Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ili na mimi niweze kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2024/2025. Bajeti hii inayoombwa ni Pesa za Kitanzania trilioni 49.8. Nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, kwa kazi nzuri anayoifanya. Pia nimpongeze Waziri wa Fedha, kwa kazi nzuri pamoja na Mawaziri wengine wote, kwa kweli wanamsaidia kwa ukaribu sana na kwa umahiri mkubwa Mheshimiwa Rais wetu kutekeleza majukumu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mchango wangu leo utajikita kwenye kuishauri Serikali namna ya kukuza uchumi kwenye eneo la lishe, lakini pia kwenye eneo la usalama wa chakula. Serikali imeweka mpango mzuri sana wa kuhakikisha kwamba kwenye eneo la lishe ili wananchi waweze kupata afya bora na waweze kuendelea kuzalisha na kulizalishia Taifa mapato yaliyo mengi zaidi kwenye eneo la uzalishaji ni kupitia ufugaji wa vizimba katika Ziwa Victoria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilitenga pesa zaidi ya shilingi bilioni 20 kupeleka kwenye maeneo hayo ili kufanyika uwekezaji wa vizimba hivyo. Vizimba hivyo vimefanyika zaidi kwenye ukanda wa Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika lakini tunafahamu kwamba katika nchi yetu ya Tanzania tunayo maziwa zaidi ya hayo ikiwepo Ziwa Nyasa. Naamini kabisa hata wawekezaji wa vizimba hivi walioko kwenye maeneo ya Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika nao pia walipata mafunzo, walielimishwa na ndiyo maana wakaweza kufanya uwekezaji huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha, mimi mwaka huu nikisimama hapa ni kusikitika tu juu ya suala la uendelezaji wa masuala ya kiuchumi katika Mkoa wangu wa Ruvuma hususani kwenye Ziwa Nyasa. Kuhusu Ziwa Tanganyika alisimama Mheshimiwa Mbunge hapa jana alikuwa analalamika kwamba wao wamepata vizimba 29 tu. Naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge huyo kwamba, sisi katika Ziwa Nyasa hakuna kizimba hata kimoja. Mnataka kutuambia kwamba, Wavuvi wa Ziwa Nyasa Wawekezaji wa Mkoa wa Ruvuma hawana uwezo wa kuelewa kama wataelimishwa juu ya uwekezaji wa vizimba? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kusiwe na ubaguzi kwenye uwekezaji kwenye maeneo yote katika nchi yetu. Maziwa yapo zaidi ya hayo mawili yaliyowekezwa lakini upande mwingine hakuendi. Keki hii ni ya kwetu sisi sote Watanzania, igawiwe sawa kwa sawa na maeneo mengine ambayo wanapewa fursa hii haipendezi na wala haitavumilika. (Makofi)
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, bado nipo kwenye eneo hilo hilo la lishe suala la ulaji wa samaki katika nchi yetu ya Tanzania imekuwa ni anasa…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Msongozi, kuna taarifa.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: …Mheshimiwa Sanga nakuomba sana nina mambo ya msingi sana ya kuchangia tafadhali sana usinitafunie muda.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Msongozi, kuna Taarifa. Tafadhali.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Leta Taarifa ya maana tafadhali. (Makofi/Kicheko)
TAARIFA
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kumpa taarifa dada yangu Mheshimiwa Msongozi, anachokizungumza kwenye Ziwa Nyasa ni kweli wavuvi wa ukanda ule wanapata shida. Serikali ya upande wa pili ya nchi jirani wana bajeti kwenye Wizara yao inayomwaga chakula pembezoni mwa Ziwa. Kiasi kwamba, samaki wote wamekimbia kutoka Tanzania wameenda kwenye nchi jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, anachokizungumza Mheshimiwa Mbunge ni sahihi kabisa hawatendei haki hasahasa kwenye suala la maendeleo ya eneo lile pale. (Makofi).
MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Msongozi, umepokea Taarifa?
