Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Mohamed Lujuo Monni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia bajeti hii muhimu ya Serikali.

Kwanza kabisa nawapongeza sana Mawaziri wote, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, Mheshimiwa Profesa Kitila na Manaibu wao pamoja na Makatibu Wakuu wa Wizara hizi muhimu. Naomba nichukue nafasi hii ya kipekee kabisa nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ya kipekee kwa namna ambavyo anawatendea wema wananchi wa Tanzania, lakini kwa namna ya kipekee ambavyo anawatendea wema Wananchi wa Jimbo la Chemba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina maeneo machache sana ya kuchangia. Eneo la kwanza ambalo ninataka kusema kidogo ni namna ambavyo fedha zinagawanywa kwenye maeneo yetu. Ni kweli kabisa kwamba, hapa leo tunapitisha Bajeti ya Serikali na tunaamini fedha hizi zinapaswa zigawanywe sawa kwenye miradi ya maendeleo katika Wilaya zote Tanzania, lakini kumekuwa na uwiano hafifu sana wa kwenye majimbo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mfano kidogo. Tunafahamu fedha za maji hazikutoka zote kwenye bajeti iliyopita, lakini yapo maeneo ambayo miradi imepelekewa fedha 90%, yapo maeneo ambayo miradi imepelekewa fedha kwa 35%. Sasa mimi naomba, tunapitisha bajeti hii, mimi nina miradi 17 ya maji, kwenye bajeti hii naogopa kwamba tunapitisha bajeti ambayo inaenda kuhudumia miradi 17 ya maji, lakini fedha zikienda 35% maana yake miradi hii inaenda kukwama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachoumiza zaidi ni ile kwamba, maeneo mengine fedha imetoka 35%, maeneo mengine imetoka 90%. Mimi naomba sasa Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kama kuna hali yoyote ya upatikanaji hafifu wa fedha au mapato kidogo yametikisika, tutoe fedha kwa ratio sawa kwenye Halmashauri zetu au kwenye Wilaya zetu. Hii inaweza kusaidia sana kutoka pamoja kama nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwamba, tunaenda kujenga bwawa kubwa pale Farkwa. Mradi huu umekuwa wa muda mrefu sana, bahati nzuri safari hii kandarasi imetangazwa. Namuomba Mheshimiwa Waziri anayetoa fedha, hebu tuletee fedha, ili tumalize jambo hili la muda mrefu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niseme kidogo kuhusu mapato. Wabunge wote hapa wamechangia kwamba kuna shida ya ukusanyaji wa mapato na hii haina mjadala. Hatunashaka hata kidogo na Mheshimiwa Waziri wa Fedha Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, hatuna shaka na Mheshimiwa Profesa Kitila, lakini hii changamoto imekuwa kubwa. Ni kweli kwamba, Watanzania hawalipi kodi, je, nani anayepaswa kukusanya hizo kodi? Ukifuatilia takwimu kwa miaka mitatu hii, ukienda BRELA utakuta watu waliokuwa registered kwenye biashara Group A au Grade A ni zaidi ya 53,000, lakini margin ya kodi average kwa miaka mitatu mfululizo ni ileile shilingi trilioni 2.3, trilioni 2.1 sasa hao wanaoongezeka hawalipi kodi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu changamoto hii ndiyo inayotuletea shida kwenye majimbo huko, ndiyo inayotuletea shida kwenye Wilaya huko. Wenzangu hapa wanasema kwenye mfuko wa maji zaidi ya shilingi bilioni 200 hazikutoka; haziwezi kutoka kama kuna makusanyo hafifu kwa sababu, Serikali haina duka. Sasa tusibaki tu kila siku tunalalamika kwamba, fedha za mapato hazikusanywi, Watanzania hawalipi kodi, lakini tuna watu tumewapa kazi ya kuhakikisha wanakusanya fedha hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nani tumlaumu? Tumlaumu Mheshimiwa Waziri? Tumlaumu Naibu Waziri? Tumlaumu Katibu Mkuu au tumlaumu nani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafikiri ni lazima kama Bunge tuangalie sasa ni nini changamoto ya fedha hizi kutokukusanywa. Mtu mmoja amesema hapa yeye tukimpa ile Bandari tu ya Dar es Salaam inatosha kutuletea hizi fedha zote tunazopata kwa mwezi. Sasa maana yake ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba, kuna loophole nyingi ambazo zinasababisha upotevu huo wa mapato. Sasa mimi naomba nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, hili jambo limesemwa sana, kila mwaka linasemwa hilo hilo na hakuna tamko rasmi la ni nini tufanye, ili tuhakikishe tunakusanya kodi hizo na hilo ndilo linalotuletea matatizo mengi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni mipango yetu. Nimesikia Wabunge wengi wanasema kuhusu mipango na ukweli migogoro yote ya ardhi, shida zote hizi za fedha kutokupelekwa sawa maana yake ni ukosefu wa mipango, maana yake ni tuna shida kwenye mipango. Unakuta jimbo linaupatikanaji wa maji 92%, lipo lingine lina 32%, tafsiri yake ni tuna mipango isiyo sawa. Sasa namuomba Mheshimiwa Prof. Kitila, ambaye namuamini sana, changamoto nyingi tulizonazo zinaweza kutibiwa kama tu tutakuwa na mipango mizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango ambayo inatekelezeka, mipango ambayo kila siku tukija hapa Bungeni tunasema hayohayo, lakini hayatekelezeki. Namuomba sasa Mheshimiwa Profesa, namfahamu ni ndugu yangu, rafiki yangu wa muda mrefu, hebu tubadilishie sasa. Ukienda kule kwangu, kila mwaka nasema hapa, kuna watu, wakulima zaidi ya 1,197 mashamba yao yapo wilaya nyingine na hauruhusiwi kwenda kulima kwa sababu, ya mipango haipo sawa. Ninaamini sana tukiwa na mipango mizuri ardhi yetu yote nchini tutaipima na kila mtu atajua kipato chake na tutapunguza karaha hii ya migogoro ya ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme maneno mawili, matatu, kuhusu hali halisi ya majimboni. Naomba sana Waziri, tuna changamoto ya vipaumbele vya Serikali kubadilika na hili ninafikiri Wabunge wote wameliona. Ukifuatilia Bajeti za Kisekta ni kama kipaumbele cha Serikali kime-shift, nataka niseme fedha za barabara sasahivi ni kama zimekuwa kidogo sana na ninyi mnafahamu kwamba, ili tuweze kukusanya kodi ni lazima tuwe na barabara nzuri. Fedha za Wizara ya Maji zimepungua sana na wewe unajua kabisa, ili mtu awe na afya nzuri aweze kukusanya kodi ni lazima apate maji. Mimi nawaomba sana, sasa ninataka kuwaona watalaamu hawa ni namna gani wana-shift kwenye vile vipaumbele muhimu vya Watanzania kwenda kwenye vipaumbele ambavyo sisi Wabunge wengi hatuvielewi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombeni sana katika hilo hebu tuangalie namna bora ya kuhakikisha kwamba, tunabaki kwenye vipaumbele vyetu muhimu ili nchi yetu iweze kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo…