Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.

Hon. Munde Abdallah Tambwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia bajeti iliyopo mbele yetu. Awali ya yote na mimi nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kunisimamisha mbele ya Bunge lako Tukufu niweze kuchangia bajeti ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya. Hakuna asiyejua wala asiyetambua kazi kubwa inayofanywa na Mheshimiwa Rais, tunampongeza sana na tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu azidi kumpa hekima busara na afya ili aendelee kuwatumikia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri wa Fedha kaka yetu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba kwa bajeti nzuri aliyoileta hapa lakini nimpongeze Waziri wetu wa Mipango kaka yetu Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo na yeye kwa taarifa nzuri ya mipango hakika taarifa imekaa kiprofesa-profesa taarifa ni nzuri sana tunakupongeza sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuchangia moja kwa moja kuhusu Tabora, nikienda kwa ujumla kwa Tabora naomba niongee kwa sababu muda ni mchache. Niombe sana Serikali pale Tabora Manispaa tuna kata za ndani na kuna kata za nje, zile kata zetu za nje karibia zote zinazozunguka Manispaa yetu ya Tabora barabara zake ni chakavu ni mbaya zinahitaji kabisa kwa makusudi mazima kuangaliwa kwa upya at least ziwe na lami. Kwa sababu pale ni manispaa lakini pia ni mkoa wa siku nyingi sana, wa zamani, hakika ni aibu kubwa kuwa na mkoa kama ule wa miaka mingi ambao mpaka leo baadhi ya kata zake barabara hazipitiki tunaomba Serikali ituangalie kwa jicho la pekee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tena watu wa TAMISEMI kama wapo hapa watanisikia pale Tabora tuna soko letu zuri tulijengewa na Serikali ya wamachinga, soko lile liko chini kabisa lilipauliwa vibaya wafanyabiashara wote wanafanyia biashara zao nje ya soko. Masika linajaa maji kiangazi jua ni kali, kwa hiyo ndani wametoka kabisa wameliacha. Niombe Serikali itufanyie dharura kuhakikisha tunapata pesa za kujenga soko lile vizuri la wamachinga, Waziri wa TAMISEMI kama yupo hapa ananisikia ninaomba sana mdogo wangu Mheshimiwa Zainab Katimba nimekuona ikiwezekana baada ya Bunge hili tuongozane mimi na wewe kwenda Tabora Manispaa kuangalia soko lile la wamachinga, hali yao ni mbaya wanashindwa kufanya biashara vizuri hawana sehemu nzuri ya kufanyia biashara. Mheshimiwa Rais ametoa fedha amewasaidia sana wamachinga lakini watendaji wetu hawakuwatendea haki. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri nimekuona twende tuongozane Tabora wakati una-wind up uniambie ili tukalikague lile soko la wamachinga pale Tabora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze sana Serikali kwa mabadiliko pia ya procurement kuhakikisha wageni wanapata kazi kuanzia bilioni 50 kwenda mbele, hili ni jambo jema la kuwajali Watanzania na Watanzania hakika wameona Serikali yao inavyowajali na kuwasaidia tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongee suala moja la EFD receipt, ukifanya biashara yoyote na Serikali au na kampuni yoyote unaambiwa upeleke invoice na EFD machine ukipeleka ukifika kule unaweza ukalipwa baada ya miezi minne au mitano lakini wakati huo umeshai-print EFD kwa hiyo, wewe inabidi ile EFD uilipie VAT, TRA lakini wewe hujalipwa ile pesa. Niiombe Serikali hatukatai kulipa kodi, maana ni wajibu wa kila mtanzania, lakini sasa EFD ipelekwe wakati mimi nataka kulipwa pesa, yaani sasa kesho kutwa unalipwa lete EFD ili tukulipe pesa zako. Lakini ukichukua EFD kabla sijalipwa, hamtendi haki kwa wafanyabiashara wanabaki na madeni makubwa lakini bila kujua kwamba wamepata pesa, inabidi akakope ili alipe EFD. