Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa fursa hii. Nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kuwa na afya njema tunapofikia hatua hii.

Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 13 Juni mwaka 2024 niliwasilisha katika Bunge lako Tukufu Mapendekezo ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2024/2025.

Mheshimiwa Spika, napenda kukushukuru wewe mwenyewe moja kwa moja, Naibu wako pamoja na Wenyeviti wa Bunge kwa kuruhusu mijadala kufanyika kwa weledi na kwa demokrasia ya kiwango cha juu. Tunakushukuru sana. Pia tunakushukuru sana kwa jinsi ambavyo unatulea tukiwa hapa Dodoma. Kuna wakati hoja za Waheshimiwa Wabunge zinakuwa za moto sana lakini umekuwa na ratiba ambazo zinatufanya Waheshimiwa Wabunge, tuendelee kuwa wamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata juzi uliandaa tamasha ambapo kupitia kwenye tamasha hilo niliweza kulipa kisasi kwa Babu Taletale ambaye alikuwa akinishinda mazoezini. Nilimshinda kwenye mita 100 kwa kumpita kama amesimama na hiyo imesababisha nipokee ofa nyingi sana za usajili. Basi hoja zote hizo zipelekwenye kwa meneja wangu wa usajili ambaye ni Ahmed Ally, Msemaji wa Simba. Babu Tale ameomba shindano lirudiwe, mimi niko tayari. Tunakushukuru sana kwa malezi hayo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutambua kazi kubwa inayofanywa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini, wakishirikiana pakubwa na Makamu Mwenyekiti ndugu yangu Twaha Mpembenwe pamoja na Kamati nzima ya Bunge ya Bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, tumepokea hoja za Waheshimiwa Wabunge wote, tunawashukuru sana kwa hoja nzuri sana ambazo mmetuletea; na kwa ajili ya ubora wa hoja hizo zilizotolewa nitakuomba nitoe ufafanuzi kwa utulivu mkubwa sana.

Mheshimiwa Spika, kwa dhati ya moyo wangu, napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru watendaji wa Wizara ya Fedha, tukianza na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha ambaye ananisaidia kwa ukaribu sana, Mheshimiwa Hamad Hassan Chande, Mbunge, Naibu Waziri wa viwango vya Wizara ya Fedha na Viwango vya Kidunia. Nakushukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa ushirikiano mkubwa unaonipatia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pongezi ziende pia kwa timu ya wataalam wa Wizara ya Fedha. Hawa wamekuwa wakikesha ili kuhakikisha kwamba gurudumu hili la Wizara ya Fedha linakwenda chini ya uongozi wake, Mwalimu wangu Dkt. Natu El-maamry Mwamba pamoja na taasisi zote ambazo ziko chini ya Wizara ya Fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee nitoe pongezi na shukurani kwa viongozi wetu wakuu ambao wamekuwa wakitupatia miongozo hapa; Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu pamoja na Chief Whip. Kweli tumekuwa nao bega kwa bega, hata wizara za kisekta wanazisimamia kama sekta ambazo ziko moja kwa moja chini ya Sekta za Kiwizara. Ninawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kurejea pongezi zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Nilisema wakati nikiwasilisha taarifa hii, narejea kusema, “Mheshimiwa Rais ameonesha uwezo wa waziwazi na mpaka nchi zingine wanaona mambo makubwa ambayo Tanzania inafanya.Tumezunguka katika baadhi ya nchi nyingi lakini kote kule tumeona jinsi wanavyoichukulia Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi yetu inaheshimika kule duniani. Kote tunakokwenda, nchi yetu inaheshimika kule duniani. Si tu kwa kuheshimika kwa kuitaja historia, unaona hata panapokuwepo na mkusanyiko wa wakuu wa nchi wengi wengi, unaona jinsi ambavyo kila tukio linapotokea wanahitaji kusikia Mkuu wa Nchi wa Tanzania anasema kitu gani. Hili ni moja ya jambo ambalo linaitambulisha nchi yetu na linatwambia tunaye kiongozi bora. Mambo haya ambayo wanayaona ni haya haya ambayo tunayaona ndani ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kazi kubwa sana imefanyika; niliorodhesha kwa kilefu siku ile wakati natoa mjadala, na tutaendelea kuyarudia mambo haya ambayo yamefanyika.

Mheshimiwa Spika, moja ya jambo kubwa lingine alilonalo Mheshimiwa Rais wetu ni zile 4R ambazo alizianzisha. Hizo 4R si kila mtu amejaliwa kipaji cha aina hiyo cha kuwasikiliza wengine.

Mheshimiwa Spika, hata sisi ni viongozi tunaweza tukajipima kwenye hayo, huwa tunaweza kuwavumilia walio chini yetu kwa kiwango gani. Iwe jimboni au iwe kwenye familia, unaweza ukaona ni namna gani Mheshimiwa Rais ana kipaji kikubwa sana cha kuheshimu mawazo ya wengine na kushirikisha hoja zinazotoka kwa wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tukianza na hoja ambazo zimejitokeza, kuna baadhi ya hoja nitazifafanua leo na kuna baadhi ya hoja tumezipokea na mtaziona tutakapokuwa tunajadiliana sheria yenyewe, kwa sababu zingine ni za kisheria. Nadhani kesho, kwa mujibu wa ratiba, tunakwenda kutunga sheria na mtaziona baadhi ya hoja ambazo tumezipokea na zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge pamoja na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Bunge lako hili ni Bunge linalowakilisha wananchi wake vizuri sana, hongereni sana Waheshimiwa Wabunge; na mimi nawaombea kwa wajumbe wote wawatendee haki kwa sababu mmewatendea haki katika kusimamia hoja zinazowahusu Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna hoja moja ilitolewa inayohusina na suala la kutoza kodi kwenye masuala ya gesi. Tumepokea hoja hii na ninawaomba Waheshimiwa Wabunge watuvumilie. Wataalam wetu wanaendelea kukamilisha wakati tunaelekea kwenye kukukamilisha sheria ya kodi na bado tunamalizia. Hoja hii mmeisemea kwa nguvu kubwa sana, ninaomba nisitaje mmoja mmoja kwa sababu ya muda, Waheshimiwa Wabunge wengi sana mmeongelea jambo hili. Nawashukuru sana na tumepokea hoja hiyo kwa uzito unaostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja nyingi kubwa ambayo imeongelewa sana ilikuwa ni kuhusu adhabu ya milioni 15. Hoja hii kwanza ilinukuriwa vibaya; ilinukuriwa tofauti na lililokuwa limelengwa.

