Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rufiji
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema aliyetuwezesha kufika katika hatua hii tukiwa na afya njema.
Mheshimiwa Spika, kipekee pia nichukue fursa hii kukupongeza sana wewe, nimpongeze Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze Wenyeviti wa Bunge kwa kuendesha Bunge letu hili na kuishauri Serikali kwa namna ambavyo tumepokea kama Serikali ushauri, maoni na mazingatio ambayo sisi Ofisi ya Rais tutakwenda kufanya kazi ambavyo Wabunge wametushauri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lazima nikiri, Bunge hili limesheheni Wabunge wanaofanya kazi kubwa sana, lazima sisi kama Serikali tuwapongeze kwa kazi kubwa sana ambayo Waheshimiwa Wabunge wamefanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kila mmoja wetu hapa ni shahidi, kila Mbunge aliyesimama kwenye Bunge hili amezungumza yale ambayo yanawahusu wananchi wake katika maeneo yao na wananchi watakuwa ni mashahidi kwa namna ambavyo Wabunge wamegusa hoja zao na ni matamanio ya wananchi kusikia Wabunge wao wakizungumza mambo ambayo yanawahusu wao katika maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yapo mambo ambayo Waheshimiwa Wabunge wamesisitiza sana na sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI pamoja na kwamba tunaunga mkono hoja ambazo zimetolewa na Wabunge walio wengi katika maeneo ambayo wamezungumza. Ninaomba nikiri kwamba huu sasa ni mwaka wa tatu na nusu wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunakiri kabisa kwamba kazi kubwa sana imefanyika katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Spika, kila Mbunge hapa ni shahidi wa kazi kubwa ambayo imefanywa katika sekta ambayo Ofisi ya Rais, TAMISEMI inasimamia; sekta ya afya, sekta ya elimu na sekta ya miundombinu na yapo maeneo kutokana na mafuriko yaliyotokea tunakiri kabisa kwamba miundombinu mingi imeharibika, lakini si kwamba Serikali haikufanya kazi. Hii ndiyo sababu hata watendaji wetu wa TARURA wanapoingia hapa Bungeni wanapongezwa kwa kazi kubwa ambayo wameifanya ya kusimamia sekta ya miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kila Mbunge hapa, kila kiongozi katika Serikali za Mitaa, Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji katika maeneo yetu, kila mmoja ana sababu ya kusema yale ambayo Serikali imefanya katika kipindi hiki, Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, sisi ndani ya Ofis ya Rais, TAMISEMI tunatambua kazi kubwa iliyofanywa, ujenzi wa zahanati, ujenzi wa vituo vya afya, ujenzi wa hospitali, uboreshaji wa miundombinu kwenye sekta ya elimu na mambo mengi kadha wa kadha katika kila jimbo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hakika hatuna sababu hata kidogo ndani ya Bunge hili, kwa uwakilishi mzuri ambao Waheshimiwa Wabunge wameufanya kwa wananchi, kila Mbunge ana kila sababu ya kurejea hapa mwaka 2025 kwa sababu kazi kubwa imefanyika na sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI tutasisitiza sana kwa watendaji walio chini ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais ameridhia utoaji wa mikopo ya 10%, mikopo hii lazima wananchi watambue kwamba ni Wabunge hawa ambao wao wamekuwa wakiishauri Serikali kuhusu utolewaji wa mikopo hii. Mikopo hii inapokwenda kwa wananchi wetu kila jimbo, kila halmashauri, kila wilaya na kila mkoa, ni Wabunge hawa hawa ambao ndiyo wamewakumbuka wananchi na kusisitiza na kuishauri Serikali kuhusu namna bora ya utolewaji wa mikopo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hapa tumesimama, ninaomba tumpongeze na kumshukuru sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Rais wetu ameridhia utoaji wa mikopo, Rais wetu ameshauri namna bora ambayo yeye anatamani kuona kila Mtanzania katika kila jimbo akipatiwa mikopo ya 10%. