Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitaanzia pale ambapo Mheshimiwa Bulaya alianza jana ambaye ni Mama Kikokotoo ama amekuwa ni sauti ya watumishi wa umma kwa kipindi kirefu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanzia kwenye historia kwa sababu tuko na Waziri wa Mipango na Waziri wa Mipango amesema, moja kati ya utekelezaji wako wa mpango wa mwaka 2021 – 2025 ni kuchochea maendeleo ya watu. Sasa watu tunaowazungumza ni pamoja na watumishi wetu wa umma, watumishi wa sekta binafsi na ni bahati mbaya sana Makatibu Wakuu wetu, wataalamu wanaowasaidia ninyi ndiyo watu ambao tunawazungumzia hapa. Kwa hiyo, kama tunazungumzia maendeleo ya watu na hasa katika eneo hili la mafao ya wastaafu, ni muhimu mkalichukulia kwa uzito mkubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na historia kwa nini tumefika hapa tulipo, nikirejea Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu Ukaguzi wa Mashirika ya Umma ya mwaka 2021/2022, ukurasa wa 23 akizungumzia mkopo wa PSPF kwenda Bodi ya Mikopo, kipindi hicho ilikuwa shilingi bilioni 58, akasema; “Serikali kuingilia maamuzi katika Mifuko ya Pensheni ndiyo chanzo cha matatizo ya kifedha ya Mifuko hii.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 58 wa Taarifa hiyo hiyo unasema, “Ukaguzi wa Mifuko uliofanyika (Actuarial Evaluation) ya mwaka ulioishia tarehe 30 Juni, 2010, ulionesha mambo yafuatayo; “Ilionesha kwamba hali ya Mifuko ni mbaya, ukadiriaji wa thamani ulibaini hasara ya shilingi trilioni 6.487 kwa mwaka unaoishia Juni, 2010.” Hatuwezi kwenda mbele bila kuangalia historia ya namna gani Serikali imechangia hili na kwa namna gani lazima mchukue hatua za ziada kuokoa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ripoti ya mwaka 2012/2013 ilikuwa na maneno sawasawa na maneno ya ripoti niliyotoka kuisoma. Nenda kwenye ripoti ya mwaka 2013/2014; hii ripoti ilipelekea kuundwa kwa Kikosi Kazi Maalumu kilichojumuisha Serikali yenyewe na wataalamu mbalimbali. Tarehe 24 Oktoba, 2014, taarifa iliwasilishwa kwenye Kamati ya PAC kwa kipindi hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wadau wote walikubaliana nini mwaka 2014; kwamba Deni la Serikali jipya kwa kipindi kile lilikuwa shilingi trilioni 1.875 pamoja na shilingi trilioni 7.1 ambalo ni deni linalodaiwa na PSSSF tangu mwaka 1999. Kilitokea nini, watumishi wa umma walikuwa wanachanga fedha ili wakistaafu walipwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, PSSSF ilivyoanzishwa na sheria zake, zile fedha ambazo watumishi walichanga Serikali mlisema, tunaomba muwalipe hao ambao walikuwa ni watumishi kabla ya mwaka 1999 ambao kimsingi Serikali ilitakiwa ninyi ndiyo muwalipe, mkaomba mfuko ulipe kwa pesa za watu wengine waliochangia mkisema mtarejesha. Mpaka mwaka 2013/2014 Serikali mlikuwa mnadaiwa shilingi trilioni 7.9075, lazima tuangalie past ili uweke mipango thabiti ya kwenda kulinda watumishi wetu, 40% mlichokisema is peanut kwa sababu ndani yake kuna mambo mengi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ripoti ya mwaka 2017/2018, page 94; deni jipya la Serikali lilikuwa shilingi trilioni 2.398, hii ni kutoka ile shilingi trilioni moja niliyozungumza. Hii haijumuishi shilingi trilioni 7.1 la pre 1998, kwa hiyo, mpaka mwaka 2017/2018 Serikali na CAG anasema hivi; “mifuko yote ya hifadhi ina madai makubwa ambayo ni chechefu. Mengi ya madeni ya Serikali na taasisi zake yalikuwa hayajalipwa mpaka tarehe 30 Juni, 2018, zaidi ya 98% ya madeni hayajalipwa.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya tunazungumzia leo kuwa yameiva, kwa hiyo, tunapozungumza haya mambo angalieni wataalamu wenu ambao kutwa, kucha wanakaa na ninyi wanawasaidia, angalieni ma-Accounting Officers ambao kutwa, kucha wanakaa wanawasaidia... (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa, Taarifa.
MHE. HALIMA J. MDEE: Ninaomba utulie, utakuwa na muda wa kujibu.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, Taarifa.
TAARIFA
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kumpatia taarifa Mheshimiwa Halima Mdee kwamba Deni la Serikali lilikuwa ni shilingi bilioni 731, lakini tayari Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, baada ya kuingia madarakani imeshalipa zaidi ya shilingi bilioni 500 katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, deni ambalo lilikuwa ni la pre 1998 lilikuwa ni 4.6 trillion ambalo pia mwaka 2021 Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imelipa kwa non-cash bond zaidi ya shilingi trilioni 2.18. Kwa hiyo, niliona nimpatie taarifa hiyo mchangiaji Mheshimiwa Halima Mdee. (Makofi)
MHE. HALIMA J. MDEE: Ninataka nikusaide kwamba kwanza...