Mheshimiwa Spika, kilichokuwa kinalengwa kwenye sheria, na ninawaomba Waheshimiwa Wabunge wote tusikilizane kwenye hili halafu tuamue vile tunavyoweza kusonga nalo mbele. Kilichokuwa kinalegwa mwaka jana, kwenye sheria ya mwaka jana tulitengeneza adhabu ambayo ilikuwa iko kwa asilimia; tuliweka kwa asilimia na asilimia tuliyoweka tulisema kwenye kile kiwango kidogo zaidi ambacho asilimia 20 yake ni ndogo sana kiasi kwamba yule anayekosea anaweza asione kama ameadhibiwa na kama anastahili kuacha kosa hili, adhabu tuliweka asilimia 20 ya vocha ya invoice ile ambayo itakuwa ina makosa.

Tukasema popote pale ambapo 20% hii tunaiona ni ndogo sana tutaweka kiwango cha chini kisichopungua 1,500,000. Kwa maana hiyo kwenye zile transaction ndogo sana ambazo 20% yake ipo chini ya 1,500,000 tukasema tutachukua 1,500,000. Hivyo ndivyo sheria tulivyokuwa tumeiweka, na hapa katikati kwa ajili ya kuweka usawa tukasema tutakuwa tunatoza 20% ya kosa lililogundulika nalo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama ni kosa lipo kiasi kadhaa ambayo ipo juu ya 1,500,000 inachukuliwa 20% yake. Sasa tulilokosea ambalo hatukuliweka ndio tulilotaka kurekebisha sasa hivi, tukasema popote pale ikizidi 15,000,000 hiyo 20% tunai-cap igote hapo kwa sababu makosa yanakuwepo yaliyo makubwa zaidi yanasababisha adhabu hiyo inakuwa kubwa sana kwa kiwango cha kutokulipika, yaani kwa mfano chukulia mtu akikutwa na vocha ya bilioni mbili; 20% ya bilioni mbili ni milioni 400. Kwa hiyo, kule ambapo tuliiacha iende wazi tukasema tui-cap kwamba itaenda 20%, 20%, 20% lakini ikizidi fixed number ya 15,000,000 inayotokana na hii 20% basi isipande iishie hapo, hicho ndicho tulichokuwa tumeweka.

Mheshimiwa Spika, tuliweka hivyo kwa sababu ukiweka tu namba moja mathalani milioni kumi unakuwa umewaumiza sana wale walio wadogo. Kwa hiyo, hiyo ndiyo ilikuwa logic ya kuweka hiyo asilimia ambayo inapanda. Lengo la kuiwekea ukomo ilikuwa ni kwamba isije ikaenda sana kwenye maeneo ambapo vocha hiyo itakuwa kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo tumepokea hoja za Waheshimiwa Wabunge na Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni sikivu na juzi tumekaa na wafanyabiashara chini ya uongozi wa Mheshimiwa Waziri Mkuu na pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Chief Whip, Waheshimiwa Mawaziri, kaka yangu Mheshimiwa Profesa Kitila ndiyo alikuwa Mwenyekiti, tukajadiliana wakaunga mkono hiki tunachopendekeza kwa maana ya kuwekea ukomo usiende juu kwa sababu kwa kweli kuna mizigo mingine inayokuwa mikubwa sana inaleta madhara.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo wakasema tunavyoweka range kubwa hii inasababisha negotiation wakati wa utekelezaji wake unakuwa na ushawishi wa masuala ambayo siyo ya kimaadili na hicho ndicho ambacho wao na Waheshimiwa Wabunge kama wawakilishi wa wananchi wamekilalamikia sana. Pendekezo ambalo tutalileta bado tunakamilisha consultation, tunapendekeza ile 1,500,000 ibaki kama ilivyo na ile ya juu iishie milioni nne, hilo ndilo ambalo tunapanga tulifanye kama pendekezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi vitu ambavyo Waheshimiwa Wabunge wamevisemea vinavyokosa maadili kwenye upande wa makusanyo ni kweli ni vitu ambavyo si vitu vya kupuuza, tumepokea sisi ndani ya Wizara, lakini pia kama Wizara tumeendelea kuongea na vyombo vinavyohusika na kusimamia haya masuala ya maadili ili kuweza kuhakikisha tunakomesha masuala haya ya upotevu wa fedha wakati wa ukusanyaji.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna malalamiko ya aina hii ambayo yanajitokeza, mengine yanaanzia ngazi za vijiji, watu wanachukua POS, anakusanya, anaondoka na makusanyo, wengine tunagawana nusu kwa nusu, hivi kingine kinaenda Serikalini kingine kinapita njia hizo zingine, tumeyapokea hayo yote na tunayafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika hoja nyingine ambayo imejadiliwa kwa kiwango kikubwa ni suala la fedha kwenda kwenye mifuko hii ya maendeleo inayosimamia hizi shughuli za maendeleo TARURA, REA, Mfuko wa Maji, Mfuko wa Barabara na maeneo mengine kama hayo. Hoja hii tumeipokea na kama ambavyo tulikuwa tukiisema lililokuwa linajitokea ilikuwa inaathiriwa pale ambapo fedha ipo kwenye mifuko, lakini ipo kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali, tumeshalipokea hili na tumelifanyia kazi, katika mwaka wa fedha huo unaoanza fedha za mifuko hazitakuwa sehemu ya Mfuko Mkuu wa Serikali ili zisiathirike kutokana na hali ya kifedha ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutaziweka pembeni na tunapanga pia tufanye utaratibu huo huo kwenye fedha ambazo ni za wahisani na fedha zile ambazo utekelezaji wake wa miradi ndiyo unakaribisha fedha zaidi yaani zile za kupata fedha kutokana na unavyotumia maarufu kama P4R, kwa hiyo, hili jambo tutalifayia kazi na tumeshakubaliana.