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba nilitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba ifikapo tarehe 30 Juni, maandalizi ya kanuni za utolewaji wa mikopo yatakuwa yamekamilika, lakini pia ifikapo tarehe 10 Julai, wataalamu wa TAMISEMI watafika katika kila jimbo katika kutoa mafunzo na elimu ya utolewaji wa mikopo hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, dhamira ya Mheshimiwa Rais ni kuwa mikopo hii iende na ikamfikie kila Mtanzania katika kila jimbo, halmashauri na Mkoa wa Taifa letu hili. Mheshimiwa Rais ametamani na anatarajia kwenda kunyanyua uchumi wa kila Mtanzania, uchumi wa wanawake katika kila eneo la nchi hii, uchumi wa vijana katika kila eneo la nchi yetu hii, lakini pia uchumi wa Watanzania wenye mahitaji maalumu, wenye ulemavu kwa asilimia mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilitaarifu Bunge lako Tukufu, niwataarifu Watanzania kwamba fedha tunazo za kutosha za utolewaji wa mikopo katika eneo hili. Tuna bakaa zaidi ya shilingi bilioni 307 lakini katika makusanyo ya mwaka huu, matarajio yetu ni kwenda kutoa mikopo zaidi ya shilingi bilioni 101.5 na fedha hizi tunazo. Matarajio yetu baada ya mafunzo, michakato ya utolewaji wa mikopo kwa halmashauri kumi ambazo zimetengwa kwa utaratibu wa kupitia benki, halmashauri hizi ni Jiji la Dar es Salaam, Jiji la Dodoma, Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Kigoma Ujiji, Halmshauri ya Mbulu, Newala, Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, Nkasi pamoja na kule Bumbuli na Siha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, halmashauri 174 na zenyewe zitakwenda kupata mikopo kwa utaratibu ulioboreshwa zaidi. Dhamira ya Mheshimiwa Rais fedha hizi ziende kuwafikiwa Watanzania katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimalizie hili lingine la kuhusu vituo vya afya; Mheshimiwa Rais alituagiza kila jimbo la uchaguzi kupeleka vituo vya afya. Maana yake Mheshimiwa Rais alielekeza majimbo ya uchaguzi 214, kila Mheshimiwa Mbunge apelekewe kituo cha afya.
Mheshimiwa Spika, nilitaarifu Bunge lako Tukufu, maelekezo haya ni amri ya Mheshimiwa Rais mwenyewe ambayo ametuelekeza Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Wizara ya Fedha kuhakikisha kwamba vituo hivi vinajengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI tutaanza sasa wakati wenzetu wa Wizara ya Fedha, tunaendelea na mijadala. Tunategemea kuanza ujenzi wa vituo vya afya na tayari nilitaarifu Bunge lako Tukufu, tunazo zaidi ya shilingi bilioni 400 ambazo zitakwenda kujenga vituo vya afya ... (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, zitakwenda kujenga zahanati, zitakwenda hospitali za halmashauri zaidi ya 21 kujenga na kukarabati. (Makofi)
SPIKA: Haya, ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru, kwa nafuu ya muda ninaunga mkono hoja na ninawashukuru sana Watanzania, waendelee kuwa na imani na Serikali inayoongozwa na Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yako maeneo ambapo tunaona kuna hitilafu ya makusanyo ya ushuru wa mazao, tumekwishatoa miongozo na mimi mwenyewe na wasaidizi wangu tutafika huko kwenye halmashauri ambazo zina changamoto ya makusanyo ya ushuru wa mazao. Maelekezo yangu, Watanzania wasinyanyaswe kwenye maeneo hayo na kiongozi yeyote ambaye hatasikiliza maelekezo ya Mheshimiwa Rais, TAMISEMI hatutasita kuchukua hatua kwa kiongozi yeyote ambaye anawanyanyasa Watanzania katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)