Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
Ex-Officio
Constituent
None
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nichukue fursa hii kukushukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia katika Taarifa hii nzuri. Pili, nimshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo, Mheshimiwa Dkt. Jason Samson Rweikiza pamoja na Wajumbe wa Kamati wote kwa kazi kubwa na nzuri waliofanya na kwa hii taarifa nzuri ambayo inatupatia picha halisi ya changamoto ambazo tunazo katika uandaaji wa Sheria Ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuelezea kidogo hali ilivyo kwa sasa katika zile Sheria Ndogo ambazo zimefikishwa kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa ajili ya uhakiki ili baadaye ziweze kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ya Kamati imeziainisha na ziko tatu. Pia, ingekuwa ni vema leo nikatoa hali halisi ilivyo sasa. Sheria Ndogo ya kwanza ilikuwa ni zile Kanuni za Shughuli za Uzalishaji, Upelekaji na Usambazaji wa Umeme za Mwaka 2023 ambazo zilifika kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uhakiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kulitaarifu Bunge lako kwamba, Kanuni hizi tayari zilishahakikiwa na zimeshatangazwa kwenye Gazeti la Serikali kwa matoleo mawili, Toleo la Kiingereza kupitia GN. No. 677 na lile Toleo la Kiswahili GN. No. 679) na Toleo hili lililotoka 9 Agosti, 2024.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna kanuni za The Accountants and Auditors Training and Examination Bylaws, 2023, naomba kulipa Bunge lako Tukufu kwamba, kazi hizi sasa ziko katika hatua za mwishoni, tumemaliza uhakiki na tunatarajia kutangaza siku ya tarehe 5 Septemba, 2024 kwenye Gazeti la Serikali kwa maana ya kesho Ijumaa. Kanuni zitakazosalia ni zile za ukusanyaji na uchakati wa taarifa binafsi ambazo ziko kwenye hatua za mwisho na nina imani kabisa kwamba, ndani ya muda uliowekwa na Kamati, kanuni hizi zitakuwa zimekwishatangazwa katika Gazeti la Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kusema tu kwamba, kimsingi Kamati hii imekuwa ikifanya kazi nzuri na kutokana na taarifa zao zimekuwa zikitusaidia kama Serikali katika kupunguza dosari na idadi ya Sheria Ndogo ambazo zimekuwa na matatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaona kwamba, katika taarifa hii idadi ya Sheria Ndogo ambazo zinakinzana na masharti ya Katiba zimepungua kutoka 13 na sasa ziko mbili. Kwa hiyo, hiyo ni dalili nzuri kwamba tukiongeza bidii katika kuyafanyia kazi mapendekezo yanayotolewa na Kamati, idadi ya Sheria Ndogo zinazopingana na masharti ya Katiba zinaweza kupungua kabisa kutoka mbili na kuwa sifuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, idadi ya Sheria Ndogo zinazokinzana na Masharti ya Sheria Mama na zenyewe zimepungua. Zilikuwa 27 wakati huo mara ya mwisho na sasa tunazo 10 tu. Vilevile, Sheria Ndogo zenye masharti yasiyoakisi uhalisia hapo bado tunahitaji kuongeza bidiii kwa sababu zilikuwa sita wakati ule na sasa ziko 22. Kwa hiyo, tunahitaji kujiuliza kuwa kwa nini zinaongezeka? Pia, Sheria Ndogo zinazoakisi makosa ya kimsingi ya uandishi huko tumeendelea kufanya vizuri maana zilikuwa ziko 70 na sasa ziko 13 tu. Kwa hiyo, hiyo ni dalili kwamba tunafanya vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria Ndogo zinazoakisi suala zima la utengenezaji wa majedwali, kwa mujibu wa sheria hizi zimeongezeka kutoka saba kwenda 13. Kwa hiyo, tunahitaji kuongeza bidiii zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeandaa mkakati mahsusi. Kwanza, ni kutengeneza Mwongozo kwa Mawakili wote wa Serikali nchini ili uweze kuwasaidia wanapotengeneza hizi Sheria Ndogo. Vilevile, watakuwa na orodha au checklist ambayo itakuwa inaainisha hayo mambo ya msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ni kufanya mafunzo kwa Mawakili wote wa Serikali nchini, lakini na mafunzo kwa Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali. Mafunzo Mahsusi kwa ngazi ya Diploma na ngazi ya Masters ili Mawakili wa Serikali waweze kuwa vizuri na tunaamini kwamba kwa kufanya hivyo, changamoto hizi tutazipunguza.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nikushukuru tena kwa kunipa nafasi hii, ninakuahidi na niliahidi Bunge lako Tukufu kwamba, mapendekezo yote tutayafanyia kazi kwa lengo la kuboresha.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)