Mheshimiwa Spika, kuhusu nyongeza ya fedha tutalisemea zaidi kwa sababu kwenye barabara tunaongeza fedha mfuko wa dharura ambao utaweza kutumika katika kutengeneza masuala haya ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, upande wa maji, tumekubaliana na wenzetu wa Wizara ya Kisekta, mwaka jana katika mwaka wa fedha uliopita Serikali ilinunua mitambo ya kuchimba visima pamoja na mabwawa na kupima maji. Mitambo hii sasa ipo kila mkoa, kila mkoa una mitambo yake, tulisema kuliko tuendelee kujaza fedha kwa kutekeleza miradi hii kwa kutangaza zabuni na kujengwa kwa utaratibu wa zabuni, tukasema pia mitambo hii ambayo Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imenunua mipya na yenyewe iweze kutumika kuweza kuchimba visima, mabwawa ili kuhakikisha kwamba fedha ile ambayo ilitumika inaleta mrejesho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge sisi sote tupo kwenye majimbo kule na utaratibu wa nchi yetu tunaujua, tusipoweka mkazo kwenye haya magari wananchi watakosa maji, magari yatakuwepo na magari haya yataota kutu. Kwa hiyo, nawaomba kule tunapokwenda mikoani kwetu tuhakikishe haya magari yanatumika, magari haya yatumike, Mheshimiwa Rais ameyaleta kwa ajili ya kuchimba visima. Haiwezekani halmashauri ikakosa mpaka 15,000,000 ya kuchimba kisima katika eneo ambalo wananchi wamekosa kabisa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hii tumeweka zaidi ya shilingi bilioni 41 kwenye ngazi ya Wizara kwa ajili ya kuchimba hivyo visima, lakini lazima pia halmashauri zetu ziwahurumie wananchi, tuunganishe nguvu na hiki ndicho ambacho tulikuwa tunasema, magari yapo yatumike, yachimbe visima ili kuweza kupunguza matatizo ya maji kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo liliongelewa ni suala la upungufu wa dola na matumizi ya dola, kwenye hili la upungufu wa dola tumesema ndani ya Serikali tumepitisha mkakati wa Serikali wa kuongeza upatikanaji wa dola ambao ndani yake sekta zote ambazo zinaweza kutuletea mapato zimejumuishwa katika mwaka wa fedha huu tunaoendelea nao. Hili ni jambo ambalo linatakiwa kuwa endelevu kwa sababu dola si sarafu ya nchi yetu, tunaipata dola kutokana na vitu tunavyouza nje, tunaipata dola kutokana na msaada, tunaipata dola kufuatana na mkopo na hasa hasa kwa nchi yoyote inayojali uendelevu tunatakiwa kuipata dola kutokana na mauzo yetu ya nje.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, huu ni mkakati tumeuweka, umepitishwa na Baraza la Mawaziri na unaanza kutekelezwa. Baadhi ya mambo ambayo yamefanyika ni pamoja na uwekezaji kwenye sekta za uzalishaji, huu ni makakati wa muda mrefu ambao utatusaidia tunapokwenda tuweze kupata dola. Hata hivyo tunapokwenda mahitaji makubwa ambayo yalikuwa yanafanyika kufuatana na utekelezaji wa miradi mikubwa yanakuwa yanaenda yakipungua. Mfano bwawa la umeme tumeshamaliza maana yake importation ya vile vifaa ambavyo vilikuwa vinajenga bwawa havitahitajika tena. Tunahamia katika baadhi ya miradi ya kimkakati ambayo inatumia importation ya bidhaa hiyo na yenyewe itaenda kutusaidia kutupa ahueni huko tunapokwenda.

Mheshimiwa Spika, kuhusu matumizi ya dola hapa nchini, tumeweka pendekezo hilo la kurekebisha sheria, natambua jambo hili liliwahi kufanyika mwaka 2007 nadhani Mama Zakia Meghji akiwa Waziri wa Fedha na limefanyika juzi mwaka 2017 wakati Mheshimiwa Makamu wa Rais akiwa Waziri wa Fedha na jambo hili limekuwa likitolewa maelekezo haya, lakini limekuwa likipata upungufu katika utekeleaji wake.

Mheshimiwa Spika, nimeelekeza tunapoanza kutekeleza hili mwaka wa fedha huu unapoanza tunatengeneza na kanuni zake tutaweka na adhabu zake kwa sababu sheria ipo inayosema shilingi ya Tanzania ndiyo fedha halali kwa malipo yoyote ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili ni jambo ambalo pia linatakiwa lilete heshima kwa nchi yetu, tuache kuifatilia dola inavyoenenda. Tunaposema tutumie dola, tutumie Tanzanian Shilling, tutumie fedha yetu ya Kitanzania, tunataka pia hata kunukuu bei zetu tuzinukuu kwa fedha ya Kitanzania, hatujasema tutumie fedha ya Kitanzania, lakini kwa kunukuu bei kwa kutumia dola. Haya ni mambo ambayo wenzetu wameyaweza ni sisi tu tunayaendekeza. Ukienda nchi za wenzetu tunapotembea kule hata hukutani, hamna sehemu ambayo unaweza ukakutana hata bei tu imetajwa kwa fedha ya kigeni, siyo hata mbali nenda Afrika Kusini hapa uone kama kuna eneo utalipia fedha ya kigeni. Nenda na maeneo mengine haukuti wanatumia fedha ya kigeni hata kunukuu bei. Twendeni tutaje bei kwa fedha ya Kitanzania, acheni dola itembee kivyake, hii ya kusema sasa dola ipo kiasi hiki, dola siyo fedha yetu achene itembee kivyake. Mbona tunaponukuu bei hatuulizi pura ya Botswana ipo kiasi gani ili tuweze kujua bei ya bidhaa hiyo ni kiasi gani, mbona hatuulizi rand ni kiasi gani, mbona hatuulizi euro ni kiasi gani. Acheni dola itembee kivyake, bei tuziweke kwa fedha ya Kitanzania. Wewe kama una shule ama una nyumba unatamani sana kupokea bei zake kwa dola nenda kajenge Marekani, mbona lipo wazi hili utapokea kwa dola na hamna mtu atakulalamikia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, twendeni bei za Tanzania ni sheria siyo Waziri wa Fedha anavyotaka ni sheria, the legal tender ni fedha halali ya malipo ya ndani ni shilingi ya Kitanzania tutaweka kanuni na tutaweka na adhabu. Tumeiweka hiyo na tutaweka na kanuni na tutaweka na adhabu, tutumie fedha yetu tunatengeneza pressure ya kuitaka dola kutafutwa na inasababisha tushindwe kupata vitu vya muhimu kwa sababu ya vitu ambavyo tungeweza kuvifanya kwa fedha yetu ya Kitanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mtu anayetafuta leseni ya usafirishaji wa ndani tunamwambia kalete dola ya nini, mwananchi wa kawaida akalete dola, akaitafute wapi dola hiyo, hivyo hivyo na maeneo mengine. Twendeni tuwape kazi wageni kuitafuta shilingi ya Kitanzania kuliko kuwapa Watanzania kazi ya kuitafuta dola ambayo siyo fedha yao. Hii hapa Serikali tumesema tutatoa miongozo ili kuweza kuhakikisha jambo hili linatekelezeka na hili ni jambo ambalo ni la kisheria na Sheria ya Benki Kuu ndiyo inavyotuelekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la cashless economy, Waheshimiwa Wabunge wameongea sana kuhusu masuala ya cashless economy, tunaendelea nalo, ni jambo la msingi sana na hili wenzetu wameshapiga hatua. Ukienda hata siyo mbali sana hata majirani zetu tu hapo, hata ukinunua muhindi anakwambia ulipe kwa utaratibu wa lipa namba, wanafanya hivyo. Ukipanda bajaji wanakwambia ulipe kwa utaratibu wa lipa namba wanafanya hivyo, jambo hili Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuwaambia hata wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, sisi ndani ya Serikali tutaongeza jitihada za kujenga mifumo, kazi hii inafanyika pakubwa kuhakikisha kwamba ulipaji hauna matatizo kwa kutumia mifumo, tukishamaliza ulipaji hauna tatizo then tutaenda kwenye utaratibu wa enforcement, lakini kwa sasa hivi tunatamani tutangulize kwanza elimu na kujenga mifumo ili tutakaposema nchi nzima tuhamie kwenye utaratibu huo tuwe tumemaliza jambo la mifumo na tuwe tumemaliza suala la kuelimishana. Hili ni jambo ambalo tunaungana na hoja za Wabunge na ni hoja za kisasa kabisa, hoja makini kabisa zinazostahili kuwafanya wapiga kura wenu wawachague tena. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo limeongelewa ni jambo la Deni la Taifa, moja, naomba niweke wazi mambo machache kwenye hili suala la Deni la Taifa. Tuliongea kuhusu deni lenyewe na nilielezea wakati wa kuhitimisha hoja. Mimi niweke wazi tu mambo machache; hili jambo la Deni la Taifa na wananchi walisikilize vizuri, moja hatutofautiani tu kuhusu figure, kuhusu jumla ya deni, lakini tunatofautiana kuhusu jambo la kwanza, kukopa kwenyewe hatujaelewana vizuri, hili jambo la kukopa, wengine wanadhani tunakopa wa sababu nchi yetu ni maskini, wengine wanadhani tunakopa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, wengine wanadhani ni Tanzania tu inayokopa.

