Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Ignas Aloyce Malocha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kukushukuru kwa kunipa nafasi, lakini pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuingia tena kwa mara ya pili katika mjengo huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana Wananchi wa Jimbo la Kwela kwa kuniwezesha, kwa kuniamini kunirudisha tena ili niweze kuwatumikia na wananchi hao walisimama kidete sana japo kuwa kulikuwa na mizengwe mingi sana lakini wananchi waliweza kusimama na hatimaye kuniwezesha kurudi katika ukumbi huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Magufuli, kwa kasi hii aliyoianza ya kusimamia wananchi. Ni kasi ya hali ya juu na mimi nawapongeza wale ambao wanatambua kwamba kasi ile ndiyo iliyokuwa inahitajika katika nchi hii kwa sasa. Nawapongeza na Mawaziri wote ambao wametambua hivyo na wameanza na kasi hiyo, ninachowaomba Mawaziri wote mtambue kwamba mna watu wenu mpaka huko chini waimarisheni, wabadilisheni kifikra ili waendane na kasi hii ya Mheshimiwa Magufuli. (Makofi)
Kwa sababu Mheshimiwa Magufuli hawezi kufanya kazi peke yake bila sisi wote kujibadili kufanana na yeye, atachoka lazima tumsaidie na kumsaidia ni kuweka mtandao wa kasi kuanzia ngazi ya juu mpaka kule chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu katika kuchangia Mpango wa Maendeleo 2015/2016. Sisi tunatambua kwamba mpango huu wa maendeleo umelenga katika kukuza uchumi, katika kuhakikisha wananchi wanaondokana na umaskini, katika kukuza pato la Taifa. Hata hivyo, nataka nichangie kwa upande wa kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua sisi wote kwamba nchi yetu sehemu kubwa ya wananchi wanategemea kilimo na katika kilimo, nataka nizungumzie jambo moja, lazima tujiridhishe hivi Watanzania wote waliopo mijini na vijijini wote wana ardhi ya kutosha kuwaendeleza? Hilo ni la kwanza kujiuliza, na mimi nasema baadhi ya maeneo yanawezekana yanatosha lakini maeneo mengi bado ni tatizo. Ni tatizo kwa sababu tumeachia watu wachache wameatamia maeneo makubwa, Serikali inazungumza kila siku haichukui hatua. Sijaona ni kwa sababu gani Serikali inachelea kuchukua uamuzi wa haraka, hii haitaji hata kusubiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mara nyingi nimekuwa nikisimama hapa nikitetea wananchi wa Jimbo la Kwela kuhusu shamba la Malonje nimelizungumza kadha wa kadha hatimaye hata kwenye uchaguzi imeniletea mpambano mkubwa sana lakini Mwenyezi Mungu akisimama hakuna ubishi ndiyo maana niko leo hapa. Wananchi wa Jimbo la Kwela nitaendelea kuwatetea lazima shamba hilo lirudishwe mikononi mwa wananchi. Namwomba Mheshimiwa Waziri kwa sababu wewe Mwenyewe umefika mara ya mwisho ukasema mimi nitakuwa mtu wa mwisho kuzungumzia suala la ardhi hii ya shamba hili la Malonje naomba utimize ahadi yako wananchi wale warejeshewe lile shamba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine katika upande wa ardhi na mimi nataka niishauri Serikali. Serikali ni kweli ilitenga Mapori ya Akiba. Unaposema mapori ya akiba lazima uende na pande zote mbili, mapori ya akiba aidha kwa wanyama lakini mapori ya akiba kwa binadamu, tusiende upande mmoja. Wakati mapori yale yametengwa baadhi ya wananchi walikuwa hawajaongezeka lakini sasa hivi watu wameongezeka. Unaita pori la akiba lakini wananchi wananyanyasika hawana kwa kulima, pori hilo halina mnyama hata mmoja hata ndege mmoja, Jamani huu ni ubinadamu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia Pori la Uwanda Game Reserve. Linatesa wananchi isivyo kawaida na halina faida yoyote kwa Serikali na nashukuru Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii nimeongea na wewe, nimekusimulia kwa kirefu sana na nikakuomba ufike, inawezekana maneno haya ninayozungumza usiyaamini, basi ufike ukaone.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanakatiza mle kwenye lile pori la akiba, wananyang‟anywa majembe, wananyang‟anywa panga zao, wananyang‟anywa fyekeo, pikipiki, wanapigwa wana nyanyasika, wakati pori lenyewe halina mnyama hata mmoja. Jamani tumefika wapi hapo? Haya mambo mengine ni ya kuchukua hatua za haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili uamini, maana mara nyingine mnachukulia sisi kama ni wanasiasa uende, namwomba Waziri wa Maliasili afike eneo lile. Hata hivyo, nikupongeze kwa sababu nilipokueleza ulitoa amri ya wananchi kurejeshewa vifaa vile walivyokuwa wamenyang‟anywa, nakupongeza katika hilo na naomba uendelee katika kutatua tatizo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni umeme, tunatambua kabisa maendeleo hayawezi kuja bila umeme, lakini nitoe masikitiko kidogo katika Jimbo langu au Wilaya yangu ya Sumbawanga Vijinini, pamoja na Wilaya hii kuwa ya siku nyingi, pamoja na jitihada zote za Serikali, Jimbo langu halina umeme hata kijiji kimoja. Vijiji 114, Kata 27, watu zaidi ya 450,000, halina hata kijiji kimoja chenye umeme.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Wakati mwingine Serikali inaweza ikatutambua sisi viongozi, tunaotokana na Chama cha Mapinduzi kama vile tunaipinga Serikali hapana, ni masikitiko ya kuona wananchi wanahangaika, hivi Serikali hii inaendeshwa kwa upendeleo?
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua Muhongo ni mchapakazi na nimeongea na wewe ninataka kwa kweli wananchi hawa wapate umeme, awamu ya kwanza ulisema utatoka Sumbawanga- Laela, ni nguzo tu zimelala, awamu ya pili ni Ukanda wa Ziwa Rukwa, kwa hiyo naishauri Serikali iweze kuhimiza kwa haraka ili wananchi hawa waweze kupata umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kulizungumzia ni kupunguza ukubwa wa maeneo ya Utawala, nazungumzia Jimbo langu la Kwela ni Jimbo kubwa na lina watu zaidi ya 450,000 lina sifa zote za kugawanya na nilipozungumza hapa kwa mara ya mwisho na Waziri Mkuu Mstaafu ali-support, kwa sababu anafahamu. Hata Mheshimiwa Keissy juzi amezungumza, hata baadhi ya Wabunge ambao wamekwenda kule akina Paresso wanafahamu, Mheshimiwa Mbatia, Mheshimiwa Aeshi wanafahamu, ni Jimbo kubwa kuliko, wakati mwingine unasema nitafanyaje kazi katika Jimbo hili, ni kubwa ukienda upande huu wengine wanakusahau.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Naishauri Serikali na bahati nzuri uliyekuwa Mkuu wa Mkoa Mheshimiwa Manyanya uko hapa, naomba jambo hili tulivae wote, tuihabarishe Serikali inatuletea matatizo makubwa sana, Jimbo hili linatakiwa kugawanyika, kama tunatenda haki kwa sababu lina sifa zote. Yapo Majimbo yamegawanywa zaidi ya mara 3, hayana sifa zote. Lakini Jimbo langu limebaki pale pale.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mapendekezo tumeleta yote ya kuomba Jimbo, kuomba Wilaya, kuomba Halmashauri, hakuna hatua hata moja ambayo imechukuliwa, sasa jamani na hawa wananchi mnawaweka katika upande gani? Naishauri Serikali ijaribu kutenda haki kwa maeneo yote yenye matatizo kama haya, nimeona nilizungumzie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni miundombinu ya barabara, ninapozungumzia barabara nizungumzie barabara ya kutoka Kibaoni, kuja Kiliamatundu na kwa maana hiyo ukifika Kiliamatundu unatakiwa ukatishe uende Kamsamba, ukatokee Mloo. Ile barabara ina zaidi ya kilometa 200.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Serikali kwa sababu katika ilani mmeiweka katika kipaumbele cha kuifanyia usanifu. Hata hivyo, naomba isiwe usanifu ile barabara inatakiwa kutengenezwa kwa kiwango cha lami kwa sababu ina uchumi mkubwa sana. Hizi kilometa 200 ninazosema karibuni kila baada ya kilometa tano kuna kijiji cha wananchi wenye uzalishaji, ukitengeneza barabara hii utakuwa umeufungua ukanda ule kiuchumi, utaongeza pato kwa wananchi, utaongeza pato kwa Serikali. Kwa hiyo, naomba Serikali iweze kushughulikia barabara ile kwa kiwango cha lami, ikiwa ni pamoja na kutengeneza daraja la mto Momba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa miaka mitatu tunaambiwa upembuzi yakinifu tumechoka na maneno hayo, tunataka waanze kujenga. Ukijenga daraja hilo umeshawaunganisha wananchi na Wilaya ya Momba wanaotokea Mloo, uchumi utaenda kwa kasi kubwa sana. Kwa hiyo, naiomba Serikali iweze kuchukua jambo hili katika masuala ya utekelezaji, kwa sababu linaumiza sana na ni ukanda wenye uchumi mkubwa sana, uzalishaji wa mpunga, ufuta, uvuvi. Sasa tunapozungumzia kutengeneza barabara si tuangalie na vigezo, vigezo ni kuongeza uchumi wa wananchi na Taifa zima kwa ujumla siyo unapeleka barabara huna hata matumaini ya kurejesha uchumi wenyewe.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante.(Makofi)