Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manonga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi kuweza kuchangia kwa siku ya leo. Kwanza nipende kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambayo ameendelea kulifanyia Taifa letu. Tumeona mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere limeongeza megawatt za uzalishaji wa umeme wa Taifa, lakini tumeona juzi Treni ya Umeme imeanza kazi kutoka Dar es Salaam kuja Morogoro kwa hatua ya awali. Kwa hiyo, ni mafanikio makubwa sana tunaipongeza Serikali kwa hatua hizi kubwa ambazo zimefanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nina yangu machache tu ambayo nataka Wizara hii ya Fedha iweze kutusaidia, kwanza Mheshimiwa Waziri umeona kumekuwa na uhaba sana wa dola. dola imekuwa ni changamoto na wewe kama Waziri unapaswa uangalie ni namna gani ambavyo dola hii inatakiwa ipatikane kwa wingi kama ilivyokuwa zamani. Kukosekana kwa Dola kunaleta changamoto kubwa sana hasa kwa wafanyabiashara na hii baadae inaleta athari ya bei ya bidhaa mbalimbali kupanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo ukienda benki wanakuambia dola wanauza 2620 nenda waambie naomba dola wanakupa kiwango kisichozidi dola 500 au Dola 1000.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi mfanyabiashara au wafanyabiashara wanaoweza kuagiza mafuta, kuagiza bidhaa nje ya nchi wanahitaji dola kuanzia labda 100,000 mpaka 1000,000 hawazipati. Lakini wakienda mtaani wanapata Dola, wanaipata dola kwa bei ya juu mpaka 2820, sasa kama mtaani dola zinapatikana huku kwenye mfumo rasmi dola hazipatikani hebu Wizara muangalie namna gani ambayo mtarahisisha upatikanaji wa dola mrahisishe maisha ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maisha ya Watanzania yanakuwa ghali kwa sababu ya ukosekanaji wa dola, sasa Mheshimiwa Waziri na timu yako mtusaidie dola ni changamoto na ni kero kubwa inawezekana ziko changamoto lakini Kenya wamefanyaje wameweza? Kwa nini sisi tushindwe kufanya mbinu ambazo majirani zetu wamefanya na wamefanikiwa ni kweli walikuwa nayo changamoto lakini sasa hivi changomoto hizo tena hawana sisi tuombe Serikali na Wizara mjipange muone ni namna gani ya kuweza kuhakikisha kwamba dola inapatikana na kwa bei ambayo ni katika rate ambayo ni reasonable. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Wizara ya Fedha wanatoa fedha wanatuambia wametoa fedha za miradi ya maendeleo mfano wanatuambia kwenye halmashauri zetu tumepewa fedha za kufanya miradi mbalimbali. Lakini hizo fedha hazitoki sasa tunaziangalia figure tu tunazo hela, lakini hela hazitoki kwenda kwenye miradi, mwezi wa nne hakuna fedha, mwezi wa tano hakuna fedha, mwezi wa sita hakuna fedha miezi mitatu hiyo na mwezi wa sita ukifika mwisho tarehe 30 tunafunga tunaanza mwaka mpya. Kwa hiyo, tena mwaka mpya kuna miezi mingine mitatu mnatulia wa saba, wa nane na wa tisa na ukichukua miezi mitatu ya mwanzo na miezi mitatu hii inakuwa miezi sita maana yake katika halmashauri miezi sita hakuna kazi yoyote inayoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Waziri na timu yako hebu fungulieni hiki kipindi kilichobakia hizo hela zilizopo tunazozisoma ziweze kutoka, kuna watu wanapata tabu. Mheshimiwa Waziri labda hufahamu kuna wazabuni wamefanya kazi pamoja, halmashauri hawapati fedha hawalipwi na halmashauri. Halmashauri inasema fedha tumeambiwa hizi hapa lakini uwezo wa kuzilipa hakuna kibali hamjatoa Mheshimiwa Waziri toeni vibali ili halmashauri ziweze kufanya kazi na wazabuni waweze kulipwa na maisha ya Watanzania yaendelee kuboreka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine Mheshimiwa Waziri wa Fedha nataka nikukumbushe Waziri wa Fedha sisi kule kwetu tuna Barabara ya Choma kuja Ziba kuja Puge inapita Nsimbo na Nkinga hii ni barabara kubwa ambayo kila mwaka tunaahidiwa kujegwa kwa kiwango cha lami, 2015 tuliahidiwa, 2020 imo mpaka kwenye Ilani ya CCM leo ni mwaka wa nne tunakaribia kwenda wa tano hatujapewa fedha za ujenzi wa barabara hii ya lami. Mheshimiwa Waziri wa fedha tumeona unatoa fedha kwenye barabara mbalimbali nchini hii ya kwetu utatoa fedha lini?