Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mola ambaye kwa mara nyingine ametuwezesha kushiriki kwa pamoja katika Bunge hili, lakini sasa hivi tukiwa katika hatua za mwisho za kuhitimisha bajeti yetu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025. Naomba niwashukuru na niwapongeze Mawaziri wote wawili ndugu yangu Dkt. Mwigulu Nchemba pamoja na Profesa Mkumbo na Manaibu wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika mjadala hapa kubwa zaidi katika bajeti ya mwaka huu kwa upande wa ukusanyaji wa mapato ni hasa biashara ya kaboni.

Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu, kwamba mwaka 2022 Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais tulikuja na mwongozo na kanuni za biashara ya kaboni kwa sababu eneo hili lilikuwa halijatumika vizuri. Kipindi kile hali yetu haikuwa nzuri katika suala la usimamizi katika eneo hili. Leo hii naomba nikuhakikishie kwamba, Bunge lako hili na Serikali yako Tukufu, tumeshafikisha usajili wa miradi takribani 50 kwa mara ya kwanza ambapo hivi karibuni tumeshuhudia Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ambao hivi karibuni walipata bilioni 14 kutokana na mapato yatokanayo na biashara ya kaboni. Hii inatuonesha namna usimamizi katika eneo hili utakavyoweza kuleta manufaa makubwa sana katika nchi hii.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali imejipanga na tunakwenda vizuri. Mfano mzuri ni huu uliotokea hivi juzi kama nilivyosema, Halmashauri ya Tanganyika ambao makusanyo yao yalikuwa ni wastani wa shilingi bilioni mbili hadi bilioni tatu, leo hii kwa mara ya kwanza wamepata bilioni 14 ndani ya vijiji vyake. Hii ni faraja kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hivyo kama nilivyosema, tayari tumesajili mradi takribani 50. Kati ya miradi hiyo 26 ni sekta ya misitu na 14 ni sekta ya energy. Kwa hiyo hata katika suala la mpango wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan la kwenda katika nishati safi ya kupikia kupitia biashara ya kaboni, eneo hilo nalo tumeweza kulifanyia kazi kubwa zaidi. Hivi sasa tunashukuru kwamba kuna baadhi ya kampuni zimeanza hatua kubwa sana hasa katika suala la kupata majiko banifu na majiko mengine ambayo yatakuwa na gharama nafuu kwa lengo la wananchi kuingia katika biashara ya kaboni.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwamba ninawashukuru Mawaziri hawa wawili hasa kwa kuweka mipango mizuri ya jinsi nchi yetu inavyokwenda. Kupitia ofisi yetu kwa ushahidi wa kutosha kabisa katika hiki kipindi cha karibuni, tumeona; na nimshukuru sana Dkt. Nchemba na hasa katika mifumo hii tunayoweka na Waziri wetu wa Uwekezaji. Leo hii kupitia Taasisi yetu ya NEMC takribani miradi elfu tisa na sitini na moja imesajiliwa kupitia NEMC. Hiyo maana yake ni uwekezaji.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri subiri kidogo.

Mheshimiwa Waziri endelea.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kama nilivyosema awali, kwamba kwa sera nzuri za Dkt. Samia Suluhu Hassan leo hii tunaona kupitia ofisi zetu kwamba tumeweza kusajili baadhi ya miradi kupitia kituo chetu cha NEMC. Leo hii takribani miradi 9,061 imesajiliwa. Hii ni trend ya miaka mitatu, unaona jinsi gani sasa sera nzuri zinavyotusaidia hasa katika ujenzi wa uchumi wetu. Miradi hiyo ukiikokotoa kwa ujumla wake uwekezaji huo ni zaidi ya trilioni 37. Hii maana yake ni ile miradi iliyopita katikia ofisi yetu kupitia Taasisi yetu ya NEMC tu.
Mheshimiwa Spika, maana yake ni kwamba Watanzania tusijidharau, tunafanya vizuri katika mchakato mzuri wa uwekezaji wetu wa uchumi katika nchi yetu. Katika hili lazima tumpe kongole Dkt. Samia Suluhu Hassan. Anayoyafanya leo hii ndiyo yameweka misingi mizuri. Kama nilivyosema, kwamba uwekezaji huu ni zaidi ya trilioni 37.55, ambapo hii ni kwa trend zilizopitia kwenye uwekezaji katika kituo chetu cha NEMC ambao ni kwa ajili ya kupata vyeti vya tathmini ya athari ya kimazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaombe ndugu zangu, kama nilivyosema, kwamba tusijidharau Watanzania leo hii tunafanya vizuri. Hata kama kuna changmoto za hapa na pale lakini tunafanya vizuri. Kubwa zaidi tushikamane na hasa katika kushughulikia masuala ya mazingira, kwa sababu nchi yetu inapoteza Dola za Kimarekani takriban milioni 500 kwa mwaka kwa ajili ya kushughulikia miradi ya adaptation na mitigation kutokana na kushughulikia athari za mabadiliko ya tabianchi. Hili jambo ni kubwa, kwa hiyo Watanzania wote lazima tuweke kipaumbele cha jinsi ya kushirikiana kwa pamoja katika kuweka ajenda ya utunzaji wa mazingira na hasa suala zima la kutekeleza miradi yote, kama Serikali ilivyoamua sasa hivi kutekeleza miradi yake ya kushughulikia masuala ya mazingira.

Mheshimiwa Spika, tuishukuru sana Serikali yetu leo hii tunaona katika sekta ya maji kazi kubwa imefanyika ambapo takriban miradi ya maji 222 imesajiliwa na katika sekta ya ujenzi takribani miradi 1,894. Yote hii inajenga uchumi katika upande wa nchi yetu. Kikubwa zaidi, hasa katika sekta ya nishati, leo hii kuna miradi 1,340 ambayo sisi upande wa Ofisi ya Makamu wa Rais tunasema kwamba eneo hili tunaweka tija katika suala la upatikanaji wa nishati, ambapo kwa namna moja au nyingine ajenda ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inaenda kufikiwa. Kwa hiyo, kubwa zaidi niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuunga mkono bajeti hii ya Mwaka wa Fedha ya 2024/2025 kwa sababu kwa kiwango kikubwa imeakisi uhalisia, na hasa katika upande wetu wa mazingira.

Mheshimiwa Spika, kabla sijagongewa kengele, kwa sababu najua kwamba dakika zangu ni saba, ninaomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)