Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.

Hon. Eric James Shigongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kunipa nafasi ya kusimama katika Bunge hili Tukufu ili niweze kutoa mchango wangu kwa Taifa langu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na Buchosa. Sisi Buchosa tunahitaji barabara yetu ya lami kutoka Sengerema hadi Nyehunge ijengwe. Kwa hiyo, nimetumwa na wananchi wangu, kwamba fedha zitengwe ili barabara ile iweze kujengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili nataka nizungumzie Taifa langu Tanzania. naipenda sana nchi hii, na ushahidi wa uoendo wangu kwa nchi yangu ni uamuzi wangu wa kumwita binti yangu jina Tanzania. Kwa hiyo hayapo mashaka ya kwamba mimi ninaipenda nchi yangu sana.


Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii, nisome data kidogo tu, kwa utalii Duniani ni ya pili, Afrika ni ya kwanza kwa utalii. Nchi yangu kwa makaa ya mawe ni ya 50 Duniani, kwa gesi asilia ni ya 82 Duniani, Tanzania kwa dhahabu ni ya 22 Duniani, kwa Helium ni ya kwanza Duniani, kwa almasi ni ya 10 Duniani, kwa Tanzanite ni ya kwanza Duniani, Tanzania ni nchi tajiri sana hatuwezi kuwa maskini hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaposikia mtu anasema nchi yangu maskini, mimi huwa sikubaliani na hilo jambo na sitaki watoto wa nchi hii waelewe nchi yao ni masikini, nchi yetu ni tajiri sana hatuwezi kuwa jinsi tulivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Venezuela ni nchi ya kwanza Duniani kwa mafuta, inafuatiwa na Saudi Arabia, na Urusi ya tatu lakini Venezuela ni nchi masikini sana kuliko Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nataka nimpongeze Rais wetu wa Awamu ya Sita kwa uamuzi wake wa kutumia sekta za uchumi kuongeza Pato la Taifa huo ni uamuzi wa Rais wetu kwamba amaeamua sekta zote za uchumi zichangie Pato la Taifa ili pato la Mtanzania mmoja mmoja liweze kuongezeka nampongeza sana Mheshimiwa Rais na Waheshimiwa Wabunge na Mawaziri niwaombe tumuunge mkono Rais ili sekta zote za uchumi ziweze kuchangia Pato la Taifa hatuwezi kuwa maskini kwa utajri tulionao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwapongeze Wabunge na nikupongeze wewe kwa uamuzi wa Bunge hili kupambana kubadilisha Sheria ya Manunuzi. Tumebadilisha Sheria ya Manunuzi na Kanuni zimebadilika kwamba kuanzia tarehe 01, Julai hakuna mgeni yeyoye anayefanya biashara ya bilioni 50 kushuka chini kwenye nchi hii. Tumefanya jambo jema sana tutakumbukwa kwa uamuzi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumedalili Sheria ya Manunuzi, Kanuni lakini kuna jambo moja tusipolifanya mabadiliko haya hayatatusaidia chochote. Benki zetu za Tanzania zibadilishe mtazamo wake kwa wafanyabishara wazawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika nchi hii benki zetu hazitaki kuwekeza sana kwenye biashara zinataka kuwekeza kwenye mikopo ya wafanyakazi na watu wadogowadogo. Hauwezi kutajirika kwa fedha yako mwenyewe kuitoa laki moja kwenda milioni moja ni rahisi. Ila kuitoa bilioni moja mpaka bilioni 100 ni kitu kimoja kigumu sana you have to use the bank, lazima tutumie fedha za watu wengine. Kanuni ya utajiri inasema hivi use other people’s money sasa wenye pesa ni benki, kama benki zetu hazitabadilisha mtazamo wake kuwasaidia wazawa wa nchi hii waweze kuchukua fedha na kufanya biashara mabadiliko haya ya sheria tuliyoyafanya hayatasaidia chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba leo nitoe elimu kidogo, naomba nitoe elimu ndogo tu ya kitu kinachoitwa triangle of money ambayo matajiri wote wa nchi hii wanaitumia pembe tatu ya pesa upande mmoja ni A, upande wa pili ni B na upande wa tatu ni C iko chini, naomba nisikilizwe vizuri A ni mtengenezaji wa bidhaa B ni mnunuzi na C hapa chini ni mfanyabiashara. Sasa mfanyabiashara anaingia mkataba na TFC kwa kuiuzia labda mbolea, watakubaliana kwamba tutanunua nao mbolea tutalipa kwa siku tisini, mfanyabiashara huyo anaenda kuongea na mtengezaji wa mbolea yuko China au Urusi wanakubaliana atalipa kwa siku 120 anadaiwa kwa siku 120 analipa kwa siku 90. Matokeo yake hapa ni kwamba kama mbolea ni ya milioni 100 mimi sina milioni 100 nitaenda benki. Benki inatengeneza back-to-back LC yaani back-to-back LC ni kwamba inaingia mkataba na mnunuzi atalipa kwa siku 90 benki inaingia mkataba na muuzaji wa mbolea atalipa