Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kojani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa fursa hii. Awali ya yote na mimi naungana na wenzangu, namshukuru Mwenyezi Mungu, Rahim, ambaye ametuwezesha kukutana hapa katika kikao hiki na hatimaye kuhitimisha Bajeti hii Kuu ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, naomba kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye ni mbeba maono ya Watanzania. Mheshimiwa Rais kwa uwezo wake mkubwa sana, ubingwa na ukinara wa kutafsiri sera kutoka kwenye makaratasi na kuwa kwa vitendo. Mara kadhaa tumekuwa na ndoto, sisi Watanzania, ya kuwa na miradi mikubwa kama SGR na mengineyo, lakini tumekuwa na ndoto ya kupeleka wanafunzi kwa mkupuo mmoja tu, siyo kwa awamu ya kwanza, ya pili na ya tatu, hilo limekamilika. Hii ni kwa sababu ya uwezo mkubwa sana wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kutafsiri sera kwa vitendo, lakini nimezoea kusema kwamba, sifa moja ya Mama aliyokuwanayo ni uwezo mkubwa sana wa kutafsiri chozi la watoto wetu au watoto wenu kwa vitendo kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni watu wachache sana, sisi wakina baba sawa lakini uwezo huu mkubwa sana mnao ninyi wakina mama, mnajua kwamba sasa hivi kilio hiki mtoto anahitaji nini? Mnajua mtoto kilio hiki nini kinamsumbua. Kwa hiyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, naomba nikushukuru sana wewe kwa malezi yako. Wewe umekuwa mlezi mzuri kwetu na ninavyokuambia hivi sasa hivi Wana-Kojani wanaku-miss sana. Siku umewatembelea wanatamani mara nyingine itokee utembelee Kojani kule. Wewe ni mlezi mzuri na tunashukuru kwa malezi yako. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, kwa kweli michango yenu ni mizuri sana na ushauri wenu ni mkubwa na tumeupokea kwa mikono miwili. Hii ni kwa sababu huko nyuma wapo walionena aah! Kwamba Bunge hili la siku hizi lakini hili Bunge la Kumi na Mbili ndiyo ambalo limetoa Rais wa Mabara yote ulimwenguni. Rais wa ulimwengu ametoka ndani ya Bunge la Kumi na Mbili. Kwa hiyo, tuna kila sababu ya kujivuna Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze na kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, yeye ni mentor kwangu na ni mwalimu mzuri kwangu. Kwa hiyo, nasema kwamba huyu ni bingwa na ni miongoni mwa Mawaziri bingwa ambao wanatufunza na kutuelekeza vizuri. Mheshimiwa Waziri nikuambie tu mengine ambayo yanatokea katika jamii, ndiyo ulimwengu na ndiyo maisha. Maana yake hata washairi wameandika na wanasema kwamba;
“Wamaani nakupa neno siwate,
Ya waneni sikiapo sitete,
Duniani mtu hapendwi na wote.” (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niendelee pia kwa kuwashukuru sana Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara ya Fedha, pamoja na Wizara zote za Serikali kwa kweli wanatusaidia vizuri na wanaisaidia Serikali yao kwa juhudi kubwa sana na uzalendo mkubwa sana. Kutokana na muda lakini pia nisisahau kumshukuru care taker wangu hapa Mheshimiwa Profesa Mkumbo, yeye alikuwa anafundisha vyuoni lakini hata hapa sisi wengine tunajifunza kutoka kwake. Tunakushukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Rais, pia kwa kutuongezea company hapa na wewe kuturuhusu kuwa na company. Mwaka jana na mwaka juzi tulikuwa wawili tu hapa lakini leo tuna company hapa unaona naongea kidogo. Tunakushukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba hasa nijielekeze moja kwa moja kwa hoja chache ambazo nimechagua kuzielezea kwa sababu hoja ni nyingi lakini nyingi zilikuwa ni ushauri na nilithibitishie Bunge lako Tukufu kwamba hoja ambazo wametoa, ushauri ambao wametoa tumeuzingatia na tumeubeba kwa meno ya magego kabisa na tunaenda kuufanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, upo ushauri Kamati ya Bajeti wameshauri kwamba Serikali ihakikishe mikopo ambayo inakopwa na Serikali inaelekezwa katika sekta za uzalishaji pamoja na miundombinu. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba mikopo yote ambayo imekopwa na Serikali imekuwa ikielekezwa kwenye miradi ya maendeleo hususani kwenye miundombinu ya barabara, maji, reli na umeme, kwa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya 2025. Kwa hiyo, niwahakikishie kwamba mikopo yote ambayo itaendelea kukopwa na Serikali itaelekezwa kwenye sekta za uzalishaji ama miundombinu mbalimbali ya barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali ilishauriwa kulipa madeni ya wazabuni wa dawa, kwa kipindi cha Julai, 2023 hadi Mei, 2024 Serikali imeshalipa jumla ya shilingi bilioni 256 kwa ajili ya kulipa madai ya wazabuni waliosambaza dawa na vifaa tiba. Aidha, mwaka ujao wa fedha Serikali imetenga shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kulipa wazabuni ambao wamesambaza dawa na vifaa tiba.
Mheshimiwa Spika, nimeona hapo imeshaanza kuwaka lakini naomba nimalizie hili. Niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba ule ushauri ambao umetoka na Wabunge basi ushauri huo umechukuliwa na Serikali. Mwisho kabisa, yupo mchangiaji mmoja Mheshimiwa Mbunge alisema kwamba kikokotoo hiki ambacho mmeongeza asilimia saba hadi kufika 40% mmefanya jambo lakini isionekane kwamba mmefanya jambo kubwa.
Mheshimiwa Spika, mimi nikuambie nyongeza hii ya asilimia saba ni kitu kikubwa sana kutoka 33% hadi 40% ni kikubwa sana. Hata ingekuwa asilimia moja tu basi ingekuwa ni hatua kubwa sana, kwa sababu wahenga wanasema; “Jicho hutaraji haja kila namna na penye moja na moja si moja tena.” Kwa hiyo, hata ingekuwa moja tu ingekuwa inatosha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie kwa kusema kwamba wafanyakazi walio wengi wameshukuru sana na Waheshimiwa Wabunge wapo ambao wametoa shukurani kuhusu jambo hili na ndiyo ulimwengu. Nimalizie kwa kusema kwamba wahenga wanasema; “Asiyeshukuru kwa yai basi na jogoo hachinjiwi.” Ahsante. (Makofi)