalo Mheshimiwa Rais amekuwa champion wa mambo ya clean energy na Taifa na globally wanaufahamu. Sasa kwa nini tunataka kurudi nyuma? Tungeomba sana, bado uhamasishaji unaendelea na hata magari ya Serikali yenyewe bado hayajafungwa, waliofungiwa ni wachache, huduma bado vituo ni vichache, leo tunawapandishia. Ningeomba sana hilo lisiwepo kwa sababu linatupeleka nyuma na kuturudisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nipongeze Serikali kwa masuala ya zero rate katika suala zima la wauzaji dhahabu wanaouza kwenye benki kuu, tuna imani watakuwa wengi na utoroshaji utapungua, kwa hiyo tunaipongeza. Lakini pia pamoja na wale wanaouza dhahabu katika vile viwanda vya uchakataji, tutakwenda kuimarisha viwanda vyetu, tutakwenda kuongeza ajira. Kwa suala hilo kwa kweli naipongeza Serikali kwa sababu ni mambo ambayo yalikuwa na changamoto, watu wanatorosha dhahabu kwa sabau ya kukwepa kodi. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mabula kengele ya pili ahsante.
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, kengele ya kwanza?
NAIBU SPIKA: Kengele ya pili.
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru naomba tu nisisitize kuna mchango wangu nimepeleka kwa maandishi kuhusiana na namna ya kuingiza vyanzo vingine vya ukuzaji wa uchumi kwa kutumia sekta ya nyumba pamoja na milki ni sekta ambayo imesahaulika na inaweza ikatuongezea pato kubwa la Taifa, ahsante sana. (Makofi)