Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ismani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia uzima na afya njema. Pili, nitumie fursa hii kutoa pongezi na shukrani zetu za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Jasson Samson Rweikiza, Mwenyekiti wa Kamati hii na Mheshimiwa Ramadhan Suleiman Ramadhan, Makamu Mwenyekiti, Wajumbe wote wa Kamati hii na Sekretarieti kwa kuratibu vizuri sana zoezi hili la Kamati hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati hii ni muhimu sana na ni nyenzo muhimu ya Bunge letu Tukufu katika kufuatilia utekelezaji wa madaraka ya kutunga Sheria Ndogo yanayokabidhiwa kwa mamlaka mbalimbali Serikalini kama ambavyo tumezisikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati hii ilifuatilia utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo 22 zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa 12 na 13 wa Bunge. Serikali tayari ilifanyia kazi taarifa kama ambazo nyingine tumezisikia kutoka kwa Mwanasheria Mkuu na Kamati yenyewe, Sheria Ndogo 19 kama ilivyopongezwa na Kamati, Sheria Ndogo tatu zilizobaki zipo katika hatua za mwisho ambapo kwa sasa zipo katika hatua za uhakiki. Maelezo ya uhakiki na hatua za Kamati kwa Sheria hizi tatu tumeyasikia hivi punde kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na nyingine tumeambiwa inakwenda kutangazwa leo. Narudia kuwapongeza sana Kamati kwa usimamizi mzuri kabisa ambao umesababisha kuondoa kero kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyobainisha Mwenyekiti wa Kamati, wamechambua Sheria Ndogo Ndogo 179 zilizowasilishwa kwenye Mkutano wa Bunge wa Kumi na Nne na Sheria 163 zilizowasilishwa kwenye Mkutano wa Kumi na Tano wa Bunge. Kazi ya uchambuzi wa sheria hizo imekuwa ikifanywa na Kamati hii kwa weledi mkubwa bila kuchoka kwa sababu inafahamu kuwa inatenda yote hayo kwa manufaa ya wananchi, hasa wale wananchi maskini wa vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda niwakumbushe tu Waheshimiwa Wabunge, kazi inayofanywa na Kamati hii kwa kweli inafanya kazi nzuri sana hasa kwa niaba ya Wabunge wote kwa sababu na sisi tumechaguliwa na wananchi ili kulinda haki na heshima yao. Pia, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, siku zote amekuwa anajipambanua kwamba hapendi kabisa wananchi wanyanyaswe au wakose huduma au kusumbuliwa, kubughudhiwa kwa namna nyingine yoyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya sheria hizi tumezisikia ni kweli zinaleta usumbufu na taharuki kwa wananchi. Hapa mwisho tumemsikia Mheshimiwa Mbunge juu ya wapara samaki wa Mtwara. Ninaamini kule hata kama wanazitumia, wataacha leo, maana sheria kama hizi zinaleta bughudha na maudhi kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani wenzetu wengi wale wanaotunga tunga sheria kama hizi, kama wanasikia basi wajifunze kazi njema inayofanywa na Kamati na wajue hii Kamati haijalala. Sheria zote ambazo zitakuwa zinaleta usumbufu, kero kwa wananchi, zitafutwa na hii Kamati na Bunge hili linaridhia kazi ya hii Kamati. Kwa hiyo, Sheria kama hizi zinaleta usumbufu, kwa hiyo, tumsaidie Mheshimiwa Rais ili akiyasema na wenzetu kule wanaoanza kutunga hizi sheria, wamsikie na waache kabisa kutunga hizi sheria ambazo zinaleta taharuki kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, sisi kama Ofisi ya Waziri Mkuu tutafuatilia na kusimamia wahusika wote kuzingatia maagizo ya Bunge lako Tukufu. Aidha, tayari tumetoa maelekezo kwa mamlaka zote kwamba, katika uandishi wa Sheria zao Ndogo, ni lazima wamshirikishe Mwanasheria Mkuu. Pia, Mwanasheria Mkuu amefika juzi na nafurahi kwamba Wabunge wengi wamempongeza kutokana na utulivu wake na umakini aliouonesha kwa muda mfupi huu uliopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kwa kuwa tuko hapa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mmemsikia akisema kwa nia njema, basi wanasheria walio chini yake huko kwenye Halmashauri wazingatie nia njema ya Mwanasheria ambaye ndiye kiongozi wao ili sheria zinazokuja kuanzia sasa ziakisi nia njema ya huyu bosi wao. Vilevile, mjue yuko makini sana. Kwa hiyo, najua Sheria kama hizo hazitakuja tena kwenye Kamati.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kumshukuru sana tena Mwenyekiti na Mwanasheria Mkuu kwa ufafanuzi, lakini nakuhakikishia kwamba, tunafurahi kazi hii, tunasema sasa Serikali inafanya vizuri, hivyo tunafurahi sana na kwamba TAMISEMI ambao wana mlundikano wa sheria hizi ndogo nao sasa wanafanya kazi vizuri. Sisi tutaendelea kuwabana ili kuhakikisha kwamba, zisiwepo kabisa sheria zinazokuja kutangazwa ambazo zina maudhui yanayokwenda kunyanyasa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa nirudie taarifa njema aliyoisema mdogo wangu David Kihenzile ya kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano huko China alipo, kwa kazi kubwa aliyoifanya leo na taarifa hii tumeisikia kutoka kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi Mheshimiwa David Kihenzile juu ya kusaini huu mkataba wa TAZARA. Hii ni kazi njema iliyotukuka ambayo kwa kweli Watanzania wote tunapaswa kumpongeza kutokana na mwanzo mzuri wa ziara hii ya kimapinduzi. Tumekuwa na reli hii ambayo imekuwa inasuasua kwa muda mrefu, lakini leo kwa kusaini mkataba ule inakwenda kutuondoshea shida, kupunguza na kuongeza mapato ya wananchi kutokana na usafirishaji utakaoboreshwa kutokana na reli hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa hii ni muhimu sana na nzuri sana kwetu kuisikia hivi leo. Baada ya maelezo haya nakuhakikishia kwamba, Serikali hailali na itahakikisha kwamba, jambo hili linaratibiwa lakini sheria ndogo ndogo zote zitakazokuwa zinatangazwa, zitatangazwa kwa namna ambayo zinakidhi malengo na matarajio ya wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)