Mheshimiwa Spika, moja hatukopi kwa sababu sisi ni maskini, tunakopa kwa sababu sisi ni matajiri. Maskini huwa hakopi, maskini hakopi kwa sababu hana cha kulipa, maskini haaminiki, hawezi kukopa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili jambo la umaskini ni subjective, ni jambo ambalo siyo objective, ni jambo ambalo tunaenda ngazi kwa ngazi. Yule aliye tajiri zaidi ndiyo mwenye deni kubwa zaidi duniani ipo hivyo, kwa hiyo, sasa hivi ukipanga ukubwa wa madeni anayeongoza ni yule mwenye uchumi mkubwa zaidi duniani na ndiyo mwenye deni kubwa zaidi duniani, hivyo ndivyo ilivyo. Kwa hiyo, zile nchi zote kumi zinazoongoza kwa uchumi duniani ndiyo yenye madeni makubwa duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukija hapa Afrika ukipanga uchumi kama tunavyopangana kuanzia nchi yenye uchumi mkubwa zaidi hapa Afrika ndiyo yenye deni kubwa zaidi hapa Afrika. Nchi ya mwisho kwa uchumi hapa Afrika ndiyo yenye deni dogo zaidi na zingine hazina hata deni ni kwa sababu gani ukopaji ni utekelezaji tu wa mradi kwamba unachukua fedha kubwa kwa mara moja utekeleze mradi halafu ulipe kutokana na kipato kile ambacho ungekitekeleza kwa mwezi mmoja mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata asiye mtumishi wa Serikali hawezi kukopa salary advance, ukiajiriwa ndiyo unaweza ukachukua salary advance, halafu unaanza kurudhisha kutokana na mshahara unaolipwa hii ipo hivyo. Kwa maana hiyo hili ambalo tunafanya kuliko ujenge reli kutoka Dar es Salaam mpaka Kigoma kwa makusanyo ya mwezi mmoja mmoja Watanzania tuelewane, ukichukua malipo ya mwezi mmoja mmoja ndiyo ukaanza kulipa mradi mkubwa kama wa reli maana yake utamuweka yule anayejenga mkandarasi kwa miaka 50 au 60. Unachukua fedha ya miaka 20 unaiweka unalipia ule mradi uanze kukurudishia malipo yake halafu wewe kwenye makusanyo yale uanze kulipia kile ulichokikopa.

Mheshimiwa Spika, hata mimi tu hapa deni langu ni dogo kuliko deni la bilionea Mheshimiwa Musukuma, Mheshimiwa Musukuma lazima atakuwa na deni kubwa kuliko mimi, hata hapa hivyo hivyo. Mheshimiwa Mbunge wa kawaida kawaida hivi ambaye hana biashara kubwa deni lake halilingani na Mheshimiwa Mbunge mwenye biashara kubwa, hivyo ndivyo ilivyo, yeye atakuwa amekopa salary advance, lakini atakuwa amekopa IFC, atakuwa amekopa mpaka mabenki ya nje ya nchi, hicho ndicho ambacho tunatofautiana kuanzia mwanzo, hatukopi kwa sababu tupo maskini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunakopa kwa sababu tunaaminika na tunakopa kwa sababu tunatekeleza miradi ya msingi ya kimaendeleo, hicho ndicho ambacho kinafanyika. Sheria moja ngumu sana iliyowekwa kwenye mambo ya mkopo ni ya nchi ya Tanzania ndiyo maana kwa Ukanda wa SADC na Ukanda wa EAC nchi moja ambayo deni lake limetajwa kwamba ni himilivu na linafuata masharti ni Tanzania na haya si maneno ya Serikali wala si maneno ya Waziri wa Fedha, ni wataalamu wanaochambua madeni wamesema Tanzania ndiyo nchi ambayo ipo na B1+ kwa nchi zote za EAC na za SADC. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Moody’s wamefanya mwaka jana, wamefanya na mwaka huu wamekuja na matokeo yale yale fitch ratings, wamefanya mwaka jana wamefanya na mwaka huu wamekuja na matokeo yale yale. Imetambulishwa duniani kote, ingekuwa taarifa ya NBS mngesema hii ni ya Serikali. Hawa ni wale magwiji wa kwenye eneo hili. Kwa hiyo, niliona niseme hili na taarifa hizi zinatuambia bado tupo vizuri.

Mheshimiwa Spika, kuna mchangiaji mmoja alisema mbona concessional loans zimeongezeka wakati commercial zimepungua?

