Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufika siku hii ya leo tukiwa wazima na wenye afya. Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwako kwa kuweza kunipatia nafasi ya kuweza kuchangia bajeti hii na ninasema tu kwamba, naunga mkono hoja iliyo mbele yetu hapa. Vilevile naomba nitumie nafasi hii kupongeza Wizara hizi mbili, Wizara ya Fedha na Wizara ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa kazi nzuri ambayo wameifanya na wasilisho zuri ambalo lipo mbele yetu hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kuchangia eneo la kikokotoo, ambalo limejadiliwa humu ndani na Waheshimiwa Wabunge wengi, lakini limekuwa pia, likijadiliwa na wabunge humu ndani katika vikao mbalimbali vya Bunge. Bajeti hii ambayo tunaenda kuipitisha ni bajeti ambayo inaonesha ni namna gani Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anaguswa na maisha ya wafanyakazi wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tangu aingie madarakani Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tumeona mwaka wake wa kwanza tu katika uongozi wake alipandisha madaraja yaliyokuwa yamekwama miaka mingi. Kuna Watumishi wa Umma waliokuwa hawajapandishwa madaraja kwa zaidi ya miaka tisa, aliwapandisha zaidi ya watumishi 222,000 katika mwaka wake wa kwanza wa utumishi. Mheshimiwa Rais, vilevile aliguswa sana na madeni ya arrears kwa Watumishi wa Umma na alitoa fedha kwa ajili ya kulipa madeni hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hili ambalo nataka nilizungumzie, la kikokotoo, nalo linaonesha ni namna gani Mheshimiwa Rais wetu anawajali wafanyakazi wa Taifa lake. Julai, 2022 kuna mabadiliko ya kikokotoo yalifanyika ambapo wale ambao ni Watumishi wa Umma walilipwa kwa mkupuo wa asilimia 50 na kushuka kwenda asilimia 33 na wale waliyokuwa asilimia 25 walipanda kwenda asilimia 33. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ilikuwa ni kilio kwa watumishi wengi ambao mishahara yao ni ya chini na mara nyingine husubiria mkupuo wa fedha hizi, kwa ajili ya kuanza maisha yao pale wanapokuwa wamestaafu. Mheshimiwa Rais wetu, kama alivyosikia kilio cha madaraja, kama ambavyo alisikia kilio cha madeni ya watumishi, Mheshimiwa Rais, alielekeza kikokotoo hiki kiweze kuangaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naishukuru na kuipongeza Wizara ya Fedha, Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri na timu nzima ya Wizara ya Fedha. Baada ya kukaa nao waliangalia ni namna gani bora tunaweza kupunguza kilio hiki na kuweka katika bajeti hii tunayoenda kuipitisha shilingi bilioni 155, kwa ajili ya kulipa kikokotoo, kunyanyua kutoka asilimia 33 kwa wale waliokuwa asilimia 50 kabla ya Julai 22 kwenda asilimia 40 na wale ambao walikuwa asilimia 25 vile vile hawakuachwa, mpaka Julai 22 nao wamepandishiwa kwenda asilimia 35. Hii inaonesha ni namna gani Serikali hii ya Awamu ya Sita inajali watumishi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumesikia Waheshimiwa Wabunge wengi mmezungumzia suala la kuangalia kiwango hiki kiendelee kunyanyuka kurejea pale kilipokuwa, asilimia 50. Tumesikia utatu huu wa vyama vya wafanyakazi na waajiri; vyama vya wafanyakazi vimezungumzia namna ambavyo wanashukuru asilimia hii 40, lakini nakuomba asilimia iweze kurudi asilimia 50 lakini huu ni mwanzo mzuri, kilio hiki kimesikika na ndiyo maana asilimia saba hii imewekwa. Kadiri tunavyokwenda na kutengemaa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii inavyokuwa inaendelea, ile actual evaluation itakavyofanyika. Serikali itazidi kuangalia ni namna gani inarudi katika asilimia 50, lakini mwanzo huu ni mzuri.

Mheshimiwa Spika, niwatoe mashaka Waheshimiwa Wabunge, hawa wanaokwenda kulipwa siyo tu wale ambao wanastaafu kuanzia Julai mosi mwaka huu 2024, wanaenda kulipwa wote hata wale waliostaafu kuanzia Julai Mwaka 2022. Katika bajeti hii inayoenda kupitishwa watumishi waliostaafu kuanzia Julai 22 mpaka Juni. Hivi tunavyozungumza 2024 jumla ya 17,068 wanaenda kulipwa mapunjo yao, yale ya asilimia saba ambayo walistahili kupata na wale ambao walikuwa wanapata asilimia 33 kwenda asilimia 35 watalipwa mapunjo yao ya asilimia mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunatarajia kuona wengi wakija kudai mapunjo ya mafao yao. Tutaendelea kukiangalia kikokotoo hiKi kadiri actual evaluation itakavyofanyika kwenye mifuko yetu ya hifadhi ya jamii. Ninawahakikishia Serikali hii ni Sikivu na itaendelea kuliangalia na kuona ni namna gani bora tunazidi kusogea katika kiwango kinachozidi zaidi ya hapa asilimia 40.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja tena. Ahsante sana kwa nafasi hii. (Makofi)