Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.

Hon. Agnes Mathew Marwa

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na mimi kwa kuchangia Wizara hii ya Fedha. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anazifanya katika Taifa hili la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze Rais wa Mapinduzi Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi kwa kazi nzuri anazozifanya lakini kuleta mapinduzi makubwa Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niende moja kwa moja kwa kuishauri Serikali kuhusiana na masuaa haya ya tozo. Moja kwa moja, naishauri Serikali hili zuio la asilimia mbili kwa wakulima ni jambo ambalo mimi kama Mbunge ningeshauri ni jambo ambalo haliwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuwa tunatafuta pesa sehemu mbalimbali tukumbuke kwamba hawa wakulima kwanza wanalima kilimo cha shida sana, wanalima kilimo cha gharama za chini sana, lakini pia kwao pesa kidogo ni tatizo sana. Hata kukopesheka benki ni shida, ni majuzi juzi tu Mheshimiwa Rais alisababisha sasa wakulima wameanza kukopesheka na Waziri wetu Mheshimiwa Bashe, lakini bado wakulima wana hali mbaya sana. Kwa hiyo mimi niiombe Wizara hii tozo ya asilimia mbili kwa wakulima wetu iondolewe, siyo jambo zuri.

Mheshimiwa Naibu Spila, pia, hii tozo ya asilimia mbili kwa samaki, jamani tunajua kabisa kwamba wavuvi wa Tanzania, masoko yenyewe hawana, maeneo ya kwenda kuuza hizo samaki kwa gharama ambayo inaweza ikawarudishia fedha ya kutosha hawana, sasa hata hiki kidogo wanachokipata pia tuwanyang’anye? Mimi nadhani kwa kweli tunapaswa kuangalia ni sehemu gani tunaweza tukatafuta hizi fedha lakini kwa hawa wakulima, kwa hawa wauza samaki au hawa wavuvi nadhani hizi tozo ziondolewe, zisirudishwe tena maana wauza samaki, wauza dagaa, wakulima, kwa ujumla maisha yao yanajulikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania bado hatujafikia hatua ya kwamba sasa tumefikia tumepata masoko ya hali ya juu kiasi kwamba wakaingiza fedha za kutosha. Kwa hiyo, ombi langu kwa Serikali ni hilo, kwanza tuondoe hii tozo ya asilimia mbili, tuwaondolee kwanza hao wakulima, tuwaondolee wavuvi lakini tuondoe kwenye samaki ili na sisi sasa tufaidi samaki zetu za Tanzania pia hawa wavuvi wafaidi uvuvi wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami pia niendelee kumpongeza Waziri wetu Mheshimiwa Bashe, maamuzi aliyoyafanya ya kuleta sukari wakati ule wa mwezi mtukufu ambao wote tulikuwa tumefunga waislamu na wakristo, mimi nafikiri ni jambo zuri sana, alitumia maamuzi mazuri sana kama baba, siyo mpaka usubiri uone nyumba inaungua mpaka muende mkakae kikao cha ukoo ndiyo muanze kuamua kwamba tufanye nini. Yeye moja kwa moja akafanya maamuzi na tukapata sukari ambayo kwa kipindi hicho ilikuwa ni adimu sana kwa kweli tunakushukuru sana na tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu maana mfungo wetu ulikuwa mzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende kwenye suala la wafanyabiashara. Wafanyabiashara wetu wa Tanzania tunatamani sana watoe hizi tozo lakini wanapokuwa wanatoa hizi tozo basi sisi tuwafanye watoe ziwe tozo rafiki zinapokuwa tozo rafiki mimi naamini watatoa, siyo kwamba hawahitaji kutoa isipokuwa tozo zimekuwa nyingi sana zinawazidia, zinapowazidia hapo ndipo inapotokea wengine wanajificha wengine wana maduka ya nyumbani.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona nchi za wenzetu tunapotoka kwenda nje, tukienda nje wewe mwenyewe utaitoa tu kwa sababu hata yule mfanyabiashara kutokana na mazingira aliyotengenezewa ana uwezo wa kuitoa kutokana na kwamba, kwanza iko chini, ni bei nafuu, lakini ni rafiki. Sasa hivi tukiingia uadui na hao wafanyabiashara linakuwa siyo jambo zuri sana. Mimi naamini kabisa Serikali yetu ina nia nzuri sana ya kukusanya kodi, hata kwenye biblia kodi imeandikwa, kwenye misaafu imeandikwa. Kwa hiyo, hata Mwenyezi Mungu anakubaliana na kodi. Mimi niwaombe sana wafanyabiashara wa Tanzania tukae chini tukubaliane kukaa chini na Serikali yetu, tuongee tuwaambie ni kodi ipi ambayo kwetu ni reasonable kwa maana ya sisi tunaweza tuka-afford kuitoa ili tuweze kufanya biashara vizuri lakini na Serikali ikusanye kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Serikali tukakae na wafanyabiashara tukae tuangalie hizi tozo tukazipunguze, tuwape tozo nafuu ambazo wanaweza kulipa kila mmoja, kila Mtanzania aweze kulipa kodi ili tusiwe na mivutano huku na huku. Mimi naamini kabisa mpaka sasa hivi mivutano inayoendelea yawezekana baadhi ya wafanyabiashara kuna kodi ambazo zinawazidia na ndiyo maana wanakuwa wanavutana na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naenda moja kwa moja kwa kumshukuru na kumpongeza sana Rais wangu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri sana alizozifanya katika Taifa hili la Tanzania. Mkoani kwangu Mara, Mama yetu tunakupongeza sana, tunakuombea sana, Mama yetu Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Marwa, ahsante.

MHE. AGNES M. MARWA: Niiombe sana Wizara sasa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Marwa, muda wako umekwisha, ahsante.

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)