Mheshimiwa Spika, concessional loans, hii ni mikopo yenye masharti nafuu. Hizi ndio unaona framework agreement ambazo tunazipata ni kwa sababu tu, nchi inaheshimika na hizi ni nafuu, riba yake ni chini ya asilimia mbili. Ni tofauti na kwenda kukopa mkopo wa kibiashara ambao riba yake ni asilimia kumi, kumi na mbili na kuendelea. Kwa maana hiyo, hii kuongezeka ni akili kubwa sana ambayo Rais wetu ameitumia kuhakikisha tunakopa mikopo yenye masharti yaliyopoa. Mtu yeyote anayekopa angetamani apate masharti yaliyopoa. Nchi nyingine hawawezi wakapata hata hiyo, lakini hizi ni PR, ni mahusiano makubwa ya nchi yetu na nchi nyingine ambayo Rais wetu ameyajenga na hili ni jambo ambalo linasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho. Niwaondolee hofu Watanzania, hakuna siku Mtanzania atagongewa nyumbani kwake na mkusanya madeni kwamba, unadaiwa hapa nchi yako ilikopa, hakuna siku hiyo. Haya ni matumizi ya Serikali yatakuwepo kwenye Bajeti za Serikali kwa sababu, hicho ndicho ambacho kinafanya nchi inakopa kwa kuangalia Bajeti za Serikali. Sasa wenzetu wanaenda huko wanaanza kumwambia mwanakijiji aliyeko kule, ninyi hapa mnadaiwa; labda wao ndio wanawadai ile michango, kwa ajili ya kuendesha vyama vyao vya siasa, lakini Deni la Taifa hakuna siku Mtanzania mmoja atakutwa nyumbani kwake kwamba, wewe unadaiwa, kwamba ataswagiwa mifugo yake au atachukuliwa mahindi yake. Utaratibu wa uendeshaji wa nchi hauko namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niliona niseme hilo na nimalizie kwamba, kwenye masuala ya deni hakuna siku tunakopa, kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Hii fedha yote inayokopwa inakwenda kwenye miradi ya maendeleo, miradi inayofungua uchumi wa Watanzania. Mathalani, zamani mtu alikuwa akitoka Mbeya kwenda Arusha inabidi apite Njombe, Iringa, Morogoro, Tanga ndio aende Arusha, lakini tukafungua njia ya kutoka Iringa kuja Dodoma na tukafungua njia ya kutoka Dodoma kwenda Manyara na tukafungua kwenda Arusha. Hata kama ule ni mkopo, lakini chachu tuliyoifanya kwenye uzalishaji kwa wananchi ni jambo kubwa kuliko kwenda kuchukua mkopo wa aina hiyo. Niliona niliseme na hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho kwenye kipengele hiki ni madeni ya wakandarasi na madeni ya wazabuni. Waheshimiwa Wabunge mmeliongea sana jambo hili. Serikali sikivu imesikia na jambo hili Mheshimiwa Rais ametukalisha mara kadhaa mimi pamoja na Mawaziri wa Kisekta, Mheshimiwa Bashungwa na Mheshimiwa Mchengerwa pamoja na Wizara nyingine za Kisekta, Maji pamoja na Umeme. Hili ni jambo ambalo tunaliandalia mpango mahususi, tutakwenda kuwalipa, hasa hao wakandarasi wa ndani na sio tu kwamba, sasa hivi ndio tunaanza, kiporo chake kilikuwa kikubwa sana. Kuna watu hata walishasahau kama kuna siku watalipwa fedha hii. Tumpongeze sana Mama yetu, akasema walipeni hawa wakandarasi, ili fedha hii iongezeke kwenye mzunguko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulianza na shilingi bilioni 200, mwaka ule uliopita tukaenda shilingi bilioni 400, mwaka huu tulikuwa na shilingi bilioni 600 na sasahivi tuna utaratibu ambao tunaupanga. Tutatoa taarifa yake kupitia kamati yako ya Kibunge ambayo inatusimamia na tutatoa taarifa tutakapokuja hapa. Tunaweka mpango mkakati mahususi, wakandarasi, wazabuni pamoja na watoa huduma wa ndani watapewa kipaumbele hicho, kama ambavyo Mheshimiwa Rais amekuwa akielekeza, watapata fedha hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, upande wa matumizi. Hoja zote ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge ambazo zinahusu kurekebisha finance bill, ni dhahiri zitaathiri mapato ambayo tulikuwa tumeyakadiria na Bajeti ya Serikali ya Wizara zote za Kisekta tulishaipitisha. Tumekaa na wataalam wangu tukakubaliana baadhi ya mambo ambayo yamepata baraka za Serikali. Tutakwenda kubana matumizi, ili kuweza kufidia fedha ambayo tumeshaipangia kwenye Wizara za Kisekta, kwa ajili ya kuhakikisha shughuli za maendeleo hazikwami.

Mheshimiwa Spika, moja; tulitenga fedha, kwa ajili ya kununua magari. Jambo hili la magari tuliliongelea hapa Bungeni na Bunge lilibariki jambo hili, linafanyiwa kazi kuweza kuhakikisha kwamba, halileti usumbufu kiutekelezaji, linaendelea kufanyiwa kazi kuhakikisha ndani ya Serikali ni wapi wafuate mfumo upi na ni wapi wafuate mfumo upi. Kwa mfano, ni dhahiri askari anayefanya doria huwezi kumwambia nenda kwa gari lako kwa hiyo, kwenye upande wa vyombo hii hoja ya watumishi kupata magari yao itakuwa iko kando, lakini tumeangalia hata wale ambao wako field. Kwa hiyo, jambo hili liko linafanyiwa kazi na wenzetu wa utumishi, Mkuu wa Utumishi na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, ili kuweza kupata utaratibu mzuri ambao utakuwa hauathiri shughuli za Serikali.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, tutakwenda kubana matumizi kwenye bajeti hii inayokuja. Nimemwelekeza Mlipaji Mkuu wa Serikali kwenye takribani shilingi bilioni 129 ambazo zilikuwa zimewekwa kwa ajili ya kununua magari akate zaidi ya fifty percent abakize shilingi bilioni 50 tu wapeleke kwenye maeneo ambayo yatakuwa na umuhimu sana, kwa ajili ya kufanya kazi hiyo. Hivyohivyo kulikuwepo na takribani shilingi bilioni 67 ambazo zilikuwa za matumizi ya matengenezo akate kwa asilimia hamsini na hivyohivyo kwenye upande wa mafuta akate kwa asilimia hamsini. Fedha hizi zitakwenda kwenye miradi ya maendeleo ambayo itaathirika na marekebisho ya Sheria ya Fedha ambayo tayari tulishaiweka kwenye makadirio, zitakwenda kwenye miradi ya barabara, zitakwenda kwenye miradi ya maji, zitakwenda kwenye miradi ya umeme pamoja na maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge, mmeongea kwa kiwango kikubwa sana kuhusu matumizi ya gesi na jambo hili ni rasilimali ambayo tunayo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimeelekeza kwenye fedha iliyokuwa imewekwa ya mafuta. Serikali ndio tunaenda kutoa mfano, tunaenda kuongoza kwa mfano kuhusu kutumia magari yanayotumia mafuta.

Mheshimiwa Spika, kuhusu upatikanaji wa vituo vya mafuta.

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri Serikali tunatumia mafuta, ndio matumizi ya gesi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu matumizi ya gesi kwenye magari kama mbadala wa mafuta.

