Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia.
Mheshimiwa Spika, nimepigiwa simu mara kadha wa kadha na wananchi ambao ni wafanyabiashara wa Mkoa wa Mbeya na mahala pengine. Nimepigiwa simu, wanalalamika kwa namna ambavyo Serikali imeeleza kuhusu faini ya milioni 15, na kama siyo faini ya milioni 15 basi mtu anakwenda kutumikia kifungo jela.
Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyabiashara wetu hawa walio wengi mitaji yao inaweza ikawa milioni nne, milioni tano. Hata hivyo, kwa sababu na wao wanajua na kutambua kwamba wanatakiwa kutoa kodi, risiti na yote hiyo ni kwa ajili ya manufaa ya ujenzi wa Taifa letu hili la Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi sana hizi mashine za EFD zinaweza zika-stuck. Hizo mashine zikigoma wanapeleka kwa wahusika ili wawarekebishie na hivyo waweze kutoa risiti. Utakuta mtoaji ama mtengenezaji wa mashine hiyo anakuwa hayupo yuko safarini anasema atarudi baada ya siku mbili au siku tatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa watu hizo fedha wanakuwa wamekopa. Kwa namna ambavyo wanataka maisha yaweze kuendelea akimpatia mfanyabiashara risiti ya mkono ili kama anakaa maeneo ya jirani aje kuchukua risiti ya EFD pale ambapo EFD machine itakapokuwa imetengemaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hapa katikati mfanyabiashara huyu akipatikana na tatizo la kutotoa risiti inakuwa ni tatizo kubwa sana. Sasa hapa kama anachukuliwa hatua ya faini ya milioni 15, mtaji wake ni milioni nne au milioni tano hizo fedha atazitoa wapi? Wananchi wetu wa Tanzania tunawajua kabisa jinsi ambavyo wanajihangaisha kwenye shughuli hizi za biashara. Tutalundika wafanyabiashara wangapi kwenye magereza?
Mheshimiwa Naibu Spika, hii Serikali yetu ya Awamu ya Sita ya mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Rais wetu, ni mama mwenye hekima, ana busara, upendo na ana mapenzi mema kwa Watanzania wake. Hapendi kuona Watanzania wanapata matatizo au wanaingia kwenye shida.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninadhani na ninatumaini kwamba inawezekana hili jambo ni Wizara ya Mipango na Wizara ya Fedha ndio ambao wamelileta. Mheshimiwa Rais mama yetu kipenzi ambaye anawapenda sana Watanzania wake na wao wanampenda sana tunaomba aliangalie na kulirekebisha jambo hili la faini za milioni 15 ili wafanyabiashara hawa waweze kuendelea kufanya biashara zao kama jinsi ambavyo walikuwa wakiendelea kufanya kama nchi ilivyotengemaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania wetu hawa walio wengi ni wazalendo. Maana tunajua kwamba nchi bila kodi hakuna kinachoendelea. Nchi bila kodi hatujengi hospitali, barabara, hatufanyi chochote, na kwenye masuala ya elimu kutakuwa kumelala.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninashauri sana Serikali iliangalie kwa umakini suala hili la faini ya milioni 15 ama kifungo cha kwenda jela kulingana na sisi wenyewe Watanzania tulivyo. Wafanyabiashara wa Mkoa wa Mbeya na baadhi ya mikoa mingine; na bahati mbaya sana nilipita hata Dar es salaam; maduka yamefungwa. Nilishangaa kwa nini nikaambiwa ni kwa sababu ya hii faini na kwamba hawataweza kulipa faini hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nashauri kwamba, Serikali mkae vizuri sana na hawa wafanyabiashara kurekebisha utaratibu ili kufikia mwafaka na kazi ziweze kwenda. Pia, ukizingatia kwa mfano pale Dar es salaam nchi nyingi zilifika ili kununua mizigo ili wapeleke kwenye nchi zao, wanabaki wameduaa na wanashangaa. Hii siyo sawa, kiasi kwamba tunaweza tukapoteza mapato mengi ambayo yangetakiwa kuingia Serikalini kutokana na mauzo yale, lakini sasa ilishindikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana na ninamwomba sana Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mama yetu huyu ambaye ana hofu ya Mungu; siamini sana kwamba hili jambo alikuwa analielewa vizuri; ninamwomba sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mama yetu tunayemwombea kila siku kwa Mwenyezi Mungu namna anavyoiongoza nchi yake hii ya Tanzania na Serikali yake yote kwa ujumla kuwaangalia hawa wafanyabiashara wa Taifa hili la Tanzania hususani wafanyabiashara wa Mkoa wa Mbeya ambao hawana mitaji mikubwa kiasi hicho. Tunamshukuru sana kwa sababu tunaamini atakwenda kufanya vizuri vile ambavyo anawajua Watanzania wake, kwamba ni masikini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, ahsante sana.