Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipatia nafasi na ninaunga mkono hoja zote ambazo zimewasilishwa hapo mezani na mchango wangu utajielekeza kwenye vyanzo vya mapato na nimeweka katika makundi manne. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, chanzo cha kwanza cha mapato; kabla sijaanza kuelezea chanzo hicho cha mapato, ninaomba ni-quote kitabu kitakatifu Biblia kwenye mistari kadhaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nisome Kutoka 4:1-8 nao unasema; “Musa akajibu akasema, lakini, tazama, hawataniamini, wala hawataisikia sauti yangu; maana watasema, BWANA hakukutokea. BWANA akamwambia, ni nini hiyo uliyo nayo mkononi mwako? Akasema, Ni fimbo. Akamwambia, itupe chini; akaitupa chini, nayo ikawa nyoka; Musa akakimbia mbele yake. BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako, ukamshike mkia; (akaunyosha mkono wake akamshika mkia, naye akageuka kuwa fimbo mkononi mwake); ili kwamba wapate kusadiki
ya kwamba, BWANA Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amekutokea. BWANA akamwambia tena, Sasa tia mkono wako kifuani mwako. Akautia mkono wake kifuani mwake; naye alipoutoa, kumbe! mkono wake ulikuwa una ukoma, ghafla umekuwa mweupe kama theluji. Akasema, Tia mkono wako kifuani mwako tena. Akautia mkono wake kifuani mwake tena, na alipoutoa kifuani mwake, kumbe! umerudia hali ya mwili wake.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, mstari wa nane na wa mwisho; “Basi itakuwa, wasipokusadiki, wala kuisikiliza sauti ya ishara ya kwanza, wataisikiliza sauti ya ishara ya pili.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasoma tena Kitabu hicho hicho cha Kutoka 17:4–6, maandiko yanasema; “Musa akamwambia Bwana, akisema, niwatendee nini watu hawa? Bado kidogo nao watanipiga kwa mawe. Bwana akamwambia Musa, pita mbele ya watu, ukawachukue baadhi ya wazee wa Israeli pamoja nawe; na ile fimbo yako ambayo uliupiga mto kwayo, uitwae mkononi mwako, ukaende. Tazama, nitasimama mbele yako huko, juu ya lile jabali katika Horebu; nawe utalipiga jabali, na maji yatatoka, watu wapate kunywa. Musa akafanya hivyo mbele ya wazee wa Israeli. Ameen.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kusema nini, lengo la maandiko haya, fimbo hiyo hiyo ambayo nimesoma katika sura hizi mbili tofauti ndiyo fimbo hiyo hiyo wana wa Israel waliitumia Musa akapiga mto, mto ukagawanyika wakapita katikati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chanzo cha kwanza cha mapato; chanzo cha kwanza cha mapato ni mapato yetu ambayo yako tayari yanajulikana kwenye vyanzo vyetu vya mapato vilivyopo. Changamoto iliyopo ni namna ambavyo hatuzitendei haki taarifa za CAG. Mapato tuliyonayo tungeamua kuzitendea kazi zile taarifa za CAG, vyanzo vilevile tulivyonavyo vingeweza kufanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nachukulia hii ni kama fimbo ya Musa kwamba kile tulichonacho tukiamua kuking’ang’ania na kukitumia vizuri kinaweza kufanya maajabu na kutenda maajabu ndani ya Taifa letu, lakini kwa sababu imani yetu imepungua hata ambapo Waheshimiwa Wabunge tukiongea hatusikilizwi, CAG akileta taarifa hapa Bungeni akisoma, mtu anakuja kujitetea mbona CAG ametupa hati safi. CAG ametoa hati safi wakati kule ndani ameeleza kuna changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tayari sisi tunayo fimbo ambayo ingeweza kufanya mambo makubwa ingeweza kupasua mto katikati na tukapita. Kwa hiyo, tunapotafuta vyanzo vipya vya mapato, kwanza tuangalie mkononi kwetu tuna nini, kwenye mkono tunayo fimbo ambayo inaweza ikageuka ikawa nyoka na bado tukaitumia ikaweza kutuletea maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyanzo vyetu hivi vya mapato tuvitendee vizuri na tusione Taarifa ya CAG kama ni kwa ajili ya kutukosoa, Taarifa ya CAG ni kwa ajili ya kutuimarisha. CAG