Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Prof. Adolf Faustine Mkenda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rombo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa fursa hii na mimi nasimama hapa kuunga mkono hoja na napenda kukumbusha tu wakati Waziri wa Fedha anasoma hotuba yake alitumia maneno yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, alizungumza kwamba a politician looks at the next election but a state person looks at the next generation. Alizungumza hivyo kwa kusisitiza kwamba Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kuwekeza na kuweka kipaumbele sana kwenye elimu siyo tu katika suala la miundombinu, lakini katika kubadilisha mfumo, mitaala na sera ya elimu, jambo ambalo matunda yake hayataonekana mapema sana, anafanya hivyo kwa sababu amekusudia siyo kuangalia tu uchaguzi ujao, amefanya hivyo kwa sababu anataka kuangalia vizazi na vizazi vijavyo vya watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hayo tunaweza tukayaona kwanza katika miundombinu halafu nitaelezea kidogo kuhusu mikopo ya wanafunzi suala ambalo limezungumzwa sana humu na utekelezaji wa mitaala mipya.

Mheshimiwa Spika, katika miundombinu ni vizuri tu nikakumbusha Waheshimiwa Wabunge kwamba chini ya uongozi wa Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Elimu ya Juu kwa mara ya kwanza kabisa katika nchi yetu sasa hivi tunaenda kujenga kampasi za Vyuo Vikuu katika Mikoa yote ambayo ilikuwa haina kampasi ya Vyuo Vikuu ukiacha Chuo Kikuu Huria. Tutamaliza Mikoa yote isipokuwa tu Mkoa wa Pwani ambao mkakati wake tunaenda kuuweka. Kwa hiyo, Mkoa kama Kigoma sasa hivi, Tabora, Kagera, Lindi, Tanga, Ruvuma na kadhalika kazi ya ujenzi inaendelea kwa sababu ya maelekezo ya Rais wetu, Wizara ya Fedha na Tume ya Mipango kwa kweli wanatusaidia kulisukuma jambo hilo mbele.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo ni kubwa vilevile ni lile suala la ujenzi wa vyuo vyetu vya VETA. Niwakumbushe tena Waheshimiwa Wabunge hasa wenyewe kwa mchango wao kwamba Serikali imeamua na ni utekelezaji wa maelezo ya Rais wetu kwamba sasa hivi katika kila Wilaya ambayo VETA imejengwa lakini Wilaya hiyo ni kubwa kiasi kwamba ina Majimbo zaidi ya moja la uchaguzi, kama VETA imeenda kwa Mbunge mmoja, huyu Mbunge mwingine anajengewa shule ya sekondari ya ufundi.

Mheshimiwa Spika, shule ya sekondari ya ufundi siyo tu mafunzo ya amali, maana yake mafunzo ya amali kuna mambo ya utalii, kuna kilimo na kadhalika, hizi ni technical secondary school kama tulivyokuwa tunajua Tanga Tech, Ifunda Tech, Bwiru Tech, Moshi Tech na hizi zitajengwa na zitakuwa zinatumia teknolojia ambayo ni modern zaidi.

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema Mheshimiwa Mchengerwa wakati anawasilisha bajeti yake zinajengwa shule 100 mpya, shule 26 tunakusudia zianze kuchukua wanafunzi ifikapo Januari kwa ajili ya kuleta mapinduzi ya elimu yetu katika maeneo hayo. Kwa hiyo, kila Mheshimiwa Mbunge sasa hivi atakuwa na cha kusema kama hana VETA, atakuwa na sekondari ya ufundi ili aweze kwenda kuisemea Serikali yetu kwa kazi nzuri ambayo inafanywa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Spika, sasa nataka nielezee kidogo kuhusu mikopo. Kwa kweli, Waheshimiwa Wabunge wengi sana wamezungumzia kuhusu mikopo ya elimu ya juu, najua kuna masuala kwamba kuna watu wameomba mikopo wanaonekana hawajapata lakini ni vizuri kwanza tujue tulitoka wapi, tuko wapi, halafu tutapata matumaini tunakwenda wapi.

Mheshimiwa Spika, wakati Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anachukua uongozi wa nchi, mikopo ya elimu ya juu ilikuwa ni shilingi bilioni 464 na nyongeza ilikuwa ikienda taratibu sana tangu tuanze mikopo ya elimu ya juu. Alipoapa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kati ya vitu vya kwanza alivyosisitiza ni kuuliza ajue mikopo ya elimu ya juu ikoje akaagiza iongezwe, iliongezwa kwa mkupuo kutoka shilingi bilioni 464 kwenda bilioni 570 kwa mwaka wake wa kwanza ofisini. Mwaka uliofuata tumefika bilioni 654, mwaka uliofuata bilioni 731. Sasa hivi tuna bilioni 787, tunakaribia shilingi trilioni moja kwenye mikopo ya elimu ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini nasema hayo? Nasema hayo kwa sababu hata pamoja na changamoto ambazo bado zinakuwepo katika mikopo ni vizuri tujue na wanafunzi wajue kwamba nyongeza iliyofanyika kwenye mikopo ya elimu ya juu ni kubwa kuliko kipindi kingine chochote tangu tuanze kutoa mikopo ya elimu ya juu. Zaidi ya hapo mapendekezo ya Waheshimiwa Wabunge yalikubaliwa na Rais wetu na hivyo Hazina ilitenga hela na tumeanza kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaosoma Diploma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mara ya kwanza sasa hivi katika fani kadhaa tunatoa mikopo kwa wanafunzi ambao wanasoma Diploma. Kazi yetu kubwa ni kuendelea kuboresha namna ya kugawa mikopo hii kwa haki, wapate wale ambao wana mahitaji makubwa zaidi wakati ambapo tunaendelea kupambana namna ya kuongeza fedha kwa ajili ya kutoa mikopo hiyo. Hili ni vizuri tuliseme ili wakati tunapoona changamoto tusije tukasahau kwamba kwa kweli tunaenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, zaidi ya hivyo napenda kuwaambia wanafunzi wote wanaosoma, wanaonisikia kwamba Serikali sasa hivi iliongeza, Rais wetu alikutana na uongozi wa wanafunzi iliongeza fedha za kujikimu kwa siku kwa wanafunzi wote kwa mkupuo.

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho najua kengele imepigwa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Muda wako umeishaisha Mheshimiwa.

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba dakika moja.

SPIKA: Mheshimiwa unachukua dakika za wenzio, sekunde thelathini malizia.

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kuhusu utekelezaji wa mitaala, bajeti ipo muda wangu hautoshi na mkumbuke mitaala inatekelezwa kwa awamu, Elimu ya Awali, Darasa la Kwanza la Tatu na Sekondari Kidato cha Kwanza Mafunzo ya Amali. Fedha zimetengwa za vitabu na walimu wote wa viwango hivyo wameishapata mafunzo namna ya kutekeleza mitaala mipya na tunazo fedha kwa ajili ya kuendelea darasa la pili, darasa la nne la tano la sita mpaka tutakapo kamilisha mwaka 2027 tutakapoanza sasa kwenda elimu ya miaka 10 ya lazima.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa fursa hii, narudia tena kusema naunga mkono hoja. (Makofi)