MWENYEKITI: Sijakuruhusu Mheshimiwa, sijakuruhusu.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, okay. (Kicheko)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Halima Mdee, unapokea taarifa ya Mheshimiwa Waziri?
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siwezi kupokea taarifa yake kwa sababu ninataka akasome ripoti ya mwaka 2013/2014. Deni la pre 1998 lilikuwa shilingi trilioni 7.1, deni pamoja na riba, ninyi mnajua mlichokifanya mkalishusha from shilingi trilioni seven mkalipeleka shilingi trilioni nne. Mlijifutia riba kwa sababu you have that mandate, yes, that shilingi trilioni four ambacho nilikuwa ninakuja. Mmelipa shilingi trilioni mbili ya non-cash bond; wewe unajua bonds zinavyo-operate, pesa haipo mfukoni, mnalipwa vile vi-interests na ndiyo maana tumesema, mpaka sasa hivi, kwanza hiyo shilingi trilioni tatu mliitoa kimagumashi, hiyo tuachane nayo, hiyo shilingi trilioni nne yenyewe hamjailipa inavyotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna fedha zinaonekana zipo lakini in reality hazipo kwa sababu ni bond, sijui kama tunaelewana, ninadhani unanielewa kwa sababu na wewe unamiliki bond.
Kwa hiyo, tunaomba, hoja zilikuwa nini, baada ya hii mifuko kuvurugwa vurugwa na ripoti ya mwisho ya mwaka 2014 ya kusema mifuko imevurugwa vurugwa, mkaleta sheria, sheria ya kuunganisha mifuko. Tukawaambia hapa mmeleta sheria, kikokotoo, formula ile tuiweke kwenye sheria ili maslahi ya watumishi yawe yamelindwa ndani ya sheria. Ndiyo inakuja 540 iliyokuwepo as against 580.
Mheshimiwa Jenista alikuwa Waziri hapa, mkang’ang’aniza iende kwenye kanuni, tukasema ikienda kwenye kanuni Waziri atajiamulia ataleta vitu vya hovyo, ikaenda kwenye kanuni vikaja vitu vya hovyo 580. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ilikuwa ni mishahara gani inatumika kupiga mahesabu? Mishahara hii ya mwisho au mishahara average ya miaka mitatu? Mkasema kwa kipindi gani? Mkasema mtaweka kwenye kanuni. Mmeweka kwenye kanuni, hivi unaweza ukatafutiwa average ya mshahara wa miaka mitatu ili kujua fate yako ya baadaye? Hivi ni kweli, are we human beings? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama kweli dhamira ipo na nimesikia juzi mnasema ooh sisi tutalipa, alisema jana Mheshimiwa Ester, mnalipa kwa mandate ipi? Yaani ni nani anawapa mamlaka Serikali kulipa? Lipeni cha watu, pelekeni pesa kwenye mifuko, mifuko ijiendeshe watu walipwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninashangaa Serikali haizungumzi, juzi Rais anasema uwekezaji unafanyika kwenye mifuko isiyoeleweka eleweka, ninakuona mdogo wangu uko Nairobi unazindua kitega uchumi, nani anajenga kitega uchumi? Ndiyo maana Mheshimiwa Profesa Mkumbo, jukumu lako wewe ndiyo maana uko Ofisi ya Rais, wenzako shirikisha mawazo ya yes, lakini you have to coordinate, lazima Serikali izungumze; siyo leo Rais anazungumza hiki, kesho Msaidizi wa Rais yuko busy kule. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, feasibility study imefanywa na nani? Imethibitishwa na nani? Kwamba that investment ya kujenga ghorofa 22 inaenda kufanyika Nairobi? Ina faida kwa mifuko? Hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi niseme hivi; hii 40% ni cha mtoto kwa sababu 580 iko pale pale ambayo ni mbaya. Muda ambao u-buy hii average ya mishahara inapatikana ni kipindi kirefu sana ambayo ni mbaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leteni sheria hapa Bungeni, tuijadili sheria upya, tuangalie upya maslahi ya hawa wafanyakazi, ndiyo tutasema kweli Serikali mna dhamira. Mnavyotwambia mwaka 2029 maana yake mnatwambia yale yale, Mheshimiwa Dkt. Magufuli aliona kimewaka akasema wanaahirisha mpaka mwaka 2023. Pale katika watu wakaondoka zao, ilivyofika mwaka 2023, Mungu amlaze mahali pema peponi, ukarudi utaratibu wa zamani. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusifanye mambo kwa sababu tuna mtu anataka kufanya kwa matamanio na utashi wake. Tufanye mambo ambayo yatakuwa na ulinzi, whoever atakayekuja in future, mtumishi wa umma aangaliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, madeni ya wakandarasi, ni hivi... (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba na mimi uniongeze tano.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Hapana. (Kicheko/Makofi)
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ungeniongeza hata moja.