Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.

Hon. Saashisha Elinikyo Mafuwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hai

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hoja iliyoko mezani. Kwanza kabisa nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote, mnafanya kazi nzuri pamoja na Naibu Mawaziri, lakini mahususi ni Mheshimiwa Nyongo, kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kila mara tunaposhauri hapa anatusikiliza na anafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuwa nikishauri mara kadhaa kwamba, tunaomba Serikali iwe na mpango wa kuanzia miaka 50, miaka 100 na kuendelea. Mheshimiwa Rais amelipokea hili na kesho nina swali linalohusu ombi hilo, nitaliondoa kwa sababu, tayari Mheshimiwa Rais ameshajibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninampongeza Profesa kwa Hotuba yake nzuri, unaona kabisa hii imeandikwa na Profesa. Nampongeza sana, lakini ninawaomba, ninafahamu Wizara hii, Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Waziri wake ni nani. Ninafahamu vizuri sana, lakini ninaomba mapema kabisa mnapoanza ofisi hii, Mheshimiwa Nyongo na Mheshimiwa Waziri, mjue hili eneo ni Wizara nyeti sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninashauri hata wakati wa kujadili hii Wizara ingejadiliwa peke yake. Ikae peke yake, tupate muda wa kuijadili peke yake, wawe na nguvu, ili isionekane kazi ya Wizara ya Mipango ni ku-compile taarifa za Wizara nyingine. Tunatakiwa tuwape nguvu, wawe na uwezo wa kupanga mipango yetu na iheshimiwe na Mawaziri wote. Hili ni muhimu sana, vinginevyo watakuwa na kazi ya ku-compile mipango ya Waheshimiwa Mawaziri na hawatakuwa na nguvu ya kuweza kuwa-question, kuwasimamia na ku-reject mipango ambayo haiko kwenye utaratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuweze kuwa na vitu endelevu, mpango ukianza mwaka huu undelee kwa kipindi cha miaka 50 na kuendelea. Pia, nashauri kwamba, Wizara hii inatakiwa iwe na watumishi wasio wa kawaida kwenye routine activity. Tutafute team, mwaka jana nilishauri hapa ikiwenzekana tuwe na intellectual team, wakae vijana watulivu wenye uwezo mkubwa, wajifungie kwa utulivu waweze kupanga mipango ya nchi yetu. Tukiamua kuichukulia Wizara hii kama Wizara nyingine, tutakuwa hatujamsaidia Mheshimiwa Rais na lengo lake la kuanzisha Wizara hii ili tuwe na mipango ya Taifa inayotekelezeka litakuwa haijatimia.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu namna ambavyo kuna routine activity, siku hizi ni bahati mbaya sana hata wakuu wa taasisi akichaguliwa akikaa siku mbili/tatu anaanza kuwaza Ubunge na siasa. Tupate watu ambao ni free from politics, ambao watasimama, watalipwa vizuri, waweze kusaidia nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mwigulu, Waziri wa Fedha, tumekuwa na changamoto ya fedha kutokwenda, lakini nasema hebu tutoke kwenye routine activity za kutafuta kodi kila mahali, eneo lilelile. Viko vyanzo vipya, mimi nakutajia vyanzo vipya hapa ukavitafute, ukaviboreshe, lakini mwisho wa siku naomba zile fedha zilizopangwa kwenye Bajeti ya Kilimo zipewe kipaumbele. Fedha za umwagiliaji, ile shilingi trilioni 1.2 iliyopangwa kwenye Wizara ya Kilimo iende na mimi nilimuahidi Mheshimiwa Waziri wa Kilimo kwamba, nitamsaidia kudai hii pesa. Kwa nini nasema hii pesa iende?

Mheshimiwa Naibu Spika, asilimia 65 ya Watanzania wamejiajiri kwenye kilimo. Kwa hiyo, ukipeleka pesa kwenye kilimo, umwagiliaji utakuwepo na watu watalima, kwa maana hiyo tutaongeza uchumi. Formula ya kukuza uchumi ni kuongeza productivity na productivity inapatikana kwa Watanzania walio wengi kwenye eneo la kilimo. Sasa pesa unazipata wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekushauri hapa mara kadhaa kuhusiana na remittance, nchi nyingi kama Comoro, Nigeria, South Africa na Egypt wanafanya vizuri kwenye eneo hili. Mbona sisi kwetu haweki kipaumbele?

Mheshimiwa Naibu Spika, kila tunapozungumza hapa mnarudi kwenye mambo yale yale, soda, bia, sijui vinywaji gani. Tunazungumza nendeni kwenye remittance, nchi nyingine wanapata fedha nyingi, lakini Mheshimiwa Deo Ndejembi ana kazi ya kufanya hapa kutafuta ajira kwa Watanzania huko nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi ukienda nchi nyingine, ukishuka pale Dubai Mall ukiangalia wale walinzi wanaolinda pale na wanaotoa huduma ni wenzetu, wanaongea Kiswahili, lakini siyo Watanzania. Sasa sisi tunashindwa nini kwenda ku-capture soko na kupeleka watu wetu huko? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumesikia nchi jirani hapa imepeleka wauguzi nje ya nchi na tunaambiwa kuna nchi nyingi duniani, yuko mchangiaji mmoja alitaja hapa, ambazo zinahitaji watumishi. Sasa Wizara inayohusika na ajira wahakikishe wanaenda huko nje ya nchi kutafuta masoko, ili vijana wetu waende kuajiriwa, ili tuweze kupata fedha nyingi zinazotoka nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, liko jambo lingine hapa kuhusu hewa ya ukaa. Haya yote ni maeneo ambayo Serikali inatakiwa kuchangamka tutoke kwenye mambo ya kukimbizana na wananchi na wafanyabiashara wadogo wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hewa ya ukaa hii ni dili duniani na watu wanapata fedha nyingi. Sasa sisi hapa kwetu Tanzania, eneo ambalo lina sifa ya kuingia mkataba ni hekta milioni 45. Waziri wa Mazingira, Mheshimiwa Selemani, yuko pale anaona na anafahamu jambo hili, lakini eneo ambalo tumeingia mkataba ni hekta milioni 1.8 tu, eneo lingine lote ambalo ni asilimia 00.1. Sasa tunashindwa nini ku-capture hizi pesa? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mafuwe, kengele ya pili hiyo.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba sana Serikali itusaidie, lakini pia kwenye...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mafuwe, kengele ya pili.

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)