Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Pandani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MARYAM OMAR SAID: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kusema neno katika hoja iliyoko mezani ambayo ni hoja ya Kamati yangu, Kamati ya Sheria Ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia nikaweza kusimama hapa muda huu. Nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuhakikisha Taifa letu la Tanzania tupo pazuri. Pia nimpongeze Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Mwinyi kwa kazi nzuri pia anayoifanya katika kuhakikisha Zanzibar inasonga mbele na inapata maendeleo yanayofaa. Nimpongeze pia Spika wetu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja nawe Naibu Spika na Wenyeviti wote kwa kazi nzuri wanazofanya kuhakikisha Kamati tunafanya kazi zetu ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sitokuwa msemaji sana kwa sababu wengi waliopita wameyazungumza mengi tu ambayo yanaonesha namna Kamati tulivyo makini katika kuhakikisha kanuni zinasimamiwa ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninawaunga mkono moja kwa moja wanakamati wenzangu katika kuhakikisha kwamba kanuni hizi zinasimamiwa ipasavyo. Kwanza, ukizingatia hizi kanuni zinatungwa na kwenda kutumika moja kwa moja kabla ya kuja kwetu. Hapa ndipo mwananchi anapoanza kuumia na ni vizuri sana Wizara zikazingatia kwamba wanapokuja kwenye Kamati waje na watu wa halmashauri, wataalam wetu wa sheria wa halmashauri kwa sababu wao ndio wanaozitunga hizi sheria. Mara zote mtu akiwepo pale tukiwa tunajadili itatupa urahisi zaidi katika kuhakikisha haumii anayetumia hizi kanuni, anayezisimamia, wala haumii mwandishi wa hizi sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wengi hapa wamezungumza namna gani Halmashauri ya Mtwara, nami niungane moja kwa moja na wenzangu kupinga Sheria Namba 217 inayohusu Halmashauri ya Mtwara, inayohusu mpara samaki. Mwenzangu mmoja hapa, Mheshimiwa Mhata amesema, chombo cha uvuvi kina leseni, kinalipa kodi, mvuvi analipa kodi, pale kwenye mnada kuna ushuru unatolewa, leo jamani na mpara samaki? Tukienda hivi na kesho tutasema kuwa kila anayekula samaki atoe ushuru. Jambo hili si sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naaibu Spika, nilifikiria nikasema, kwa mfano hii sheria inakuja kule kwetu Zanzibar na ikaja moja kwa moja Kaskazini ambako ndiko Jimbo langu lilipo, kule wapara samaki wengi ni wazee na ukienda siku za wikiendi utakuta ni watoto wadogo walioona ngoja nikatafute pesa yangu ya kutumia shuleni Jumatatu, ndivyo tulivyozoea, kiasi ambacho hata wewe mnunuzi wa samaki ukishanunua ukimpa yule mtoto kupara, mwisho wa siku pengine umempa shilingi 500, akakwambia mimi nitakuparia kwa shilingi 200, unaona huruma unamwachia na ile 500 yote na hudai chenchi. Leo hii Serikali pale tukaweke mkono tudai tena ushuru? Hili si sawa na tuachane nalo, wala tusilijadili sana. Hii Sheria tuachane nayo kabisa na Halmashauri ya Mtwara wasione kwamba tunawaonea, hii ni hali halisi na uhalisia ulivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini sheria kama hizi ambazo hazijafika huku kwetu ziko nyingi na ziko huko zinatumika. Wizara na Mwanasheria Mkuu wa Serikali tuongeze umakini katika kuhakikisha kwamba tunazisimamia hizi sheria tukizingatia kwamba zinakwenda kutumika ndipo zinakuja kwetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wamesema mengi hapa kuhusu makosa ya kiuandishi. Hebu mathalani jamani kwenye makosa ya kiuandishi, sheria hii imeanza kutungwa na Halmashauri pale kwa mtu wa sheria, ikaenda kwa Mwanasheria Mkuu ikaenda kutungwa mpaka inafika kwenye Kamati, kosa la kiuandishi jamani? Tuwe makini katika kuhakikisha kwenye hizi sheria tutapunguza haya makosa kama si kumaliza kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi sitaki niseme mengi kama nilivyotangulia kusema, wenzangu waliopita wameyazungumza mengi na mimi ni katika kukazia tu yale yaliyozungumzwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru na ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)