Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BALOZI LIBERATA R. MULAMULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nakushukuru kwa kunipatia fursa hii na mimi nichangie kwenye Bajeti ya Serikali na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa 2024/2025, hoja mbili zilizoko mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwapongeza kwa dhati Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji na pacha wangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha kwa hotuba na wasilisho zuri sana la Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Bajeti ya Serikali vinavyotupatia mwanga wa mbele tunapokwenda na kutupatia matumaini makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kuunda Wizara ya Mipango inayojitegemea na Wizara ya Fedha maana uzoefu umeonesha kwamba mipango lazima iongoze hazina na si vinginevyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakika inafurahisha kuona Mawaziri wetu pamoja na Naibu Mawaziri wakiwa wameketi pamoja kama mapacha katika kuwasilisha Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/2025. Unaona kabisa kwamba mpango na bajeti vinasomana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, nimefurahishwa na mtiririko mzuri wa Hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali kuanzia shabaha, malengo, misingi ya bajeti, vipaumbele, ufuatiliaji na tathmini na mafanikio ya Serikali ya Awamu wa Sita na kuimarika kwa sekta za uzalishaji, viwango vya kodi na kadhalika. Katika kusikiliza kwangu na kusoma hotuba zote mbili nimevutiwa na mambo matatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, ni dhima ya kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu (people centered development). (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nimevutiwa na msisitizo wa usimamizi wa matumizi ya Fedha za Umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, nimevutiwa na maeneo ya vipaumbele kwa mwaka wa fedha 2024/2025 yaliyoainishwa kwenye Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2021/2026 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2024/2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimevutiwa na msisitizo wa kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma. Niseme kwamba, Tanzania ya Viwanda inawezekana, tukiamua itawezekana. Nchi yetu imejaaliwa nguzo muhimu za kuwezesha Tanzania kuwa Tanznaia ya Viwanda kama hivyo vilivyosemwa hapa. Tuna jiografia za kimkakati, madini, maji ya kutosha pia tuna nguvukazi ya vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia diplomasia nzuri ambayo imetufungulia fursa za Masoko ya Ulaya, Asia na Mabara yote. Pia, tuna masoko yanayotuzunguka ambayo tunayamudu kwa hali yetu ya sasa katika Afrika Mashariki na SADC.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho lakini siyo kwa umuhimu tuna amani na utulivu ambao peke yake ni kigezo muhimu katika maamuzi ya uwekezaji na Mheshimiwa Waziri wa Fedha amelisisitiza hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuwa na vyote hivi bado sisi hatujaweza kuwa Tanzania ya Viwanda. Hii maana yake nini? Maana yake kuna kitu kinakosa. Tunakosa ufungamanishaji (packaging) wa vitu hivi, ili kuvitafsiri katika matokeo ya uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni maarifa na teknolojia, tunayo mahusiano mazuri na karibu na dunia nzima, tuyatumie kuvuta maarifa hayo na teknolojia hizo nchini. Tutumie fursa ya upepo wa dunia kuelekea kwenye nishati ya kijani, kuvutia viwanda kwa kutumia madini ya kimkakati yaliyopo nchini ambayo kesho ndiyo yatatufikisha katika dunia ya sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kuhusu sekta ya viwanda katika Mkoa wa Kagera; Mkoa wa Kagera unasikitisha kwamba ni mkoa ambao una rasilimali zote, una madini na unaweza ukawa kitivo cha viwanda, lakini mpaka leo tunavyoongea sijui kama kuna kiwanda ambacho wanakiita kama kiwanda. Kwa hiyo, mimi rai yangu kwa Serikali ni kwamba kwa kweli hatuwezi kufika mbali kama hatuupi umuhimu wa sera ya viwanda ambayo inaimarisha uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa kabla hujaniondoa, niseme kwamba ili tufanikishe utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Bajeti Kuu ya Serikali, tunahitaji tuwe na mfumo thabiti na endelevu na ufuatiliaji na tathmini (monitoring and evaluation). (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha amesema ataviongezea nguvu vitengo vyote vya ufuatiliaji na tathmini, lakini nikumbushe, huko nyuma Kamati ya Bunge ya Bajeti ilishauri kuwepo sheria na sera maalumu ambazo zimeambatanishwa kuwa ndiyo msingi katika kuhakikisha masuala ya ufuatiliaji na tathmini yanakuwepo katika utekelezaji. Ni vyema ushauri huo ukazingatiwa katika utekelezaji wa bajeti na mpango wetu wa maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)