basi 120, maana yake ni nini? Nitalipwa na Serikali siku 90 kabla sijadaiwa na mtengenezaji wa mbolea maana yake hapo ni nini? Unatengeneza pesa bila kutumia pesa lakini benki lazima ikae nyuma yangu kunisaidia, benki zetu haziko tayari kufanya jambo hilo ni waoga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba CRDB wamejitahidi lazima niwapongeze na Mheshimiwa Bashe nimpongeze sana amewasaidia sana wafanyabiashara kwenye korosho kule kutumia mfumo huu Mtanzania anafanya biashara ya bilioni 100 anasaidiwa na benki tutumie mfumo huu kuwatajirisha Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania wamechoka kuwa masikini, mimi mwenyewe nimechoka kuwa masikini. Nataka Watanzania watajirike kwa sheria hii kwa sababu hawana mtaji benki ziwe tayari kufungua back-to-back LC kuwasaidia ili huu mfumo wa pembe tatu ya fedha niliousema uweze kusaidia, hauhitaji pesa kupata pesa na hili jambo lazima lieleweke. Kama benki zinaogopa basi Serikali iwe tayari kutoa government guarantee kwamba kwenye korosho unahitaji bilioni 300 Serikali itoe karatasi peke yake government guarantee kuzipa benki ili ziwakopeshe Watanzania waweze kufanya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hilo lieleweke na kama jambo hili likifanyika nakuhakikishia Watanzania watabadilika, tumechoka kuwa maskini lazima jambo hili lifanyike tusaidie tuweze kutoka hapa tulipo. Kwa hiyo, kuendelea kuona wageni wanakuja hapa kila siku wanatajirika sisi tunaendelea kuwa maskini hatutaki na sisi hatutaki kuchukia siku moja tuweze kuwa kama nchi nyingine, tunataka amani ya nchi yetu iendelee kuwepo na Watanzania waendelee kunufaika na nchi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema hivi mambo manne ya kufanya kuisaidia nchi yangu la kwanza Sekta za Uchumi zichangie Pato la Taifa. Lazima tuhakikishe jambo hili linafanyika kama utalii umechangia Mheshimiwa Rais amecheza sinema mapato yameongezeka kutoka Dola milioni 900 mpaka Dola bilioni tatu ndani ya miaka mitatu iwe hivyo kwenye uvuvi, madini na kilimo nakuhakikishia tukifanya hivi iko siku tutapunguza mikopo tunayokopa, tutapunguza budget deficit na kesi ya bajeti inapungua tutatumia fedha zetu kujiletea maendeleo wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni suala zima la Sheria, Sheria zetu tulizonazo ziwe zinatoa fursa kwa Watanzania wazawa kufanikiwa, Sera zetu za Uchumi tuzipitie upya. Inawezekanaje mfanyabiashara wa Kitanzania akafungue duka Zambia? Inawezekanje mfanyabiashara wa Kitanzania akasajiri malori yake Rwanda? Kuna shida mahali fulani hapa ndani lazima tupitie upya tariff zetu ziwe za ushindani inawezekanaje ukanunie mashuka Kenya? inawezekanaje ukanunue mashuka Uganda? Kuna nini hapa kwetu ambacho kinakosewa? Tutazame upya sera zetu za Uchumi na sheria zetu ziwe ni zinazoshindana na nchi jirani tunapigwa bao tukiwa tunaona? Haiwezekani tukaendelea namna hiyo kama kweli tuna nia njema ya kuendeleza nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni upendo kati yetu sisi wenyewe Watanzania tupendane, Watanzania tubebane haiwezekani akaja mtu kutoka China akafanikiwa mimi Mtanzania nikabaki chini. Nchi yetu imefika mahali ukitaka kazi mahali fulani unalazimika kumkodisha mzungu wa kukodisha. Wako wazungu wanakaa Serena pale wanalipwa Dola 500 kwa saa, akaonekane mzungu ili wewe Mtanzania upate kazi, naomba Watanzania tupendane tushirikiane sisi kwa sisi ili tuweze kuinuka kwa pamoja katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni law enforcement, Sheria tunatunga, tuzisimamie ili kwamba sheria hizi wanaozivunja wapate adhabu inayowastahili. Haiwezekani watu unakusanya fedha zinaliwa watu wanaiba halafu bado hawawezi kidhibitiwa na sheria zetu. Tuna sheria nzuri sana, tuna Sheria ya Manunuzi nilishaisema, tuna Sheria ya Utakatishaji Fedha, Sheria ya Fedha, Sheria ya TAKUKURU, sheria hizi zote zikisimamiwa sawasawa tutawadhibiti wote wanaoiba fedha zetu kutakakuwa na hofu na woga kwenye fedha za umma hatuwezi kwenda hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huko nyuma niliwahi kushauri kwamba tutafute utaratibu wa kuwachapa watu wanaoiba fedha za umma. Sasa mimi ninashauri tuongeze idadi ya magereza kwa watu wanaoiba fedha za nchi yetu…

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Eric.

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana. (Makofi)