Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Mimi kwa mara nyingine ninasimama tena kwa mara ya kwanza kuchangia katika hotuba hii ya bajeti pamoja na Wizara ya Mipango na Uwekezaji. Basi naendelea kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu kwa kunipatia nafasi hii, ili niweze kushirikiana na wenzangu katika kuhakikisha kwamba, tunalipeleka gurudumu la Taifa letu mbele na tulipeleke kwa kasi ambayo inahitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniamini na kunipa tena nafasi kufanya kazi na Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, ambaye kwa kweli, ni Profesa ambaye ni mtu mwema, muadilifu na kwa kweli, nilifurahi sana kusikia kwamba, nakwenda kufanya kazi chini yake kwa sababu namfahamu. Nimefanya naye kazi katika Kamati iliyokuwa ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, ni mtu mwema, ni mwalimu mzuri na hakika nitajifunza mambo mengi kupitia kwake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naendelea kuwashukuru wapiga kura wangu kwa sababu, wameniwezesha kuwa hapa. Naendelea kushukuru, nachukua fursa hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa kweli, nimesikiliza michango mingi ambayo imechangiwa na Wabunge katika kuboresha mpango huu au katika kutoa maoni yao katika Wizara hii ya Mipango na Uwekezaji. Kwa kweli, tumeweza kuchuma maoni mengi na tumeweza kupata mambo mengi mbalimbali ambayo yanakwenda kuboresha katika kuhakikisha kwamba, tunaweka mipango mizuri katika kuleta maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wabunge Wengi sana wamechangia na mambo mengi Mheshimiwa Waziri wangu atayaeleza, lakini kwa kifupi kuna Mbunge, kwa mfano Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere. Ameweza kutoa maoni yake na kwa kweli, tumeweza kuyachukua ikiwa ni pamoja na kuomba kwamba, Serikali kupitia Wizara hii ya Mipango na Uwekezaji tuje na mipango mizuri ya kuhakikisha kwamba, mipango hii ya maendeleo inakuwa sawa kwa Mikoa yote bila kubagua Mkoa wowote.

Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua fursa hii kumueleza Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, ina mipango mizuri kwa Mikoa yote. Mikoa yote inajaliwa kwa namna sawa, lakini mipango hii inatekelezwa kwa uimara mkubwa zaidi, kwa maana ya kuangali fursa zilizopo katika Mikoa hiyo, pamoja na kuhakikisha miundombinu na mahitaji mengine yote ambayo yanapewa vipaumbele katika Mikoa hiyo, basi yanafikiwa. Hii yote inategemea sana vipaumbele vya Mikoa husika ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine Mheshimiwa Mwambe, ametoa mchango wake mzuri sana ambao kwa kweli, tumeupokea. Moja ya hoja aliyoitoa Mheshimiwa Geoffrey Mwambe ni, ametaka kwamba, Serikali iangalie namna ya kupitisha mapendekezo ya bajeti na mipango katika jumuiya za wachumi, ili kupata michango zaidi kabla hatujaingia kwenye bajeti.

Mheshimiwa Spika, ushauri huu ni mzuri sana na kwa kweli, tumekwishaanza kufanya hivyo. Tunawashirikisha sana wachumi waweze kutoa maoni yao kuelekea katika mpango wa mwaka au kuelekea katika mpango wa kuandaa bajeti na hili limeanza kutekelezwa kama ilivyo kwa mujibu wa kanuni. Mipango hii inaanza kutekelezwa kuanzia katika ngazi ya Kata kwa maana ya WDC kwenda ngazi za Wilaya, Mikoa na mpaka kufika katika ngazi za Wizara hadi katika mpango wa Wizara, kwa maana ya mpango mzima kwa nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, huu mchakato ni shirikishi ambao unaanzia chini kabisa. Tunaendelea kuwasisitiza Wananchi, Waheshimiwa Wabunge na Madiwani kuhakikisha kwamba, katika uandaaji wa mipango hii wawe wanashiriki, ili waweze kutoa vipaumbele, basi mipango hiyo iweze kuingia katika bajeti na baada ya hapo iweze kutekelezwa kwa maana ya kupelekwa mipango hiyo, ili kwenda kufanya kazi za maendeleo.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rweikiza naye ameweza kutoa hoja mojawapo. Ametaka Serikali, kupitia TIC, kuandaa miradi na andiko kuweza kuwasaidia wawekezaji wa ndani, ili kutekeleza miradi mikubwa kwa pamoja, mfano uzalishaji wa mataili ya pikipiki.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa miradi mikubwa sasa hivi inashirikisha wadau ambao ni Watanzania kuhakikisha kwamba, tunawekeza katika miradi mbalimbali, ili tuweze kupata fedha na kuweza kufanya biashara. Kwa mfano tu mzuri, ukiangalia Mwaka 2022 na 2023 miradi iliyosajiliwa, ya TIC, tuliona kabisa hesabu zinaonesha theluthi moja ya miradi yote iliyosajiliwa ni ya Watanzania na theluthi mbili ni miradi ambayo ipo chini ya ubia, kwa maana ya Watanzania wameshiriki katika miradi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miradi ambayo imesajiliwa na TIC ni 526 tofauti na ilivyokuwa Mwaka 2022 ambapo,ilikuwa ni miradi 293 tu. Miradi ya Watanzania pekee Mwaka 2022 ilikuwa ni 99, lakini mpaka kufikia 2023 ilikuwa ni 159. Kwa miradi ya ubia ilikuwa ni 130 Mwaka 2003 ukilinganisha na miradi 82 tu Mwaka 2002 na miradi ya wageni pekeyake ilikuwa ni miradi 214 kwa Mwaka 2023 na miradi 112 ambayo ilikuwa imesajiliwa Mwaka 2022. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naendelea kwa kumalizia kusema kwamba, maoni pamoja na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge, sisi kama Wizara ya Mipango, tumechukua. Sasahivi tunaandaa Mpango wa Mwaka 2050, tunaomba sana kupitia Tume ya Mipango, Waheshimiwa Wabunge tushirikiane na Watanzania wote, ili tuweze kuandaa mpango mzuri wa Mwaka 2050, ili tuweze kuleta maendeleo katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda basi nakushukuru na mimi naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)