Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilwa Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa nafasi hii nikielekea kuchangia Mpango na Bajeti ya 2024/2025. Awali ya yote nimshukuru Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye sisi Wana-Kilwa tulipopata majanga ya mafuriko mwanzoni mwa mwezi Mei mwaka huu Mheshimiwa Rais akatoa maelekezo juhudi za haraka zichukuliwe ili kuweza kurudisha miundombinu katika hali yake ya kawaida. Kwa hiyo kwa upekee wake nimshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimshukuru Mheshimiwa Bashungwa ambaye alikuwepo uwandani kwa kipindi chote mpaka hali imetengamaa. Vilevile kwa upekee wake nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye Kitengo cha Maafa cha Serikali ndiyo kipo chini yake na kwa kweli alitupa ushirikiano wa kutosha na tumepata misaada ambayo angalau imekidhi haja kutoka Serikalini.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa upekee nimshukuru Mheshimiwa Waziri Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Mheshimiwa Jenista. Nishukuru Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi na Mheshimiwa RC Lindi Mheshimiwa Zainab Telack, nimshukuru Mheshimiwa DC wa Kilwa, Mheshimiwa Nyundo na Kamati yake ya Usalama ambayo kwa kweli walikuwa bega kwa bega kipindi chote cha majanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru Halmashauri yangu ya Wilaya ya Kilwa chini ya Mkurugenzi wetu, dada yetu Hanan Bafagih ambaye kwa kweli alishirikiana vizuri na wananchi na msaada ambao ameweza kuutoa kupitia halmashauri yetu. Mheshimiwa Rais aliungwa mkono katika juhudi hizi na taasisi mbalimbali za ndani na za nje ya nchi. Kwa hiyo wale wote ambao wameunga mkono katika kusaidia kupunguza majanga ya maafa haya tunawashukuru na hapa nitawataja kwa uchache wakiwakilisha wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Taasisi ya Blue Springs, Kampuni ya Bin Shomari Tanzania Limited iliyopo hapa Tanzania lakini kwa upekee wake Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Tingi Mheshimiwa Rajab Ngatanda ambaye yeye ndiyo alikuwa anaratibu pamoja na taasisi hizi ili kuona kwamba misaada ya kibinadamu inawafikia wananchi wetu waliyopata mafuriko.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hao Waheshimiwa Madiwani wetu katika kata zote ambazo zote ambazo majanga haya yalitokea nitumie fursa hii kutoa shukrani zao ikiwemo: Mheshimiwa Chijinga wa Kata ya Masoko; Mheshimiwa Kinjokwile wa Kata ya Kikole; Mheshimiwa Matajiri wa Kata ya Mandawa; Mheshimiwa Rukia Jamadar, Viti Maalumu; pamoja na Mheshimiwa Fatuma Kindamba au Mama Mpulu naye ni Diwani wa Viti Maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Taasisi za Kidini nazo hazikuwa nyuma katika kutakua changamoto zilizotokana na majanga haya ikiwemo BAKWATA, Kanisa la AICC-Kilwa, Kanisa la PFCT Kilwa pamoja na taasisi zetu ikiwemo NMB Kilwa, TRA Kilwa, MSD pia na watu binafsi walikuwa mstari wa mbele. Tunatoa shukrani kwa wote ikiwemo Umoja wa Wafanyabiashara wa Masoko pale Kilwa Masoko. Watu binafsi kwa upekee wake ambao walitupa ushauri na hususan mimi binafsi nilipata ushauri ni kutoka kwa mtangulizi wangu wa nafasi hii Mwakilishi wa Jimbo la Kilwa kusini Mheshimiwa Seleman Bungala alinipa ushauri wa karibu sana katika kuona kwamba tunaendea vipi utatuzi wa changamoto hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya shukrani hizi nianze mchango wangu katika bajeti hii. Kwanza kwa kutoa rai Serikalini kuwa na mipango ambayo haileti madhara kwa wananchi wetu. Wakati tunapitisha mpango wa tatu wa maendeleo hapa tulipitisha uboreshaji na upanuzi wa viwanja vya ndege 12 vikiwemo viwanja viwili vya Kilwa Masoko pamoja na Kiwanja cha Ndege cha Nachingwea. Kwa masikitiko niseme tu kwamba viwanja hivi wananchi wetu bado hawajapewa fidia baada ya tathmini ambayo imeshafanyika kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano Nachingwea mpaka sasa hivi wananchi 113 bado hawajalipwa shilingi bilioni 3.4. Tunasubiri nini, Serikali inasubiri nini kutekeleza kitu ambacho walipanga wenyewe wakati tunapitisha Mpango wa Tatu wa Maendeleo? Wananchi wangu wa Kilwa Masoko wapatao 447 wana-cover vitongoji viwili mpaka leo bado hawajalipwa fidia yao kiasi cha shilingi bilioni sita na ushee hivi. Serikali inasubiri nini kulipa fidia kwa wananchi wetu hawa ambao wameendelea kupata madhara baada ya tathmini kufanyika?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni zaidi ya mwaka sasa wamekumbwa na mafuriko, hawana makazi Serikali inasubiri nini? Suala hili mimi hapa Bungeni nimelizunguma hapa Bungeni nimelizungumza mara kadhaa. Nimelizungumza katika swali la msingi namba 18 Mkutano Kumi na Tatu, Kikao cha Pili tarehe (01 Novemba, 2023). Nimelizungumza katika swali la nyongeza namba 30 Mkutano wa Kumi na Nne, Kikao cha Pili (tarehe 31 Januari), 2024. Nimelizungumza wakati nachangia Hotuba ya Waziri Mkuu Mkutano huu wa Kumi na Tano, Kikao cha Tatu (tarehe 04 Aprili). Pia nimelizungumzia kama swali la msingi, niliuliza swali la msingi namba 76 Mkutano wa Kumi na Tano, Kikao cha Sita, tarehe 15 Aprili mwaka huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini majibu ya Serikali ni kwamba tukipata fedha tutalipa. Niseme tu kwamba Wananchi wa Kilwa wataona mpango huu una maana na bajeti hii ina maana endapo Serikali itakuja kutoa tamko hapa haraka iwezekanavyo wananchi hawa wa Kilwa, Nachingwea na viwanja vingine vilivyofanyiwa tathmini wakalipwa haraka iwezekanavyo iili kuondoa adha inayoendelea. Tarehe 15 Februari mwaka huu timu ya wajumbe kadhaa ikiwemo wawakilishi wa wahanga wa tathmini hii, walikuja hapa wakakutana na uongozi, wakakutana na Serikali ikiwemo Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Fedha mwenyewe Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na akawaahidi kwamba atawalipa haraka iwezekanavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia bajeti hii nakumbusha wananchi wangu hawa waweze kulipwa fidia yao ili mambo mengine yaendelee...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Ally. Mheshimiwa Kavejuru Eliadory Felix...
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)