Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Nne na Mkutano wa Kumi na Tano, pamoja na Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Mbili na Mkutano wa Kumi na Tatu

Hon. Eng. Dr. Leonard Madaraka Chamuriho

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Nne na Mkutano wa Kumi na Tano, pamoja na Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Mbili na Mkutano wa Kumi na Tatu

MHE. ENG. DKT. LEONARD M. CHAMURIHO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia mchango huu kuhusu Ripoti ya Kamati yetu. Pia ningependa kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutuongoza vizuri katika nchi hii, hasa kwa kuanzisha falsafa zake mpya za 4R. Vile vile, kuendeleza utawala unaozingatia sheria ambao unajumuisha sheria ndogo ambazo ni sehemu au jukumu la hii Kamati ya Kudumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa vile vile, kutoa shukrani kwa Mawaziri wote na Naibu Mawaziri ambao wamehudhuria katika vikao vya Kamati yetu, kwani ni sehemu muhimu sana ya majadiliano katika hoja ambazo huwa zinatolewa na Kamati. Wao hufika kutoa ufafanuzi wa sheria ndogo walizokasimiwa kuzitunga, ambazo kwa jicho la Kamati huonekana zina dosari ambazo inabidi zifanyiwe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tungependa kuwapongeza na kuwashukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambao huwa bega kwa bega na Kamati katika kutoa mwongozo wa kisheria na vile vile katika masuala ya kuwaongoza hao walioandika hizo sheria ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kanuni hizi au sheria ndogo ambazo huwasilishwa huambatana na majedwali. Majedwali haya ni muhimu sana kwani hurahisisha usomaji wa sheria ndogo na vile vile hujumuisha mambo yanayofanana na kuyaweka pamoja ili sheria iweze kusomeka na kutumika kwa vizuri zaidi. Hivyo basi, kama kuna dosari katika haya majedwali ya sheria ndogo inaathiri kwa kiwango kikubwa utekelezaji wa sheria ndogo na kwa namna moja au nyingine huleta usumbufu katika azma hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitajikita katika dosari zilizoonekana katika majedwali hayo na kutoa mifano mbalimbali ili tuone ni jinsi gani ambavyo majedwali hayo huathiri na yanavyoweza kuboreshwa zaidi. Nitatoa mifano michache.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano wa kwanza ambao nitautoa ni Tangazo la Serikali Na.1 la Januari, 2024 ambalo lina-rules under The Accountant Auditors Appeal Board ya Mwaka 2024. Ukiangalia jedwali la kwanza (a) kuna makosa ya kiuandishi ambayo yanarejea kanuni iliyoanzisha ambayo siyo yenyewe. Sasa, hapo katika utekelezaji, mtekelezaji akifika pale na kwenda kuangalia ni wapi anatakiwa ashughulike napo anakuta sipo na inaleta usumbufu kwani anaweza akaacha kuishughulikia, kumbe pale imeelekezwa kwa makosa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika sheria ndogo hiyo vile vile fomu (b) inatoa notice ya anwani za kutoa huduma ambayo ukiangalia zinapoelekeza sipo ambapo kanuni inataka kufanya hivyo. Hiyo inaleta usumbufu kwa yule ambaye anaitekeleza kwani akiangalia kanuni wezeshi anakuta kwamba siyo hiyo. Katika sheria hiyo utakuta kwamba hata fomu (c) (d) na (e) zina changamoto hiyo hiyo; hivyo unakuta kwamba umakini kidogo ulikosekana pale. Bila kurekebisha kanuni hiyo inakuwa ni kama haikukamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kanuni ya pili ambayo ningependa kuitolea mfano ni Tangazo la Serikali Na. 8 la tarehe 5 Januari, 2024 ambalo linahusu regulation under civil aviation facilitation of air transport ya Mwaka 2024. Haya nayo pia yanarejea katika jedwali la kwanza sehemu ya tatu na yanarejea kanuni iliyoanzishwa ambayo si yenyewe. Usumbufu ule ambao unakuja katika utekelezaji unatungwa kwenye jedwali, kufika kule unakuta jedwali lile silo linalohusika. Kwa hiyo, unaweza ukadhani kwamba jedwali hilo halipo kumbe lipo. Hilo litaleta changamoto katika utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mwingine ni Tangazo la Serikali Na. 908 la tarehe 22 Desemba, 2023, ambalo ni Sheria Ndogo ya Ushuru wa Masoko na Magulio Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba ya Mwaka, 2023. Katika sheria ndogo hiyo ya Mlimba kuna jedwali namba tatu ambalo limewekwa mara mbili lakini linaongelea maudhui tofauti. Hivyo, katika utekelezaji wake utakuta mtu ameambiwa aende jedwali namba tatu lakini akienda kule anakuta jedwali silo ambalo linatakiwa kufanya hivyo. Moja katika jedwali hilo namba tatu japokuwa hii ni kanuni ya Mlimba unakuta kwamba jedwali hilo linakuelekeza uende kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Rorya. Kwa hiyo, unakuta kwamba, makosa mengine yanaweza kuepukika kirahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mwingine ni Tangazo la Serikali Na. 921 la tarehe 22 Desemba, 2023 ambalo linahusu Sheria Ndogo ya Usafi, Afya na Hifadhi ya Mazingira ya Halmashauri ya Wilaya ya Arusha ya Mwaka 2023. Jedwali hili linaelezea viwango vya ukaguzi kwa ajili ya usajili, ukaguzi, kupima afya, kupulizia dawa na kadhalika. Pia, ukielekezwa ukienda pale unakuta viwango vya usajili havipo. Kwa hiyo, ndani ya kanuni unaambiwa viwango vya usajili vipo katika jedwali hilo, lakini ukienda pale unakuta viwango hivyo havikuwekwa. Kwa hiyo, hii inaweza ikaleta usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa sheria ndogo hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tangazo la Serikali Na. 96 la Mwaka 2024 linahusu Sheria Ndogo ya Hifadhi ya Mazingira ya Halmashauri ya Wilaya ya Magu ya Mwaka 2024. Hii ina jedwali la tatu ambayo inaonesha fomu ya kufifilisha kosa katika makosa yanayofanyika katika halmashauri hiyo, lakini ukienda katika fomu hiyo unakuta linataja halmashauri nyingine kabisa ambayo hata haipo. Kwa hiyo, unajikuta kwamba huduma ya kufifilisha kosa inakosekana kwa sababu ile fomu siyo husika na haiwezi kutumika katika azma hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mwingine ni Tangazo la Serikali Na. 209 la Mwaka 2024, ambalo linahusu Sheria Ndogo ya Usimamizi wa Maegesho na Vituo vya Vyombo vya Usafi ya Halmashauri ya Mji wa Mafinga ya Mwaka 2024. Katika sheria ndogo hii kuna jedwali la kwanza sehemu (b) linaweka viwango tofauti vya ushuru wa mabasi ya aina moja. Unakuta basi ambalo lina abiria wasiozidi 28 limewekewa ada tofauti na ada ya basi lenye uwezo wa kuchukua abiria 28 katika jedwali hilo hilo. Basi la aina moja lakini lina ada katika viwango viwili tofauti. Kwa hiyo, hii katika utekelezaji inaleta changamoto kubwa ambayo inaweza ikaleta usumbufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jedwali hilo pia imetolewa ada katika sehemu (a) kipengele cha 13, ada ya shilingi 10,000 kwa ajili ya maegesho, lakini haisemi hiyo ada ni ya siku moja, wiki moja, mwezi mmoja au mwaka mmoja. Hiyo nayo inaweza ikaleta usumbufu mkubwa sana katika utekelezaji wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, tangazo lingine ambalo ningependa kulitolea mfano ni Tangazo la Sheria Na. 217 la Mwaka 2024 ambalo ni Sheria Ndogo ya Marekebisho ya Sheria Ndogo ya Ada na Ushuru wa Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara ya Mwaka 2024. Sehemu ya pili ya jedwali la kwanza limechanganya maudhui. Unakuta katika jedwali hilo linahusu ushuru wa kituo cha basi lakini humo humo unakuta kuna ushuru mwingine ambao hauhusiki upo katika jedwali lingine ambalo ni wa kuingiza malori mjini. Kwa hiyo, unakuta mtekelezaji anashindwa kuelewa atumie jedwali hilo au lingine hasa ukizingatia kwamba viwango vinavyowekwa huko ni tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mifano ni mingi, lakini ninaomba niishie hapo na niwapongeze sana Mwenyekiti wangu, Mheshimiwa Dkt. Jasson Rweikiza na Makamu wake Mheshimiwa Ramadhan Ramadhan kwa kutuongoza vizuri katika mwenendo wa Kamati yetu.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)