Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi, na nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, kwa sababu chini ya uongozi wake tumeendelea kuona namna ambavyo mazingira ya biashara na uwekezaji katika Taifa letu yameendelea kuimarika chini ya uongozi wake mahiri.

Mheshimiwa Spika, pia nikupongeze nawe kwa namna ambavyo unaendelea kuliongoza Bunge letu na kwa namna ambavyo unaendelea kutuwakilisha kimataifa.

Mheshimiwa Spika, niendelee kuwapongeza pia viongozi wengine wakuu. Mheshimiwa Makamu wa Rais, Rais wa Zanzibar pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu na Naibu Waziri Mkuu kwa namna ambavyo wanaendelea kutusimamia na kutupatia miongozo mbalimbali na hatimaye tunaweza kupata tija na ufanisi katika Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, sambamba na pongezi hizo niwapongeze sana Waheshimiwa Mawaziri Wawili, Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa namna ambavyo wanaendelea kusimamia na kuongoza katika masuala ya sera na utekelezaji katika sekta zao na kwa kuleta Mpango mzuri wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka 2024/2025 pamoja na bajeti yetu hii kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha ujao 2024/2025.

Mheshimiwa Spika, utaweza kuona namna ambavyo bajeti hii imeendelea kuakisi umuhimu wa kuendelea kukuza uchumi wetu na pia umuhimu wa mchango wa bajeti hii kupitia mkazo mbalimbali wa kisera na mazingira kwa upande wa kukuza ajira. Vile vile, unaona namna ambavyo imeweka mkazo pia katika suala la uwekezaji wa ndani na kuendelea kuongeza au kuvutia uwekezaji kutoka nje ya nchi. Kubwa zaidi, nikiwa ninasimamia sekta ya utalii tushukuru kuona kwamba, katika Mpango wa Maendeleo ya Taifa katika sekta chache zilizowekewa kipaumbele suala la sekta ya utalii nalo limeingizwa na tunashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, pia ukiangalia katika bajeti hii unaona namna ambavyo imelenga kuongeza zaidi ushiriki wa sekta binafsi katika shughuli za biashara na uwekezaji. Imeendelea pia kuweka mkazo wa matumizi ya Shilingi za Kitanzania katika malipo mbalimbali. Nipende tu kumhakikishia Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Waziri wa Nchi Mipango kwamba, kama Wizara ya Maliasili na Utalii tayari tumeshaanza marekebisho ya kanuni zetu ili kuhakikisha kwamba tunaakisi tozo zote na gharama zinazotozwa katika sekta zetu basi zinatozwa kwa Shilingi za Kitanzania. Kubwa zaidi tupongeze pia kwa namna ambavyo bajeti ijayo imeelekeza katika kukamilisha miradi ya maendeleo ya kimkakati, na tunaamini itaweza kumalizika ndani ya muda si mrefu.

Mheshimiwa Spika, nipende pia kujielekeza katika mafanikio ambayo tumeyaona kupitia uongozi imara wa Taifa letu na Wizara, na pia kupitia kinara wetu maalum Mheshimiwa Rais ambaye amekuwa kinara namba moja katika suala la kuhamasisha na kutunza utalii, kwa kweli tunampongeza sana Mheshimiwa Rais na tunaendelea kuwa nyuma yake.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia katika miaka miwili tangu amekuwa madarakani kwa upande wa kuvutia watalii kutoka nje ya nchi zaidi ya asilimia 96 wameongezeka; na ukiangalia mpaka Desemba, 2023 tuliweza kupata watalii wa nje takribani milioni 1.8. Kwa upande wa watalii wa ndani kiwango kiliongezeka hadi kufikia asilimia 152 na tuliweza kupata watalii milioni 1.9 hadi Desemba, 2023.

Mheshimiwa Spika, vile vile tumeweza kutambulika kimataifa. Kupitia Takwimu za Shirika la Utalii Duniani kwa mwaka 2023 tuliweza kushika nafasi ya 12 duniani kwa ongezeko la idadi ya watalii wa kimataifa kabla ya janga la UVIKO. Ukiangalia kwa miezi hii mitatu ya Januari mpaka Machi mwaka huu wa 2024 tumeweza kuweka rekodi kubwa ya kimataifa na kidunia. Tumeweza kushika nafasi za tano za juu duniani kwa nchi ambayo imeweza kuvutia watalii zaidi duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli pongezi nyingi zimfikie Mheshimiwa Rais, lakini na Watanzania wote kwa namna ambavyo pia wameendelea kushiriki kukuza utalii kwa kuhakikisha kunakuwa na uwepo wa amani.

Mheshimiwa Spika, vilevile ukiangalia kwa takwimu za Januari mpaka Machi, katika mapato yanayotokana na shughuli za utalii, duniani pia tumeweza kushika nafasi ya nne na nafasi ya kwanza Afrika. Lile suala zima la kuvutia watalii katika nafasi ya tano tumekuwa pia nafasi ya kwanza Afrika, pongezi sana kwa Watanzania wote, tuendelee kuwa wakarimu zaidi ili tuweze kuvutia watalii wengi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, kwa takwimu za Benki ya Dunia za mwezi Mei ...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: ... tumeweza kupata dola bilioni 5.75, niwapongeze tena kwa mara nyingine Watanzania na ninashukuru kwa kunipa nafasi na ninaunga mkono hoja. (Makofi)