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, una akili, ninaipokea Taarifa yako, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kama ifuatavyo: suala la ulaji wa samaki katika nchi yetu imekuwa ni anasa yaani Mtanzania kwenda kununua samaki kwa kweli samaki ni bei mbaya sana, lakini kulingana na uwekezaji huu sasa unaoenda kuwekezwa ninaamini kabisa utaongeza tija. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilidhani kwamba tungeongeza sasa kwenye uwekezaji wa eneo hilo turuhusu hata samaki wengine kutoka nje ya nchi waweze kuingizwa. Samaki watakapokuwa wanaingizwa kwa wingi katika nchi yetu basi suala la lishe… kwa sababu samaki ana virutubisho vingi lakini imekuwa ni anasa kumpata samaki huyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, familia nyingine hawawezi kula samaki kwa sababu hawana uwezo wa kumpata huyo samaki. Kwa hiyo, samaki hawa wakiruhusiwa kuingizwa kwanza tutaongeza Pato la Taifa lakini pia wananchi wataweza kunufaika kwa kupata lishe iliyo bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, chakula cha mifugo, mimi naona kabisa kwenye eneo la chakula cha mifugo tumefeli. Niwaambie wazi kwamba tumefeli kwa sababu unaangalia kwenye suala la wafugaji wanapata shida sana kwenye kupata chakula na wakipata hicho chakula unakuta chakula ni bei kubwa mno. Kwa mfano, wafugaji wa samaki na wawekezaji wa mabwawa unakuta chakula kilichokuwa kizuri kwa wao wanavyozungumza kinapatikana nchi za nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini chakula hicho kinapoingia nchini kinakuwa na tozo nyingi nyingi kiasi ambacho kikishaingia maana yake kinaendelea kuongeza bei kubwa kwa mlaji wa mwisho. Kiasi ambacho sasa uwekezaji ule unaokusudiwa kwenye ufugaji wa samaki haufikiwi. Mimi nadhani ni vizuri basi kuondoa zile tozo zisizokuwa za lazima ili wawekezaji hawa waweze kufanya vizuri kwenye uzalishaji wa samaki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Sukari; huu sasa ni uchangiaji wangu namba mbili ambao unahusisha suala la usalama wa chakula. Nichukue nafasi hii kwanza kuishukuru Serikali kuona umuhimu wa kuleta Sheria ya Sukari, kwa maana ya mabadiliko. Sheria hii ni vizuri sasa ikabadilishwa na ikarekebishwa ili kwenye eneo hili tuweze kupunguza urasimu ambao unaendelea katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la gap sugar ni jukumu la Serikali kusimamia na kuhakikisha kwamba inalinda hali ya walaji katika nchi yetu lakini pia kusiwe na upungufu wowote na hata kusababisha ongezeko la bei kubwa katika nchi yetu. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme, ukiwasha washa taa hiyo unanichanganya, labda ungeizima kwanza. (Makofi/Kicheko)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Msongozi, muda umeisha. Tuna changamoto ya muda tafadhali. Naomba hitimisha tafadhali.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya, nahitimisha. Sheria ya Usalama wa Chakula ni kama hivyo nilivyoeleza. Kuna vitu ambavyo vinasikitisha sana wawekezaji wa sukari katika nchi yetu wapo saba ambao ndio wenye viwanda. Wamekuwa wakilindwa katika nchi hii kwamba wazalishe wauze na kama inatokea gap sugar wao ndio wawe waagizaji, lakini wamekuwa wana-delay kwenye kuagiza sukari kwa wakati kwa sababu ambazo wao wanazijua ili sukari hii iadimike na waweze kufanya biashara kubwa kwenye suala la sukari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili halikubali, halikubali kabisa kwa sababu inavyooneka sasa hivi ni suala la masikio kuzidi kichwa hatuwezi kuendeshwa katika nchi hii na watu saba ambao wao ni matajiri wawekezaji wa sukari kwenye eneo hilo… (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante, naomba hitimisha.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: …kiasi ambacho sasa wanaweza ku-drive nchi hii na wa wakatupangia bei kwenye eneo hili. Suala hili halikubaliki na kwa sababu umeninyima muda nafikiria kama niunge mkono hoja. (Makofi/Kicheko)