Mheshimiwa Spika, Serikali tunaenda kuwa mfano. Bahati nzuri sana Serikali huwa tunatumia kituo chetu ambacho ni cha Serikali chini ya bohari, kule ambako huwa tunatumia Serikali. Kwenye fedha tulizotenga za mafuta tutakwenda tukate fedha za mafuta tujenge hivyo vituo, tujenge Kituo Dodoma. Kama makadirio gari likijaziwa Dodoma halifiki Dar es Salaam, basi kijengwe na hapo Dar es Salaam, kijengwe na Morogoro na tutaendelea hivyo kujenga na center nyingine kubwakubwa ambazo zitasaidia kuweza kuhakikisha kwamba, jambo hili linafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutakata fedha ambazo tulishaziweka kwenye mafuta, tutaweka huo mfano, lakini pia, kama wenzetu wa private sector wameweza kuweka hiyo dual kwamba una fursa ya mafuta na una fursa ya gesi katika kipindi cha transition, hiyo na yenyewe tutaifanya na bahati nzuri sana GPSA iko chini ya Wizara ya Fedha kwa hiyo, maelekezo haya nimeyatoa waanze hivyo. Watakata bajeti ya mafuta tuweke hicho kituo kuweza kuhakikisha kwamba, utaratibu huo unafanyika. Ni lazima tuanze, lazima tuwe na pakuanzia kwenye jambo hili na ninaamini tutaweza kupiga hatua.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine kwenye eneo hili ni fidia. Tumepokea hoja za Waheshimiwa Wabunge wote zinazohusiana na fidia, maeneo mengine yanahusisha uwekezaji, maeneo mengine yanahusisha maeneo ambayo yamechukuliwa na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama.

Mheshimiwa Spika, tumepokea na tumeweka bajeti yake. Tuna maeneo kama Nyatwali, limeongelewa sana kwa upande wa uwakilishi, Mbunge wetu wa kutoka Bunda pamoja na jirani yake, tumepokea eneo hili. Kuna eneo la Kipunguni, limeongelewa sana hili na tumeshafanya vikao sana mpaka ambavyo ame-chair Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mbunge wa Segerea ameliongea sana, Mheshimiwa Bonnah. Tumepokea hili na haya maeneo ya fidia tutaanza nayo.

Mheshimiwa Spika, tulitamani tuwe tumeshalipa Bunge hilihili na tulishatoa ahadi ya aina hiyo, lakini yalijitokeza, haya mambo ya mafuriko, ambayo tulilazamika kuyapa kipaumbele, hasa hasa ukiona maeneo ambako unakuta Mikoa miwili au mitatu inakuwa iko kisiwani, tulilazamika tuanze na hayo halafu tuendelee na haya ambayo tumeyaweka. Pia, nimeelekeza OC zitapunguzwa kwa asilimia 20, ili kuweza kuhakikisha kwamba, fedha hizo zinakwenda kwenye miradi ile ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, kuna hoja ambazo zilikuwa zinaendelea za upande wa wenzetu wafanyabiashara. Na mimi nawaomba ndugu zangu, sekta binafsi kwa ujumla, wakiwemo na wafanyabiashara ambao tumeongea mambo yao kwa kirefu sana na ninyi wawakilishi wao mmeliongea jambo hili kwa kirefu sana.

Mheshimiwa Spika, kwanza nawaomba, Serikali inajali sana hoja hizo ambazo wenzetu wanazitoa. Serikali inajali sana, lakini la pili ni Serikali hii ni sikivu sana na inasikiliza sana hizo hoja za wenzetu hao walioko kwenye sekta binafsi. Moja ya jambo ambalo kwenye mtazamo wa kiuchumi wa Mheshimiwa Rais amelipa kipaumbele kikubwa ni kuhakikisha nchi hii uchumi wake unaongozwa na sekta binafsi, sisi Mawaziri ni nani hata tusitekeleze haya? Maono yake ni kuhakikisha uchumi huu unaongozwa na sekta binafsi, sisi Mawaziri ni nani hata tusitekeleze hilo? Kwa hiyo, kiongozi yeyote aliyeko Serikalini huu ndio mwelekeo wa Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba, tunailea sekta binafsi na sekta binafsi ina uwekezaji na ina biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na Waheshimiwa Wabunge, jambo hili ninyi kule ndio wawakilishi wa wananchi, waambieni ndugu zetu hawa wala hatuna haja ya kuvutana kwa sababu, sisi Serikalini na wao tunaongea lugha moja. Mimi kila nikionananao huwa nawaambia hamhitaji hata kugoma kutekelezewa mambo yenu kwa sababu, kile mnachokisema ndicho Mheshimiwa Rais anachoelekeza. Ingekuwa na maana sana kama mnachokisema Serikali iko kinyume na hicho, hapo ndipo ambapo nguvu huwa inatumika. Kwa hiyo, mimi nawaomba wenzetu wala tusijirudishe nyuma, sisi kama nchi, kwa mambo ambayo tunakubaliana mtazamo. Twende tuwe tunakaa tunaongea hoja moja-moja na tunapoongea hoja moja-moja tunaongelea nchi yetu na tunaongelea maisha yetu.

Mheshimiwa Spika, sisi tumekaa na ndugu zetu hawa ambao tumewaambia wafanyabiashara kama Rais anawasikiliza anaweza kutenga siku nzima, huwa anakaa nanyi sekta binafsi anawasikiliza siku nzima. Waziri Mkuu alisimama pale, wao wenyewe wanajua, saa nane mpaka kumi anawasikiliza, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu amewasikiliza, sisi Mawaziri wa nne tumeenda tumewasikiliza, kama tunasikiliza na tunakubaliana hoja moja-moja na hatujakataa kuendelea kuzifanyia kazi, kwa nini tushinikizane kwa mgomo?

Mheshimiwa Spika, migomo hii inaturudisha nyuma kama Taifa na inarudisha nyuma familia moja-moja. Kwa hiyo, kwa sababu, tunasikilizana mimi rai yangu ni hatuna haja ya kutumia utaratibu wa nguvu, twendeni tuendelee na utaratibu huu.

Mheshimiwa Spika, mwaka jana sekta binafsi walituambia tupandishe wigo ule wa kuandikisha VAT, tulifanya hivyo. Tulipotoka Kariakoo tulifanya hivyo na tukakubaliana tutandelea kwenda hatua kwa hatua. Hata hoja nyingine inawezekana zipo ambazo hatujatekeleza, sio kwa sababu ya kukataa, tumekuwa na hoja ambazo tumefanya engagement; kwa mfano, moja ya hoja ambayo ilikuwa inatolewa ilikuwa inahusisha kushusha VAT kutoka asilimia 18 kwenda asilimia 12. Hata mimi ningetamani iwe kumi na mbili, ningetamani iwe hata kumi, lakini hatujaacha tu kuishusha kwa sababu ya kiburi cha Wizara, wala hatujaacha kuishusha kwa sababu ya Serikali tu kukataa, tumeacha kushusha kwa sababu tuna mambo mengi tunatekeleza. Ukishusha asilimia mbili tu VAT unapoteza shilingi bilioni 600 kwa mara moja.

Mheshimiwa Spika, ukishusha hivyo na tuna miradi mikubwa, kama Taifa tunaitekeleza inaathiri bajeti, ukishusha kwa kiwango hicho unakuwa na asilimia kumi, itaathiri. Wapo wengine wangedhani ukishusha hivyo, itaongeza volume, sasa kabla hujapata hiyo volume iliyoongezeka ukishusha na miradi ipo inatakiwa itekelezwe, inatekelezwaje? Kwa hiyo, tumesema twende nayo hatua kwa hatua na hii tunapunguza mzigo wa miradi, tunaenda kwenye huo utaratibu na Serikali ilishaweka hilo lengo la kuendelea kupunguza huo utaratibu.