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Mheshimiwa Waziri katika majibu yako utuambie maana yake Waziri wa ujenzi anasema mimi sina tatizo Wizara ya Fedha wanatakiwa watoe fedha. Sasa Mheshimiwa Waziri wa Fedha toa fedha ili barabara hiyo iweze kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami vinginevyo maana yake tutakwenda 2025 sijui tutaenda kuwambia nini tena wananchi, fedha ziko wapi, tunawaambia fedha tunazo, haya leteni mjenge tunawaambiwa Wizara ya Fedha, haiwezekani, mtatupa wakati mgumu sana kwenye uchaguzi. Niombe sana Mheshimiwa Waziri ujitahidi katika bajeti hii ambayo tumeipitisha au tunaenda kukupitishia kesho uhakikishe fedha za barabara ya lami ya Choma - Ziba - Nkinga - Nsimbo mpaka Puge unatoa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara ya lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri nadhani utakuwa umenielewa au utasahau? Maana yake najua una mambo mengi sijui jambo gani tukuambie ili ukumbuke kwamba hii barabara inatakiwa itolewe fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, juzijuzi tulipata matatizo pale ya mabasi na yanaanguka kule maeneo ya Shinyanga wale wagonjwa mmewaleta kule Nkinga na mnatembea vizuri kwenye barabara ya lami mkifika Ziba kuwapeleka Nkinga barabara ni ya vumbi mbaya kwelikweli na ni rough mnawapeleka Ndala kule kwa Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla barabara yenyewe mbaya kwelikweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunauliza nyinyi wagonjwa mnawatoa kwenye lami mnawaleta kwenye Hospitali ya barabara ya vumbi si wengine wanakufa njiani hata kabla hawajafika hospitalini halafu inakuja helkopta kutoka Dar es Salaam inakuja kuwachukua wagonjwa kwenye hospitali ya rufaa lakini hospitali ya rufaa haina barabara ya lami. Sasa Mheshimiwa Waziri haujaona umuhimu wa hii barabara kuwekewa lami kweli? Hebu niombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Naibu wako, na timu yenu tunaomba fedha ya barabara ya lami mtupe tumechoka kusubiri kipindi kirefu. Tumeona hata ile Mheshimiwa Waziri pale kwako unaanza utaratibu wa kuweka lami sasa na mimi nafurahi kwa sababu ni shortcut ya Ndagu kutokea Singida unaweka lami na sherehe kubwa ilifanyika na mimi naomba mfanye sherehe kubwa pale kwangu Jimboni Manonga Ziba na kwa Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla kule Ndala barabara ya lami Mheshimiwa Waziri ni Serious maana yake haya mambo tunaona tu kwenye video maeneo mengine na sisi tunapenda mambo kama haya mazuri yafanyike kwetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nakukaribisha sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba pamoja na Mheshimiwa Chande nakumbuka uliwahi kupiga push up pale Ndala na ulipiga pushup pale Nsimbo mwaka 2015 na 2020. Sasa 2025 utakuja kupiga pushup au utakuja kufanya nini tena? Maana yake unakujaga pale kuomba kura kwa wananchi sasa sijui utakuja? Au hauji safari hii. Maana yake uliowaambia utawajengea lami ni wewe na 2015 ni wewe na 2020 ni wewe, sasa 2025 utakuja na staili gani? utapanda punda au utapanda nini Mheshimiwa Waziri Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba tunaomba lami toa fedha Wizara ya Fedha toeni fedha ili tujenge barabara ya lami Barabara yetu ya Ziba - Puge hii barabara tumeisema miaka yote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii barabara tunaisema kila siku tunaomba na sisi tupewe fedha tujenge barabara ya lami kero yangu kubwa ni hiyo Mheshimiwa Waziri kwenye hii bajeti mmetupa lakini tunaomba utekelezaji fedha zitoke mwaka jana mmetuandikia mnatupa mwaka juzi mmeandika mnatupa sasa mwaka huu mzitoe hizo hela ili tuende kwenye utekelezaji. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Haya ahsante Mheshimiwa.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia naunga mkono hoja. (Makofi)