Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa nafasi hii ya kuchangia. Pia niungane na wenzangu na hasa Mwenyekiti wa Kamati yetu ya Sheria Ndogo kuanza kabisa kwa kuunga mkono hoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu wenzangu wamekwenda kwenye case specific, mimi nitakwenda kwenye mambo ya jumla ambayo tunafikiri yataweza kusaidia katika utungaji wa sheria hasa kwenye halmashauri zetu na kwa kuanza kabisa najua Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Ofisi ya Mwandishi wa Sheria pamoja na Wizara wanafanya juhudi kubwa sana kuhakikisha hizi kanuni au hizi sheria ndogo zinaleta tija. Sasa kwa sababu ya makosa ambayo tumeshayaona mara nyingi, nitoe ushauri wa jumla kwanza. Ni vizuri sheria zote za halmashauri zinazokuja hapa kabla hazijaingia kwenye Kamati Ndogo au wakati zinaingia Wabunge wa maeneo husika pamoja na kwamba ni Madiwani wapewe zile sheria na wao wazipitie.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninasema hivi kwa sababu zipo sheria ambazo either kwenye mchakato wake wa kutengenezwa kuna maneno yameingia katikati ambayo yanaenda kusababisha kero kwa wananchi; na Mheshimiwa Mbunge anaonekana yeye tayari ni Diwani na amezijadili wakati kiuhalisia Mheshimiwa Mbunge anakuwa hapa Bungeni kwa zaidi ya miezi saba kwa mwaka mzima na hivyo huenda kikao kilichopitisha sheria hizo yeye hakuwepo. Zikienda kuleta kero kule tayari na yeye zinamgusa moja kwa moja
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeyaona hayo kwa sababu baadhi ya Waheshimiwa Wabunge tuliowa-consult kwamba kuna sheria hii inataka kupita kwenye halmashauri yako tunaona iko hivi, unaona kabisa kwamba Mheshimiwa Mbunge hana taarifa. Kwa hiyo huo ni ushauri wa jumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wa pili ni halmashauri ambazo zina mchanganyiko wa maeneo yenye miji pamoja na maeneo yenye asili au yanayokuwa yana asili kama ya vijiji. Tumeona kwenye sheria za mifugo, sheria za kilimo pamoja na sheria za mazingira. Unakuta kuna halmashauri, hata Dar es Salaam, kwa mfano Temeke, kuna sheria ambayo ilikuwa inaelezea kuwa na limit ya mifugo na mifugo iwe na kitambulisho nadhani; lakini kuna maeneo katika halmashauri hiyo hiyo yana asili ya kijiji ambayo sheria hiyo ikienda, inaenda kusababisha matatizo. Kwa hiyo, ni vizuri sheria zisiwe generous hivyo ili ziweze kuleta tija zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wachangiaji wengi wameongelea ile sheria iliyokuwa inatoza kodi kwa wapaa samaki, wale wanaokwarua, wanakwangua au, wapaa samaki, sijui Kiswahili sahihi; ambapo walikuwa wanawa-charge shilingi 200 kwa kila mtu. Sasa ukiangalia zipo sheria zinazoelezea asilimia ya gharama za ukusanyaji wa kodi yoyote. Ukiangalia tu hawa hapa wa samaki ambao walikuwa wanatakiwa walipe shilingi 200 ukiangalia kale ka-rim kakuweka kwenye mashine ya EFD kale kashilingi 2,000 kanatoa risiti 100, kwa hiyo risiti mia moja kwa shilingi elfu mbili ukigawanya kale kakaratasi peke yake katakula shilingi ishirini. Hapa hatujapiga mahesabu ya wino, hatujapiga mahesabu ya mkusanyaji, hatujapiga mahesabu mengine yoyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, utaona kabisa hii kodi ambayo wenzetu walikuwa wanataka kuileta si tu wanaleta usumbufu kwa wale watu wa chini bali pia gharama yake ya ukusanyaji inaweza ikapita hata hiyo shilingi 100, shilingi 200, kwa hiyo, itakuwa haina hata tija kwenye makusanyo ya halmashauri hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na makosa ya jumla; kwa mfano, halmashauri inaleta kodi kwenye eneo ambalo haihusiki tena katika kusimamia. Kwa mfano, sheria ile iliyoletwa na halmashauri ya Mtwara Mikindani ya ku-charge lori kubwa kuingia mjini, si tu kwamba ilikuwa inaleta usumbufu zaidi kuliko wao walivyokuwa wanafikiria kupunguza msongamano, lakini ni dhahiri kwamba barabara za mijini nyingi ni tani 10, haya malori wanayoongelea ni tani 30, wao wanatoa tozo kwenda kukusanya hiyo hela wakati barabara ziko chini ya TARURA. Kwa hiyo, unaona kwamba wanakusanya kwenye eneo ambalo si lao.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mwingine ni kuhusu sheria ya ukataji barabara kwa ajili ya kupitisha miundombinu. Halmashauri inataka kukusanya lakini barabara ni mali ya TARURA. Kwenye hilo la lori kubwa ni kwamba wanakusanya kodi kwenye uvunjaji wa sheria na wala si faini. Maana yake ni kwamba mtu mwenye lori la tani 30 atalipa hiyo hela wanayotaka aingize lori lenye tani 30 likaumize barabara wakati sio mamlaka yao na barabara zimeshahama.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine, kuna halmashauri zinaleta sheria za ukusanyaji ushuru wa mauzo kwa mfano ya nafaka halafu wanasema bei itakayokuwa inatumika ni bei ya soko bila kuonesha ni bei ipi; ya soko, inayotolewa na Wizara, inayotolewa na Benki Kuu au inayotolewa na halmashauri yenyewe. Wanasema tutakusanya asilimia tatu kwa kilo kwa bei ya soko, lakini bei ipi ya soko inayopatikana kupitia chanzo gani. Kwa hiyo, haya yote yanaenda kuleta mkanganyiko.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la mwisho lililokuwa na mkanganyiko; halmashauri nyingi zimeleta sheria ya ukamataji mifugo na wanasema mifugo itakamatwa kwa siku kadhaa na kama fine haitalipwa watapiga mnada. Hata hivyo, kwa huo muda ambao wanakuwa na hiyo mifugo, hawakuonesha wajibu wa halmashauri kwenye kuhudumia hiyo mifugo, chakula, maji na baada ya hizo siku sita kama watakwenda kwenye mnada na mnada ukashindwa kufanyika kwa sababu bei ya soko haikufikiwa, ni nani ataendelea kusimamia hali ya hiyo mifugo kwa kipindi chote. Kwa hiyo, hayo ni mapungufu ambayo kiujumla yameonekana na yatakapoendelea kuboreshwa yatasaidia hizi sheria ndogo zije zikiwa na uhalisia zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)