Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Ummy Ally Mwalimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii, lakini na mimi nakupongeza kwa kazi kubwa na nzuri ambayo unaifanya katika kuliongoza vyema Bunge letu na unaliheshimisha sana. Pili, nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mheshimiwa Waziri wa Mipango kwa kuleta hoja nzuri. Kipekee, sisi Sekta ya Afya Bajeti ya 2024/2025 imebeba dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za afya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kubwa ambalo tunajivunia katika bajeti hii ni Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakilalamika kila siku kuhusu Sera ya Matibabu Bila Malipo kwa Akinamama Wajawazito na Watoto Wenye Umri Chini ya Miaka Mitano. Bajeti hii kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, Serikali imekuja na chanzo mahususi cha kugharamia huduma za afya, kwa ajili ya akinamama wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Huyu ndiye Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatafsiri kwa vitendo Sera ya Afya ya Mwaka 2007, kwa mara ya kwanza kuna chanzo mahususi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunakupongeza sana wewe na Bunge lako pia, kwa kupitisha Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote. Bunge la 12 linakwenda kukumbukwa na Watanzania kwa kupitisha Mfuko wa Kuhudumia Bima ya Afya kwa Wasio na Uwezo na katika bajeti hii ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha tuna chanzo mahususi, hatutafika asilimia 100, lakini tunapo pakuanzia. Historia itakukumbuka Mheshimiwa Spika, Watanzania watakukumbuka, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia ataendelea kukumbukwa na Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja zipo nyingi za Waheshimiwa Wabunge ikiwemo na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Bajeti. Naomba nijikite katika mambo makubwa matatu; kwanza, tunawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa maoni na ushauri wenu. Jambo la kwanza, Waheshimiwa Wabunge wamezungumza, ikiwemo Kamati ya Kudumu ya Bajeti, suala la Serikali kuiwezesha MSD, kuipatia mtaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili nalo tumeliona katika bajeti hii kwamba, Serikali imetoa mtaji kwa MSD, shilingi bilioni 100, ambapo utaiwezesha MSD kutekeleza majukumu yake. Nimepata heshima ya kuwa Waziri wa Afya, huu ni mwaka wangu wa nane, hakuna siku Serikali ilitoa mtaji mkubwa kwa MSD, tulichopata ilikuwa ni shilingi bilioni 16. Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia, ametoa kwa mkupuo shilingi bilioni 100 na kuzipeleka MSD, ili kuweza kuimarisha utendaji kazi wa MSD. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na Waheshimiwa Wabunge tunaona mabadiliko mazuri kwa upande wa MSD. Tukiangalia mapato ya MSD sasa hivi, 2021/2022 kwa mwaka ilikuwa ni shilingi bilioni 336, Mwaka 2023/2024 yamepanda mpaka shilingi bilioni 530, maana yake ni kazi nzuri inafanyika ndani ya MSD. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili ni, badala ya MSD kusambaza dawa mara nne kwa mwaka kwa sababu, ya kuwezeshwa na Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, dawa zinasambazwa mara sita kwa mwaka. Kwa hiyo, kama dawa hakuna ni changamoto yetu sisi watendaji katika ngazi ya hospitali na vituo vya kutoa huduma za afya. Natumia Bunge lako Tukufu kuwataka Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuandaa makisio sahihi ya mahitaji ya dawa, kwa ajili ya maeneo yao kwa sababu, dawa sasa zinakwenda kila baada ya miezi miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, ni kwamba, tumeanza kama MSD kuongeza kununua dawa zinazozalishwa ndani ya nchi yetu. Mwaka 2021/2022 tulitumia shilingi bilioni 14 kununua dawa zinazotengenzwa ndani, tumeongeza mpaka shilingi bilioni 39.77 kwa hiyo, unaiona dhamira ya dhati ya Serikali kuwaunga mkono wawekezaji wa ndani wanaozalisha dawa na vifaa tiba, ili tuweze pia, kuongeza ajira na kukuza uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili ambalo Kamati ya Bajeti imelisema pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengi ni suala la uhaba au changamoto ya watumishi wa afya katika vituo vya kutoa huduma ya afya vya Serikali. Tunakubaliana na Waheshimiwa Wabunge kwamba, kweli tunayo hii changamoto, nilikuwa naangalia mkeka wangu, tumefanya uchambuzi.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)