Mheshimiwa Spika, hivyo hivyo hata ile service levy; service levy yetu hii, Waheshimiwa Wabunge ninyi mnatoka kule majimboni, inachangia zaidi ya asilimia 25 ya uendeshaji wa Halmashauri zetu sasa ukiitoa kwa mara moja kabla hujaleta mbadala kutakuwepo na chaos kwenye Halmashauri zetu. Kwa hiyo, hili na lenyewe tumeongea na wenzetu, tumelipokea, na tumesema tunatafuta utaratibu wa kuweza kupata mbadala wa uendeshaji wa Halmashauri zetu huku tukipunguza, ili ufanyaji kazi uwe mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, walileta tuanzishe utaratibu wa bei elekezi; tumekubaliana na wenzetu wa sekta binafsi. Tutaanza na bidhaa nane kwa kuanzia kutekeleza utaratibu huu.

Mheshimiwa Spika, kulikuwepo na mambo ya consolidation na deconsolidation; tumekubaliana tunaanza kuanzia tarehe moja na wenzetu. Tutaanza kuanzia tarehe moja na wenzetu, tutaanza utekelezaji na mengine tunajenga mifumo.

Mheshimiwa Spika, haya mengine ambayo tunalalamikiana sasahivi ni transitional, tunakokwenda kule mbele tutaelewana. Kwa hiyo, mimi natoa rai kwa wenzetu hawa, wala tusiende kwenye utaratibu huu ambao unatusababishia matatizo kwa wote.

Mheshimiwa Spika, hivyohivyo na masuala ya kiukaguzi; hiyo na yenyewe tumesema tunakamilisha mifumo. Mfumo wa kodi za ndani pamoja na mfumo wa forodha ambayo itaenda kutuondolea haya matatizo ambayo yanajitokeza.

Mheshimiwa Spika, mambo mengine ambayo yamelalamikiwa ambayo ni ya kiutawala; tumeshapata ridhaa, Mawaziri wa Kisekta wala hatutawaita kituo kimoja, tutazunguka kule mikoani. TRA watakuwepo, Wizara ya Mipango itakuwepo, Wizara ya Biashara itakuwepo, Wizara ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI itakuwepo na Wizara ya Fedha itakuwepo. Tutatatua haya mengine ambayo ni ya kiutawala ambayo yanatukwamisha, wala hatuna haja ya kulumbana, nchi hii ni yetu sote.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kuna mapendekezo mengine yalikuwa yametolewa ya kuwaondoa machinga Kariakoo, waondoeni machinga kwenye maeneo haya. Hilo na lenyewe, Mheshimiwa Rais alishatoa maelekezo kwamba, hatatumia nguvu ya dola wala migambo kuwaondoa machinga, atawatengenezea utaratibu mzuri wa kipato wa kufanya shughuli hizo, ili waweze kufanyia shughuli katika eneo mbadala bila kuathiri shughuli zao kwa hiyo, haya ndiyo ambayo yanaendelea.

Mheshimiwa Spika, kuna maeneno ambayo tumeshafanya. Kwa mfano, Dodoma, mnaona pale ambapo wanafanya kazi ndugu zetu, wanafanya kazi nzuri kabisa. Hata Dar es Salaam tunajenga masoko, tukishamaliza mpangilio mzuri wa ufanyaji kazi utafanyika. Hii na yenyewe si kwamba, tumewakatalia wenzetu wafanyabiashara, lakini tulikuwa tunajali kwamba, wafanyabiashara ni watoto wa mama na ninawaheshimu sana na machinga ni watoto wa mama na nina waheshimu sana na sisi ndicho ambacho tunakitekeleza na hivyo ndivyo ambavyo Serikali inatekeleza. Yale mengine yote ambayo ni ya kiutawala, sisi kama Serikali tumeyapokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine zote ambazo zilitolewa na Kamati ya Bajeti ambazo zinahusisha vifungu kwa vifungu, ninaweza nisipitie kifungu kwa kifungu kwa sababu, tumeenda kwenye vile vifungu na tumefanya engagement na kamati. Almost tumeelewana katika maeneo hayo ambayo walikuwa wameyaweka.

Mheshimiwa Spika, hivyo hivyo na hoja nyingine ambazo zimetolewa na Mbunge mmoja mmoja; nyingine zimeshatolewa majibu na Wizara za Kisekta, lakini zile ambazo zimetolewa na Wabunge kwenye hoja moja moja ambayo inahusiana na Sheria ya Fedha, tumezifanyia kazi, kesho tutakaposoma Hotuba ya Marekebisho ya Sheria ya Utungaji wa Sheria ya Mwaka huu tumeweka yale ambayo Waheshimiwa Wabunge waliyasema. Tumeyarekebisha na tumeweka yale mengine ambayo tumeyafanyia marekebisho, ili kuweza kuhakikisha kwamba, hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge wamezisema zinaweza kuonekana katika Sheria hii mpya.

Mheshimiwa Spika, la mwisho, narudia kwa kuwashukuru sana na kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge. Bunge hili limekuwa Bunge makini sana, Bunge objective sana, ambalo linajali maslahi ya Taifa letu. Wabunge hawa tunashirikiana nao kuanzia kwenye kamati na mara zote wamekuwa wakitoa hoja zinazojenga nchi yetu na ndio maana Serikali imekuwa haipati ukakasi katika kukubaliana na hoja hizo.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo kaka yangu Mheshimiwa Profesa Kitila amesema, hoja hizi mwanzoni nilikuwa sijafanya utafiti huu, kumbe sio tu kwamba, zinatolewa na Waheshimiwa Wabunge wazalendo, lakini ni Wabunge ambao wanaelewa wanachokisema na ndio maana michango yao ambayo wanaitoa imekuwa michango makini sana. Kwa hiyo, sisi tumepokea hizo hoja zote, tutapata fursa ya hoja moja-moja na zile ambazo tutakuwa tumekubaliana na kamati tutakuwa tumekubaliana kwa niaba ya Bunge na tumefanya hivyo kwa engagement ya takribani muda wote ambao tumekuwa hapa, tumekuwa tukifanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, mwisho. Namshukuru sana na kumpongeza Kaka yangu Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo, tunafanyanae kazi kwa ukaribu sana na mimi huyo ni kaka yangu na hii imerahisisha sana ufanyaji wa kazi kwa sababu, timu zetu wanakaa pamoja na wanafanya kazi vizuri sana. Ndio maana hata tunapokuwa na majukumu haya, tunapokwenda kwenye kamati tunaenda tukiwa na mambo ambayo sisi tumefanya kazi pamoja. Hivyo hivyo na Wizara za Kisekta tunafanya kazi kwa ukaribu sana na Wizara nyingine zote za kisekta.