mlinzi kwenye nyumba yetu ambaye tumemuweka analinda vitu vyetu vya thamani, lakini mlinzi huyo anapokwambia nimeona changamoto, tena unamwambia hakuna shida, huyo mwizi anayetaka kuiba wewe muache tu. Sasa ulimuweka wa nini? Si ulimuweka aweze kukulindia mali zako za thamani, anakusaidia kujua hapa pana shida, hapa pana shida, ungechukua taarifa yake ukaifanyia kazi vizuri inawezekana usingeweza kupata shida. Kwa hiyo, vyanzo vyetu vya mapato tulivyonavyo sasa, tuweze kuvilinda na tutumie Taarifa za CAG ili tusiendelee kutoboa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, chanzo cha pili ni biashara za cross borders, international trade; biashara nyingi ambazo ni international trade hakuna mahali ambapo hazifanyi vizuri. Tumeshuhudia namna ambavyo zinafanya vizuri, nami sitaacha kuongelea soko la DRC. Soko la DRC sisi tuko hapa tumepakana na Congo uso kwa uso, lakini mataifa yanayotoka mbali yananufaika na Congo vizuri. Hatutumiii neema ambayo tumepewa na Mwenyezi Mungu, na yenyewe hii ni fimbo nyingine Mungu ametupa, tungeweza kuitumia vizuri, ingeweza kuleta miujiza na matokeo mazuri kwenye Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 28 Oktoba, 2024 wiki moja tu ambayo imepita Serikali ya China pamoja na Serikali ya DRC ilizindua barabara yake yenye urefu wa kilometa 466 kutoka mji wa Kalemii, Jimbo la Tanganyika kwenda Manono ambako China wamejenga kiwanda kikubwa sana cha kuzalisha lithium na wanatarajia kusafirisha hiyo lithium, metric tani zaidi ya laki tano kutoka Bandari ya Kalemii kuja kwenye Bandari yetu ya Kigoma, watatumia railway tunaita SGR kwenda kutumia Dar es Salaam Port na kupeleka China. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mara kadhaa nimekuwa ninaongea hapa kwamba kwa nini na sisi tusijenge barabara kutoka Kalemii au Moba kuelekea Lubumbashi ambako kuna soko? Lakini Mchina huyo huyo ameshaanza kujenga railway kutoka Angola kuja Lubumbashi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa China anakotoka huko Bara la Asia kuja mpaka huku kwetu na sisi DRC tunaye hapa, basi wazo langu maadamu Mchina ameshaweka barabara kutoka Manono kuja Kalemii, Jimbo la Tanganyika DRC, na sisi tuka-connect barabara kutoka Manono kwenda Lubumbashi ambazo zinapungua zinakuwa kama kilometa 470 hivi wakati tunaendelea kujenga barabara kutoka Moba kwenda Lubumbashi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo yote ni kwa faida gani? Ni kwa faida yetu wenyewe. I don’t think kama China kusingekuwa na manufaa ya mambo yote haya angeamua kuweka uwekezaji wote, as we are speaking now ukiangalia nchi ambayo inaongoza kufanya biashara na DRC, sisi hata kwenye top four hatupo na ni majirani zetu. Kenya wapo huko mbali wanafanya vizuri biashara na DRC. Soko la Congo siyo la kupuuza litaleta ajira nyingi sana kwa vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, chanzo kingine cha tatu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Muda wako umekwisha.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninahitimisha.

MWENYEKITI: Lakini hitimisha.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, chanzo cha tatu cha mapato ni border; nimeshachangia tena hapa kwamba pale Momba tunalo gate ambalo katika kutoa michango yetu, wenzetu upande wa pili Zambia walivyogundua wameshaweka gate toll. Kwa hiyo, chochote kinachopita kule kwao kinapita wanaingiza mapato, lakini sisi kwetu magendo yanaendelea kuingia, yanaendelea kupita, njia iko wazi, kwa hiyo, ni jambo la muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho tuwekeze kwa wakulima, mkulima wa nchi hii bado analima kwa kutumia jembe la mkono. Tuwekeze kwa mkulima kwa sababu ndiyo chanzo kimojawapo cha mapato ndani ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa tunaomba Vodacom wapunguze gharama za ma-bundle. (Makofi)