Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwa hoja mbili ambazo zimewasilishwa na Waziri wa Fedha pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uwekezaji pamoja na Mipango. Nianze kwa kuwapongeza sana watoa hoja kwa wasilisho zuri, pia niwapongeze Waheshimiwa Naibu Mawaziri.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu, hoja nyingi zimechangiwa kuelekea kwenye Wizara ya Ujenzi na kwa sababu ni dakika saba, ninaomba niahidi kwamba Waheshimiwa Wabunge hoja zenu zote tutawasilisha kwa maandishi.

Mheshimiwa Spika, nitatumia dakika saba hizi kuzungumzia baadhi ya changamoto ambazo mojawapo ni changamoto ya madeni kwa makandarasi na kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu atakapokuwa anahitimisha, ninaamini suala la madeni kwa makandarasi ataweza kuliezea vizuri.

Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto ya madeni, Serikali inaendelea kuweka jitihada kubwa ya kuweka fursa kwa wakandarasi wetu hususani wakandarasi wazawa. Ukiangalia takwimu kwa miaka 11, kuanzia mwaka 2012 hadi 2023, kilometa ambazo zimejengwa na wakandarasi wazawa ni jumla ya kilometa 102 kwa miaka 11, lakini bajeti ambayo tunaenda kutekeleza kuanzia mwezi ujao Julai, Wizara na kwa maelekezo ya mpendwa wetu Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, baada ya kuangalia takwimu kwa kazi ambazo zinaenda kwenye sekta ya ujenzi, 96% wanapata wakandarasi wazawa, lakini wanachukua 40% ya keki ya fedha ambazo zinaenda kwenye sekta ya ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, takwimu hizi hazikumpendeza Mheshimiwa Rais, akaelekeza Wizara ya Ujenzi tuje na mkakati. Mkakati tumeuandaa, local content strategy tumeikamilisha na kwa mwaka wa fedha 2024/2025 tumetenga kilometa 120 mahususi kwa ajili ya wakandarasi wazawa. Katika hizo, zipo kilometa 20 ni mahususi kwa ajili ya wakandarasi wazawa wanawake na tutawatengea vipande vidogo vidogo ili waweze kukidhi matakwa ya kujenga kilometa hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunatumia nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa maono yake, kwa sababu tunaona kwenye miaka 11 kilometa 102 tu ndiyo ziliweza kujengwa na wakandarasi wazawa, lakini kwenye mwaka huu wa fedha ambao tunaenda kutekeleza, kilometa 120 ndani ya mwaka mmoja zimetengwa mahususi kwa ajili ya wakandarasi wazawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na fursa hizi nilizozitaja kilometa 120, nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha na hapa kwenye Bunge mwaka jana Bajeti Kuu kama hii kulikuwa kuna hoja ya Waheshimiwa Wabunge kwamba thamani ya miradi kwa wakandarasi wazawa ni shilingi bilioni 10 peke yake. Ninamshukuru Waziri wa Fedha, kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, amesharekebisha kanuni, sasa hivi thamani ya miradi kwa wakandarasi wazawa ni shilingi bilioni 50, imepanda kutoka shilingi bilioni 10 kwenda kwenye shilingi bilioni 50. Baada tu ya bajeti hii tutakaa mimi na kaka yangu Mheshimiwa Waziri wa Fedha na PPRA ili tuweze kujipanga kuhakikisha kanuni hii inaanza kutekelezwa ipasavyo kwenye mwaka wa fedha 2024/2025. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, tunaendelea na mazungumzo na wafadhili wa maendeleo African Development Bank. World Bank tumeshakaa nao, tunataka miradi mikubwa ambayo tunatumia fedha zao, lakini ni fedha zetu kwa sababu ni mikopo na mikopo hii inalipwa na sisi wenyewe Watanzania. Tumewaomba World Bank, African Development Bank pamoja na wafadhili wengine wa maendeleo, barabara na madaraja ambayo tunayajenga kuwe na kipengele cha ku-subcontract kwa ajili ya wakandarasi wazawa ili kuendelea kutengeneza fursa na mkakati huu utasaidia hata kuokoa fedha za kigeni tunapokopa fedha kwa ajili ya kujenga barabara na madaraja, basi kwa kiasi kikubwa fedha hizo zibaki ili ziweze kusaidia kujenga uchumi wa nchi yetu, kwa hiyo, hili tunaenda kulisimamia pia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaendelea kusimamia suala la fedha za Mfuko wa Barabara 100% kuendelea kutekelezwa na wakandarasi wazawa. Sambamba na hilo, kwenye masharti ya tender tumefanya marekebisho, miradi yote ya TANROADS kuanzia mwezi Julai kwenye upande wa manunuzi tumefanya maboresho kwenye masharti ya zabuni yaliyokuwa yanawakwamisha wakandarasi wazawa bila sababu za msingi. Sasa hivi kuanzia Julai nimeelekeza Wizara ya Ujenzi na taasisi yetu ya TANROADS, tutapunguza kiwango cha mapato ghafi (average turnover) ili kuweza kuwapa unafuu wakandarasi wazawa. Tutaruhusu kutumiwa kwa tender au bid-securing declaration badala ya tender ama bid-security. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutaruhusu kutumia performance bonds au performance securing declaration badala ya performance bank guarantee. Vilevile kwenye upande wa wakandarasi wote wazawa, mimi na kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu tulikaa nao mwezi Novemba na tukakubaliana kwamba mkakati huu kwa bajeti hii ambayo tunakuja kuandaa ya kuanza mwezi Julai, tutaanza kutekeleza haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ningependa kuwaondoa wasiwasi Waheshimiwa Wabunge kwa sababu kuna michango kwamba pamoja na fursa hizi za kuendelea kuchelewa kulipa wakandarasi wazawa, pia kunawakwamisha kwa sababu wanapata kazi, lakini malipo yanachelewa.

Mheshimiwa Spika, mimi na Mheshimiwa Waziri wa Fedha tumekaa na benki zetu nchini na kuangalia namna ambavyo Serikali itashirikiana na benki hizi kupunguza risk portfolio ya mikopo ambayo inaenda kwa wakandarasi wazawa. Jambo hili tutalisimamia, kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu yuko hapa, tutakaa na benki ili tuweze kukubaliana namna ambavyo wakandarasi wanaweza wakaanza kazi, wakapata advance payment, lakini pale Serikali ambapo inachelewa kuwalipa, basi benki zetu ziweze kuwarahisishia malipo kwa kutumia security ya mikataba ambayo tunaingia nao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)