Mheshimiwa Spika, kwenye haya mambo ya kodi na mambo ya fedha tumefanya vizuri sana kazi pamoja na Wizara ya Mipango, Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara zile za sekta za uzalishaji tumefanyanao kazi kwa pamoja kwa ukaribu sana kuweza kuhakikisha kwamba, masuala haya yanafanyiwa kazi ipasavyo. Tumefanya marekebisho mengi, mtayaona kesho.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo lilikuwa limeongelewa sana ni kuhusu hili lililokuwa linagusa sekta za uzalishaji. Tutakapokwenda kwenye kupitia vifungu vya Kisheria kuna mapendekezo ambayo tumesikiliza maoni ya Kamati ya Bunge pamoja na maoni ya Mbunge mmoja-mmoja.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Prof. Kitila ameongelea kuhusu uwekezaji tunaoufanya, ameongelea eneo la sekta ya sukari. Kuna jambo lingine lilikuwa linatolewa kuhusu, kama hivi tunavyoitwa maskini, hivi tutatoka lini?

Mheshimiwa Spika, kwanza hivi tunavyoongea Benki ya Dunia imeleta barua ambayo inasema wanatuma watu wa kufanya evaluation, kuangalia kama Tanzania inastahili kuendelea kuwa miongoni mwa nchi maskini zaidi Duniani. Kwa hiyo, zoezi hili linaendelea na wenzetu wanatuona. Mambo ambayo anayafanya Mheshimiwa Rais ni yale yanayoenda kutoa jawabu la kipato cha mtu mmoja-mmoja.

Mheshimiwa Spika, kulikuwepo na hoja ambazo zilikuwa zinatolewa, za kitaalam tu kwamba, kipato cha mtu kimefika kiwango cha kipato cha mtu cha kati cha chini, lakini kulikuwepo na hoja za mtu mmoja-mmoja akijitokeza akisema, lakini tunaambiwa tuko kipato cha kati na kipato cha kati kiwango chake ni zaidi ya dola 1,040 ambayo ilishapatikana. Mtu mmoja-mmoja sasa anajiuliza, Je, hivi ni kweli mimi ninaipata hiyo?

Mheshimiwa Spika, zile zilikuwa numbers. Umechukuliwa wastani wa uzalishaji ndani ya nchi ukagawanywa kwa wastani wa idadi ya watu ndani ya nchi, lakini anachofanya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, hivi tunavyoona kwenye uwekezaji kwenye sekta za uzalishaji, anaenda kutibu jambo la kipato cha mtu mmoja-mmoja kwa uhalisia wake. Ndio maana kwa sasa hivi tunaona zinakwenda shilingi bilioni 40 kwenye kijiji kutekeleza mradi wa umwagiliaji. Wale waliokuwa wanazalisha kwa uhafifu kwa mara moja wakizalisha mara tatu kwa ufanisi hawawezi kuendelea kuwa maskini kama walivyokuwa. Kwa hiyo, hii inaenda kutibu lile tatizo la kipato cha mtu mmoja-mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, fedha zimekwenda kwenye vijiji kwa kiwango ambacho hazijawahi kutokea, zinakwenda kwenye sekta ya uzalishaji. Tumeona kwenye umwagiliaji, lakini tumeona hata kwenye hii BBT ambayo inaendelea kwa sekta zote. Hii inawapeleka vijana wawe kazini, huwezi ukainua kipato cha mtu mmoja-mmoja ukiwa una-unemployment kubwa kwenye nchi husika. Kwa hiyo, hii inayowapeleka vijana wawe kazini inaenda kutibu kipato cha mtu mmoja-mmoja na future ya nchi hii iko kwa vijana. Lazima tuwapeleke vijana wawe kazini na tukishawapeleka utaona kwamba, kipato cha mtu mmoja-mmoja kitakwenda kuongezeka.

Mheshimiwa Spika, suala la marejesho tumeliongea ni suala la kiutawala. Suala la kero bandarini kati ya mtu mmoja-mmoja anapobeba mzigo kutoka Bara kwenda Zanzibar na kutoka Zanzibar kuja Bara tumelichukua ni la kiutawala. Tutayafanyia kazi hayo kuweza kuhakikisha kwamba, hayaleti matatizo.

Mheshimiwa Spika, tumepokea masuala ya akaunti za wafanyabiashara, yaliongelewa masuala ya M-koba Bank pamoja na maeneo mengine yanayohusiana na hayo. Tumeyapokea na ninadhani ni masuala ya kiutawala, tutaenda kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, haya ya kuifanya NFRA iagize sukari; wale tunaowaita wafanyabiashara ni wafanyabiashara na wale wenye viwanda na wenyewe ni wafanyabiashara. Sisi tumeona, ili kuweza kutibu suala la bei ya sukari, hasa inayohusiana na masuala ya upungufu, tutumie taasisi hii ambayo imesaidia kwenye bei ya bidhaa nyingine kuweza kuhakikisha kwamba, inamfikia mlaji katika bei inayohusika.

Mheshimiwa Spika, moja ya jambo linalokera pale Serikali inapotoa msamaha, ni wale walioko kwenye hiyo sekta, wanaofanya kazi za biashara, kudhania ule msamaha uliwalenga wao. Tumeona haya katika maeneo mengi; tulitoa kwenye smarts phone, simu janja na vitu vingine, badala ya kuwanufaisha Watanzania ikakwamia katikati. Tulitoa kwenye dippers badala ya kuwanufaisha Watanzania ikakwamia katikati, hata kuna wakati tulikuwa tunatoa shilingi bilioni 100, kwa ajili ya kushusha bei ya mafuta, hata hiyo haikwenda asilimia yote kwa maana kwamba, bei ile imnufaishe mia kwa mia yule ambaye Mheshimiwa Rais alikuwa amemlenga.

Mheshimiwa Spika, hivyohivyo na kwenye sukari. Bei imekuwa ikishuka, lakini bila kutumia huu utaratibu kumekuwepo na matatizo ndio maana Waziri wa Kisekta aliona kwa utaratibu huu ni lazima hili jambo tulisimamie, ili Mtanzania aweze kunufaika ipasavyo. Kwa hiyo, sisi kama Serikali tumeona haya mambo ni lazima tuyafanyie utawala wa karibu, ili kuweza kuhakikisha kwamba, yanamnufaisha Mtanzania mmoja-mmoja ambaye alikuwa amekusudiwa.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa muda huu kwa mara nyingine. Hoja hizi, kama nilivyosema, zote tumezichukua na tutazifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, baada ya ufafanuzi huu, kwa mara nyingine nakushukuru wewe mwenyewe na wataalam wote ambao wamefanya kazi ikawa nyepesi, nawashukuru na Waheshimiwa Wabunge. Naomba sasa kutoa hoja.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)