Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TAMIMA HAJI ABASS: Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua nafasi hii kutoa mchango wangu kwa njia ya maandishi katika Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2024/2025 iliyowasilishwa mbele ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Spika, naishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa inayochukua katika kuleta maendeleo kwa wananchi wake.
Mheshimiwa Spika, pia nampongeza Waziri wa Mipango na Uwekezaji kwa kuja na mpango wa maendeleo pamoja na Waziri wa Fedha kwa kuwasilisha bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025, bajeti ambayo ni nzuri na mkombozi wa mwananchi.
Mheshimiwa Spika, pamoja na uzuri wa bajeti hiyo haitakuwa na thamani yoyote iwapo utekelezaji wake hautapewa umuhimu kwa maana ya watendaji ambao ndio watekelezaji wafanye kazi kwa bidii kuhakikisha wanakamilisha kazi walizopangiwa.
Mheshimiwa Spika, vilevile Wizara ya Fedha ina wajibu wa kuzipatia fedha walioomba Wizara za Kisekta ili waweze kukamilisha shughuli walizozipanga, iwapo Wizara hazikupatiwa fedha zote na kwa wakati ni wazi kwamba malengo hayatoweza kufanikiwa.
Mheshimiwa Spika, naendelea na mchango wangu kwenye eneo la kuchangia pato la Serikali na nazungumzia eneo la mazingira. Serikali ijenge viwanda vikubwa vya kuchakata taka na kuzalisha mbolea ambayo tutatumia nchini pia tutauza nje na kupata fedha za kigeni.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tunazalisha taka nyingi ambazo zimekuwa kero kwa kuchafua mazingira na kusababisha maradhi ya mllipuko, tukumbuke kuwa kila kiumbe nchini kinazalisha taka, hivyo changamoto hiyo tuigeuze kuwa fursa.
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu; kwanza, kupitia halmashauri zetu uwekwe mkakati maalumu wa kukusanya taka kwenye masoko yote; pili, kuwa na mkakati maalumu wa kukusanya taka majumbani; tatu, kuwa na mkakati maalumu wa kusafisha mitaro ya maji machafu; nne, kuwa na utaratibu maalumu wa kusafisha fukwe; tano, kitengo cha kukusanya taka kwenye halmashauri zetu kiimarishwe kwa kupatiwa vifaa vya kisasa na sita, wawepo wakaguzi wa kila siku kukagua usafi wa masoko. Hii itasaidia maeneo yetu kuwa safi, pia kupata malighafi ya kutengeneza mbolea.
Mheshimiwa Spika, baada ya hayo, naunga mkono hoja.