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongee sasa Sheria ya Sukari na mimi nichangie kama Wabunge wenzangu walivyochangia. Kwa ujumla niipongeze Serikali kwa kuleta hapa Sheria ya Sukari, niiombe Serikali wakati Waheshimiwa Wabunge wanaipitisha sheria hii ya sukari cha kwanza tumuombe Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, tunaomba wenye viwanda wote wawe na mawakala kwenye mikoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakala wako Dodoma, Dar es Salaam na Mwanza imagine mtu anatoka Tabora ana duka lake la rejareja la sukari apande bus aende Mwanza anunue mifuko 10 ailete Tabora akifika Tabora bei ya sukari lazima iwe imepanda. Kwa hiyo, tunaomba kabisa kwenye sheria wahakikishe wenye viwanda wanakuwa na mawakala kwenye mikoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niombe kwenye sheria hiyo itakapokuwa inatungwa inaletwa hapa Bungeni wawe wametupa bei elekezi ya sukari tupate bei elekezi ya sukari tujue sukari itauzwaje kwenye mikoa yetu lakini pia iwe na bei elekezi ya kununua miwa kwa wauza miwa kama tani ni 70,000 au ni 100,000 basi iwe inaeleweka ili pia kuwalinda wale wakulima wanaouza miwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni jambo la kushangaza sana unapoona sukari kwenye nchi yetu ni bei kubwa lakini Rwanda sukari iko chini, Malawi sukari iko chini, Zambia sukari iko chini, unajiuliza tatizo ni nini na sisi tuna viwanda, tuna mashamba ya miwa, Rwanda hawana hata kiwanda lakini sukari iko chini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, imefika wakati sasa Serikali ijue gharama ya uzalishaji wa sukari kwenye kiwanda kilo moja inazalishwa kwa shilingi ngapi? anaifikisha sokoni kwa shilingi ngapi? kwa nini sukari hii inakuwa bei kubwa Tanzania Malawi bei ndogo, Zambia bei ndogo, Rwanda bei ndogo, tatizo ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana tuiombe Serikali tumuombe Waziri na wataalamu wake watuambie kwa nini sukari Tanzania inakuwa bei kubwa na kwenye sheria waandike labda ni lazima kila baada ya mwaka wabadilishe na kutuonyesha gharama za uzalishaji wa sukari ukoje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la sukari limekuwa kubwa ni lazima sasa tujikite kuhakikisha kwamba tunaenda nalo vizuri lakini pia naunga sana mkono Serikali kuileta sheria hapa Bungeni kwa sababu hatuwezi kuachia tu vitu hivi ambavyo Watanzania wote karibia almost asilimia 90 ya Watanzania wanavitumia viwe tu mikononi mwa wafanyabiashara wachache, je, siku yoyote imetokea market failure? Mfano imetokea mvua kubwa kama iliyotokea miwa ikawa imebebwa na maji unamwambia sasa ndio nampa kibali kaagize sukari anaagiza sukari unaambiwa kuna vita Gaza meli inazunguka kutoka Brazil, meli inachukua miezi mitatu huku kuna mvua hatuna stoke yoyote ya sukari kama Serikali utawaambia nini Watanzania? Watanzania watalaumu tu wakiona sukari 10,000 huwezi kuwaambia eti oooh, nimewapa kibali wafanyabiashara bado sukari haijafika, bado sukari sijui meli imezunguka, lazima Serikali ijitosheleze kwa chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwenye jukumu la kujua usalama wa chakula wa nchi hii ni Serikali, mwenye jukumu la kujua sukari nyingi au ni ndogo ni Serikali, mwenye jukumu la kujua tuna stoke ya kutosha ya sukari ni Serikali. Huwezi kuja Waziri ukatuambia kwamba eti sukari hakuna na mimi nilikuwa sijui wenye viwanda wamefungia sisi hatutakuelewa. Kwa hiyo, hili ni jukumu la Serikali kuhakikisha linashika mikononi hiki kitu wanaki-control si unaona hata kwenye mafuta kuna baki ile ya mafuta wanaleta kwa procurement ile lakini kuna mtu ana control anajua kwenye baki mafuta yamebakia kiasi gani, nani kachukua mafuta kiasi fulani, nani anauza mafuta kwa bei gani, yaani kila kitu kinakuwa kiko open na kuna mtu anajua.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo ukiwauliza EWURA watakuambia kuna mafuta nchini kiasi fulani. Petrol station kwa mfano wanayo kiasi fulani na bei ya kuuzia ni hii bei imepanda kwa shilingi hizi kwa nini imepanda bei imeshuka kwa shilingi hizi kwa nini imeshuka. Niombe sana kwenye sukari waige mfumo huo na iwe wazi ili Watanzania wasije wakaingia kwenye janga hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa kilimo kaka yangu Mheshimiwa Hussein Bashe kwa ujasiri wake aliokuwa nao kwa uzalendo mkubwa aliouonyesha na amewaonyesha Watanzania. Siku nyingine sisi Waislam tunaambiwa useme Alhamdulillah’ kwa kila jambo. Tulivyomuona Mheshimiwa Mpina anafanya yale watu wakasikitika wengine lakini kumbe Mwenyezi Mungu alitaka aonyeshe ukweli wake na ukweli umebainika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, basi kwa kusema hayo naunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)